KAMA UNA TUKIO LOLOTE LA KIJAMII, SIASA, UCHUMI TUWASILIANE KWA E-mail: shehesemtawa@gmail.com SIMU: 0719 352 268

Wednesday, 18 March 2015

MBAGA: MAONYESHO YA UWEKEZAJI YATATOA MSUKUMO KWA WAWEKEZAJI

KAMPUNI ya Mawasiliano na Masoko ya East  Africa Unique, inaandaa maonyesho ya uwekezaji  ili kuweka msukumo wa uwekezaji.
Maonyesho hayo yatafanyika katika Hoteli ya Golden iliyopo jijini Dar es Salaam kuanzia Mei 3 hadi Juni 4 Juni mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo, Rodgers Mbaga alisema maonyesho hayo kampuni yake imepanga na kuweka mikakati ya kuhakikisha biashara endelevu kwa kuandaa mafunzo ya kuwajengea uwezo wenye miradi.

"Katika maonyesho hayo  mafunzo yatakayotolewa ni pamoja na  kutayarisha miswaada, mapendekezo ya miradi  ambayo inawavutia wawekezaji  na watoaji wa mitaji," alisema.

Mbaga alisema mafunzo mengine ni uendeshaji wa miradi, usimamizi wa fedha  na kufuata taratibu, uuzaji na utafutaji wa masoko, mbinu za mawasiliano  na namna ya kushawishi wawekezaji na watoaji mitaji kukubali miradi inayopendekezwa.

Aliongeza kuwa wataangalia namna ya kufikiri, kuongeza  upeo wa kulenga miradi  ya wastani  isiyopungua dola za Marekani laki mbili na nusu, kuwa waaminifu na kujituma kulingana na uwezo na ukomo wao.

"Watakaoshiriki TIPEC ni  sekta binafisi (TPSF), Baraza la biashara la  kitaifa (TNBC), Mamlaka ya Export Processing Zone (EZPA), Mamlaka ya maendeleo ya biashara Tanzania (TANTRADE), Taasisi za wenye viwanda  na biashara biashara (TCCIA) na Shirikisho la wenye viwanda Tanzania (CTI)," alisema.


Aliongeza kuwa kuanzia mwaka 2016 TIPEC itatembelea nchi zisizopungua  mbili  ili kukuza miradi ya mahususi ya biashara.

No comments:

Post a Comment