KAMA UNA TUKIO LOLOTE LA KIJAMII, SIASA, UCHUMI TUWASILIANE KWA E-mail: shehesemtawa@gmail.com SIMU: 0719 352 268

Tuesday, 17 March 2015

NSSF YANUFAISHA WAKULIMA

Mbunge wa Mbinga, Kayombo
NA MWANDISHI WETU

MKOPO wa sh. bilioni mbili uliotolewa na Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF), kwa wakulima wa zao la Kahawa wilayani Mbinga, umesaidia kwa kiasi kikubwa wakulima hao kuongeza uzalishaji na kukuza vipato vyao.
 Mbunge wa Mbinga Mashariki, Gaudens Kayombo, alieleza hayo mjini hapa jana alipozungumza na waandishi wa habari.
 “Asilimia 90 hadi 95 ya wananchi wa wilaya ya Mbinga ni wakulima na mkopo huu umesaidia kukuza vipato vyao kupitia zao la kahawa,”alisema.
 Alisema mwaka jana waliingia mkataba na NSSF na vyama vya msingi vinne kufanikiwa kupata mkopo na  kununua zao hilo kutoka kwa wakulima na ndani ya siku 100 walikamilisha kulipa mkopo huo.
Pia alisema mkopo huo ulifuta mfumo holela wa ununuzi wa zao hilo ambapo wakulima walikuwa hawapati faida ya kutosha.
 Alizitaka kampuni za watu binafsi zinazonunua zao hilo wilayani hapa kuangalia wakati wa kununua zao hilo, ili wakulima nao waweze kufaidika.
  “Katika kipindi cha miaka tisa na zaidi kuna maendeleo makubwa yamepatikana chini ya kaulimbiu ‘Mbinga Mbinguni’,” alisema na kuongeza kuwa wanatarajia Mbinga iwe mfano wa wengine kuiga.

No comments:

Post a Comment