![]() |
| Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Michael Mhando |
BAADHI ya wananchi wameitaka serikali
kuwachukulia hatua za kisheria watendaji wa hospitali wanaojihusisha na vitendo
vya kuwauzia damu wagonja.
Walisema hivyo jiji Dar es Salaa jana wakati
wakitoa maoniyao kuhusu uhaba wa damu salama uliojitokeza katika hospitali
nchini.
Walisema hali hiyo imekuwa kikwazo kikubwa
kinachowafanya baadhi yao waone kuwa hakuna haja ya kuchangia damu.
Wanachi hao walisema wamekuwa wakijitolea katika
kuchangia damu kwa ajili ya wagonjwa, lakini wagonjwa wanapopelekwa katika
baadhi ya hospitali wahudumu huwauzia damu hiyo, kitendo ambacho kinawashangaza.
Walisema wakati umefika sasa kwa serikali
ikishirikiana na wakuu wa hospitali hizo kuweka mkakati wa kuzuia vitendo hivyo
ili kurudisha imani kwa wachangiaji damu.
Wakati hali ikiwa hivyo, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya
na Ustawi wa Jamii kupitia Mpango wa Taifa wa Damu Salama, utaendesha shughuli
ya upimaji wa afya na kukusanya damu salama katika mikoa sita.
Kwa mujibu wa Kaimu Mkurugenzi Mkuu
wa NHIF, Michael Mhando, hatua hiyo inalenga kupunguza uhaba wa damu salama kwa
matumizi ya wagonjwa nchini na wakati huo huo kuwawezesha wananchi kujua afya
zao na hivyo kuchukua hatua stahiki mapema.
Mhando alisema hatua hiyo imefikiwa
baada ya kuwepo kwa uhaba wa damu salama katika vituo mbalimbali vya matibabu
nchini, ambavyo vingi vinahudumia wanachama wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya.
“Tumetaarifiwa na wenzetu wa Damu Salama kuwa mahitaji ya damu salama nchini ni
chupa 400,000 hadi 450,000 kwa mwaka ambayo ni sawa na wastani wa chupa 106,000
za damu kwa robo mwaka,” alisema Mhando na kuongeza:
“Hata hivyo, kutokana na kutofikia
kiwango hicho, Mpango wa Damu Salama Tanzania ulijiwekea lengo la kukusanya
chupa 150,000 kwa kipindi cha mwaka jana ambayo ni sawa na lengo la kukusanya
chupa 37,500 kwa mwaka.
“Hili ni suala la dharura na linahitaji hatua
za haraka na ushirikiano miongoni mwa wadau wa sekta ya afya na wananchi kwa
ujumla,” aliongeza mkurugenzi huyo wa NHIF. Alisema takwimu zinaonesha kuwa
kiasi cha chupa 19,000 za damu salama zilikusanywa katika kipindi cha robo
mwaka cha Oktoba - Desemba 2014, wakati ambapo chupa 150,000 zimekusanywa kwa
kipindi cha kuanzia Januari 2015 hadi sasa.
“Hii inaonesha wazi kuwa upo uhaba
mkubwa wa damu kulinganisha na uhitaji uliopo hasa katika vituo vikubwa mfano
Muhimbili ambapo zinahitajika chupa 50 hadi 60 za damu kwa siku,” aliongeza
Mhando.
Alisema kutokana na umuhimu wa suala
hilo, NHIF umeona ni vyema kuunga mkono juhudi za Serikali katika kipindi cha
uhaba mkubwa wa damu salama kwa kushirikiana na Taasisi ya Mpango wa Damu
Salama na wadau wengine kwa kufanya zoezi la ukusanyaji wa damu kutoka kwa
uchangiaji wa hiari wa wananchi.
Alisema shughuli hiyo itaanza Machi
23, mwaka huu kwa muda wa siku tano katika mikoa ya Dar es Salaam ambayo
itakuwa katika vituo vya stendi ya Gongo la Mboto, Mbagala, Banana, Buguruni,
Karume Sokoni na Mlimani City.
Mikoa mingine na vituo vyao katika
mabano ni Mwanza (stendi ya Igoma, Pasiansi, Nyegezi, Buswelu Center, Buhongwa
Center), Mbeya (viwanja vya shule ya msingi ya Mwegeishi na Gombe, Mbata na
Rundazove, stendi ya Mbalizi na Uyole), Kilimanjaro, Moshi (stendi Mwika, Soko
la Chekereni (Kahe), Kwa Sadala (Hai), Soko la Lawate (Siha) na Soko la Kwa
Mangula (Rombo).
Mingine ni Tabora (viwanja vya Ndala
TTC, Urambo Center, Urambo Center, Kaliua Center, Usoke Center na Town Center
na Mtwara (Hiyari Center, Nanyamba Center, Naliendele Center na Umoja na
Mikindani Center).
Kwa mujibu wa Kaimu Mkurugenzi Mkuu
wa NHIF, wanatarajia kuwa wananchi 6,000 watajitokeza kuchangia damu na wao
wenyewe katika Mfuko huo watakuwa miongoni mwa washiriki wa kwanza kuchangia.
Kwa upande wake, Meneja Masoko na
Mawasiliano wa Mpango wa Taifa wa Damu Salama, Rajab Mwenda alisema uchangiaji
wa damu hauna madhara yoyote na kuwataka Watanzania kujenga utamaduni wa
kuchangia damu ili kuokoa maisha ya wenzao wenye uhitaji wa damu ili kuokoa
maisha yao.

No comments:
Post a Comment