| Rais Kikwete akiwa katika picha ya pamoja na Makamishna, aliyowaapisha jijini Dar es Salaam jana. |
RAIS Jakaya Kikwete amewataka makamishna wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), kwenda kutumia uzoefu walionao katika kuipatia ufumbuzi migogoro inayojitokeza katika sehemu za kazi.
Kikwete alitoa kauli hiyo katika viwanja vya Ikulu jijini Dar es Salaam jana baada ya kuwaapisha makamishna hao akiwemo mwenyekiti wa tume hiyo.
Alisema anaamini kuwa makamishna hao wanao uwezo wa kuamua migogoro inayojitokeza kati ya mwajiri na mwajiriwa pindi wanaposhindwana.
Makamishna walioapishwa ni Idris Mavura, ambaye ni Mwenyekiti, Jafari Omar na Saulu Kihemela. Wengine ni Suzan Ndomba, Njaa Ramadhan, Johnes Majura na Mathias Kabunduguru.
Mwenyekiti wa Tume hiyo, Mavura, alisema: “Nitakapofika ofisini nitafanya kazi kwa kuanzia walipofikia watangulizi wangu, kwani najua walifanya kazi nzuri hadi kupunguza migogoro hiyo kati ya waajiriwa na waajiri.”
Mavura alitoa wito wa kuwataka waajiri na waajiriwa kwamba ili kusiwepo na migogoro, ni vema kila mmoja akazingatia sheria na kanuni za kazi, kwani kwa kufanya hivyo anaamini migogoro itapungua.
Kwa upande wao makamishna wa tume hiyo, walisema tume hiyo inatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sera na sheria na kwamba wamejipanga kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu kama sheria inavyowaelekeza.
No comments:
Post a Comment