![]() |
| Kamanda Msangi |
MTOTO Johnson Mwamwele (5), mkazi wa Kata ya Nsalaga jijini Mbeya, amekufa papohapo baada ya kukatwa kichwa na mjomba wake, Yonah Mwamwele (38) kwa kutumia sururu na kutenganisha kichwa na kiwiliwili.
Baada ya kitendo hicho cha kinyama, wananchi wenye hasira waliamua kumkimbiza mtuhumiwa huyo na kumkamata, kumpiga na kisha kumuua kwa kumchoma moto.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ahmed Msangi alisema, lilitokea jana saa 5:30 asubuhi katika eneo hilo.
Kamanda Msangi alisema, kabla ya mtuhumiwa huyo kutenda mauaji hayo ya kinyama, alionekana akimkimbiza mtoto huyo ambaye ilibanika kuwa ni mpwa wake hadi kwenye nyumba inayoendelea kujengwa iliyopo mtaani hapo.
Kamanda Msangi alisema, mafundi waliokuwa wakiendelea na ujenzi wa nyumba hiyo walimsihi mtuhumiwa huyo ili amwache mtoto huyo lakini aliwatisha kwa sururu hiyo kitendo kilichowaogopesha mafundi hao na kulazimika kurudi nyuma.
Kwa mujibu wa Msangi, baada ya kuingia ndani ya nyumba hiyo, Mwamwele alimfuata moja kwa moja mtoto huyo na kumpiga sururu ya shingo, iliyotenganisha kichwa na kiwiliwili chake na kufariki dunia papohapo.
Alisema kuwa baada ya mafundi hao kushuhudia kitendo hicho walipiga yowe ya kuomba msaada, ambapo ghafla kundi kubwa la watu lilijitokeza na kuanza kumkimbiza mtuhumiwa huyo na kufanikiwa kumkamata, kumpiga na kisha kumchoma moto hadi kuteketea.
“Baada ya kukamilisha mauaji hayo ya Mwamwele, wananchi hao wenye hasira walirudi kwenye nyumba hiyo na kuanza kuipiga mawe na kuvunja vioo vyote, wakilaani mauaji hayo ya mtoto huyo kufanyika humo na kukosa msaada,” alisema.
Kamanda Msangi alisema, upelelezi unaendelea ili kuweza kubaini chanzo cha mtuhumiwa huyo kufikia uamuzi wa kumkata kichwa mtoto huyo.
“Kimsingi tunaendelea na upelelezi ili kuwabaini wale wote walioamua kujichukulia sheria mkononi kwa kumuua mtuhumiwa, kwani ni mahakama pekee ndiyo yenye uwezo wa kutoa adhabu na siyo nje ya hapo,” alisema.
Tukio hili limetokea ikiwa ni takribani mwezi mmoja na wiki mbili na nusu tangu kutokea kwa tukio la kuuawa kwa askari PC Joseph Isack Swai ambaye alikwenda kumwokoa mtoto wa miezi minane aliyekuwa akiteswa na baba yake mkoani Dodoma.
Askari huyo ambaye alilazimika kumrukia mtoto huyo na kwa bahati mbaya aliteleza na ndipo mtuhumiwa akamkata kichwani na kupoteza damu nyingi na kufariki dunia.
Hata hivyo mtuhumiwa huyo alitoweka baada ya kufanya kosa hilo hatua iliyolazimu wananchi kumsaka na kufanikiwa kumkamata, kumshambulia na kumuua.
Mwisho..

No comments:
Post a Comment