KAMA UNA TUKIO LOLOTE LA KIJAMII, SIASA, UCHUMI TUWASILIANE KWA E-mail: shehesemtawa@gmail.com SIMU: 0719 352 268

Friday, 13 March 2015

MECK SADIK AITAKA NPS KUFANYAKAZI KWA UELEDI

Mkuu wa Mkoa, Sadik
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki ameitaka Kampuni inayojishughulisha na maegesho ya magari ya ‘National Parking System’(NPS), kufanya kazi zake  kwa umakini ili kuondoa dosari katika suala zima la ukamataji wa magari katika Jiji la Dar es salaam.
 
Sadiki ametoa rai hiyo Jijini Dar es salaam leo, huku akiipongeza kampuni hiyo inayoendelea na jukumu hilo la ukamataji magari yanayoegeshwa kimakosa katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es salaam,jukumu ambalo pia lilikuwa likifanywa na Kampuni ya Tambaza Auction Mart ambayo mkataba wake ulisitishwa na Manispaa ya Ilala.
 
Alisema ni NPS ikajielekeza katika kufanya kazi zake kwa weledi  hatua itakayosaidia kuondoa malalamiko yanayotokana na kero mbalimbali walizokuwa wakizipata wenye magari kutoka kwa kampuni zilizokuwa zimepewa jukumu hilo jambo lililomfanya kuziagiza halmashauri kusitisha  mkataba iliokuwa imeinga nazo.
 
“Litakuwa jambo la busara kama kampuni hii ambayo ipo kwa muda mrefu katika shughuli hii  itafanya kazi zake kwa kujielekeza katika maeneo yanayowahusu kisheria ili kuondoa uwezekano wa uwepo wa malalamiko yasiyo ya lazima kutoka  kwa wananchi” alisema Sadiki
 
Alisema kimsingi majukumu yote ya kampuni hiyo ya NPS na utendaji wake wa kazi yanatambuliwa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Jiji la Dar es salaam kwa kuwa ndiyo iliyoingia mkataba na kampuni hiyo katika utekelezaji wa majukumu yake likiwemo la uegeshaji wa magari.
 
Mapema mwaka huu Mkuu huyo wa mkoa wa Dar es salaam aliziagiza manispaa za Ilala na Kinondoni kuvunja mkataba na kampuni za udalali za Tambaza Auction Mart na Mwamkinga pamoja na Yono zilizokuwa zimepewa jukumu la ukamataji magari
 
Hatua hiyo ilifuatia utendaji wa kampuni hizo na hasa baada ya kudaiwa kuwa kero kwa watumiaji wa barabara jambo lililozifanya kulalamikiwa na wananchilicha ya viongozi wake kupewa karipio na serikali zaidi ya mara tatu kuhusu kuboresha huduma zake.
 
Baadhi ya malalamiko hayo ni pamoja na vitendo vya ubabe kutoka kwa wafanyakazi wa kampuni hizo,rushwa pamoja na faini zilizopitiliza pindi wanapokamata magari hayo.
 
Inadaiwa wamiliki wa gari zinazokamatwa hutakiwa kulipa Sh. 45,000,  fedha za faini ya Jiji,  wakati kampuni hiyo ikihitaji kulipwa zaidi ya Sh  105,000 za ‘brake down’ na ukamataji,  na anayeshindwa kulitoa gari kwa siku hiyo hutakiwa kuendelea kulipa Sh. 29,000, kwa siku hadi atakapolichukua.

No comments:

Post a Comment