KAMA UNA TUKIO LOLOTE LA KIJAMII, SIASA, UCHUMI TUWASILIANE KWA E-mail: shehesemtawa@gmail.com SIMU: 0719 352 268

Sunday, 15 March 2015

KINYAFU: NGUZO TISA ZA UMEME ZIKO NDANI YA BARABARA SARANGA ARSENAL

Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Mussa Natty
DIWANI wa Kata ya Saranga wilayani Kinondoni, Ephraim Kinyafu, amemtaka Mhandisi wa Manispaa hiyo kutoa maelezo kutokana na kushindwa kuhamisha nguzo tisa za Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), ili kupisha ujenzi wa barabara ya Saranga Arsenal.

Kinyafu, alisema Tanesco iliingia makubaliano kwamba kabla ya ujenzi wa barabara hiyo kuanza Manispaa hiyo itafute mkandarasi wa kuhamisha nguzo hizo, ambaye gharama zake ingezilipa.

Alisema, sasa ni zaidi ya miezi mitatu nguzo hizo hazijahamishwa hali iliyoifanya Kampuni ya Ujenzi wa Barabara hiyo Skol (SBC), kuwamua kujenga huku nguzo hizo zikiwa robo tatu ndani ya barabara jambo ambalo ni la hatari.

Kinyafu, alisema hayao jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, wakati alipofanya ziara ya kushtukiza ya kukagua maendeleo ya mradi huo ambao ulianza mwishoni mwa mwaka jana.

Alisema, hivyo kwa vile aliwasiliana na Tanesco ambayo ilimjibu kuwa tatizo la kuhamishwa nguzo hizo haliko kwao wanachosubiri wao ni utekelezaji wa malipo kwa mkandarasi atakayepewa zabuni hiyo kama ilivyokubaliana awali na Manspaa hiyo.

Kinyafu alisema licha ya makubaliano hayo, hadi sasa hakuna taarifa ambazo zimetolewa na ofisi ya mhandisi wa Manispaa hiyo kwamba ni sababu zipi zilizofanya wachelewe kumpata mkandarasi wa kuhamisha nguzo hizo tisa.

“Hii ni hatari kwa nguzo za umeme kusimama katikati ya barabara tunaweza kujakupata janga kubwa ambalo linaweza kugharimu roho za watu na uharibifu wa mali na serikali kuingia gharama kubwa katika kuwadumia waathirika,”alisema Kinyafu.

Msimamizi wa Kampuni ya SBC, Efard Benson, alisema wameamua kujenga huku nguzo hizo zikiwepo kwa sababu taratibu kwa upande wao zilikuwa zimekamiliaka tangu mwishoni mwa mwaka jana na istoshe wanakwenda na wakati.

Alisema, kama wangeendelea kusubiri kuhamishwa nguzo hizo ina maana hadi leo wangekuwa hawajaanza ujenzi kitendo ambacho kingewaongezea gharama zisizo za lazima.

“Kweli uwepo wa nguzo zile ndani ya barabara ni kikwazo pia tayari kumekwishatokea ajali mara mbili kwa magari kuzigonga na kusababisha taharuki kwa nguzo hizo kuanguka barabarani pia wananchi kuosa huduma hiyo kwa zaidi ya siku moja,” alisema Benson.


Benson, alimuomba diwani, kwamba aendelee kutia msukumo katika kuhamishwa nguzo hizo kwani tangu hiyo barabara ilipoanza kujengwa kwa kiwango cha lami magari mengi yanapita, akibainisha kuwa uwezekano wa kutokea ajali ni mkubwa kama hazitahamishwa haraka.

No comments:

Post a Comment