KAMPUNI ya IPTL na PAP imesaidia kampeni ya kupinga mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) inayojulikana kama ‘Imetosha’ iliyoanzishwa na Balozi wa kujitolea, Henry Mdimu, kwa kutoa sh. milioni 10.
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi hundi ya fedha hizo jijini Dar es Salaam juzi, Katibu na Mshauri Mkuu wa Sheria wa makampuni ya IPTL na PAP, Joseph Makandege, alisema matukio ya mauaji kwa albino yamefika hatua ya kutisha hususan katika Kanda ya Ziwa, hivyo kuna kila sababu kila mmoja kushiriki kusaidia mapambano hayo.
Alisema ulemavu wa ngozi walionao watu ni upungufu wa kibaiolojia ambao ni mapenzi ya Mungu, hivyo imani potofu zinazoendelea hazina budi kupigwa vita.
“Kuna minong’ono mitaani kwamba watu wanaotenda matukio hayo wana imani potofu kwamba ukitumia kiungo cha albino utafanikiwa.
Kama kweli viungo vyao vingekuwa vinaleta utajiri, basi watu wenye ‘ualbino’ wangekuwa matajiri namba moja duniani,” alisema Makandege.
Mratibu wa kampeni hiyo, Mdimu, aliishukuru Kampuni ya IPTL na PAP kwa moyo waliouonyesha wa kusaidia harakati hizo na kumtaka kila Mtanzania kwa nafasi yake kusaidia kupaza sauti kwamba ‘imetosha’ mauaji na unyanyasaji wanaoupata watu wenye ‘ualbino’.

No comments:
Post a Comment