KAMA UNA TUKIO LOLOTE LA KIJAMII, SIASA, UCHUMI TUWASILIANE KWA E-mail: shehesemtawa@gmail.com SIMU: 0719 352 268

Sunday, 8 March 2015

STAR TIMES INAKABILIANA NA CHANGAMOTO ZA MIUNDOMBINU



KAMPUNI binafsi inayoshughulikia mawasiliano ya habari kwenye mtandao wa televisheni ya dijitali, Star times inakabiliana na changamoto za miundombinu hafifu na umbali wa maeneo katika zoezi la kusimika mitambo.

Akizungumzia suala hilo, Mkurugenzi wa Uhusiano wa Umma wa Kampuni hiyo,  Zuhura Hanif alisema anaipongeza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), kwa kuzima mitambo ya analojia ili kufanya mabadiliko makubwa ya matangazo ya luninga na pia kuelezea changamoto wanazokumbana nazo kama kampuni.

Alisema, kampuni hiyo ipo katikia wakati mgumu wa kuwafikia wateja popote walipo kwani huduma zao zinahitajika sana, hasa maeneo ya vijijini.

“Tanzania ni nchi kubwa sana yenye ukubwa wa kilometa za mraba takribani laki tisa na nusu, mikoa 26 na wakazi takribani million 44 kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi iliyofanyika hivi karibuni, hivyo tatizo kubwa tunalokumbana nalo ni miundombinu hafifu na umbali wa maeneo hayo katika zoezi la kusimika mitambo yetu kuwa mgumu kidogo lakini tunapambana kufanikisha hilo,”alisema Hanif.

Akizungumzia hatua ya uzimaji wa mitambo hiyo, alisema Tanzania ni nchi ya kwanza barani Afrika kuzima mitambo ya utangazaji wa luninga kwa mfumo wa analojia na kuhamia dijitali, zoezi ambalo lilianza mapema mwa mwezi Disemba 31 mwaka 2013.

“Uzimaji wa mitambo ya analojia ni fursa kubwa kwa watazamaji wa luninga kwani unawapa matangazo bora na yenye uangavu tofauti na mfumo wa awali, pia matangazo hayo watazamaji wanaweza kutazama chaneli na programu nyingi zenye maudhui mbalimbali yenye kukidhi haja ya kila mmoja wapo,”alisema.

Hata hivyo, Hanif alieleza kuwa kabla ya kuzimwa kwa mitambo hiyo, kulikuwepo na changamoto kwa watazamaji kutokana na hofu juu ya masuala mbalimbali ambayo walidhani yangeweza kukwamisha zoezi hilo.

“Wapo waliofikiria Tanzania bado hatuko tayari kwani kiteknolojia tuko nyuma, uchumi wetu ni mdogo, hakuna wawekezaji wa kutosha kutoa huduma hii, upatikanaji wa visimbuzi, gharama kubwa za visimbuzi, elimu ya kutosha kwa watumiaji na kadhalika, l
akini tofauti na ilivyotarajiwa, mitambo ilizimwa na kwa awamu katika maeneo ambayo yamewekewa miundombinu ya mfumo wa dijitali,”alisema.

Alieleza kuwa mafanikio makubwa yameonekana katika maeneo ambayo mitambo ya analojia ilizimwa na wakazi wake kuhamia katika dijitali, ambapo wananchi wameipokea vizuri huduma hiyo kwani miundombinu ilikuwa tayari imekwishaandaliwa ili kuondokana na usumbufu wa aina yeyote.

“Kwetu sisi kama wawekezaji zipo changamoto ambazo tumekumbana nazo na tunaendelea kukumbana nazo, lakini kwa ushirikiano wa karibu na serikali mambo yanakwenda vizuri,”alisema.

No comments:

Post a Comment