KATIBU Mkuu wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, amesema chama hicho kipo
hatua za mwisho kufungua kesi ya madai dhidi ya mtu anayedaiwa kumiliki eneo
walipo Umoja wa Mafundi Gereji, Tegeta, jijini Dar es Salaam.
Eneo hilo maarufu kama Tegeta
Magereji limeingia katika mgogoro kati
ya mafundi hao na mtu anayedaiwa kuwa mwekezaji baada ya kudai kuwa eneo hilo
ni lake.
Hata hivyo, mafundi hao
wanapinga kuondoka katika eneo hilo kwa madai wanatambulika kisheria.
Akizungumza na waandishi wa
habari jijini Dar es Salaam leo, Dk. Slaa alisema kwa sasa wanaendelea kulifuatilia
suala hilo na kwamba wahusika wakuu ni wanasheria wa chama hicho.
“Ni kweli tunaendelea
kulifuatilia kwa kina suala hilo na kwa sasa tumewaachia wanasheria wetu hasa
Mallya (John Mallya) ambaye ndiye anashughulikia suala hilo kisheria,” alisema.
Kwa upande wake, Mwanasheria
wa Chadema, John Mallya, alisema wamekamilisha kila kitu na wanachosubiri ni
baadhi ya masuala kukamilika ili wafungue kesi ya madai Mahakama Kuu.
“Tutafungua kesi ya madai
Mahakama Kuu kwani wateja wetu si walioshitakiwa mahakamani na sisi tumepitia
kila kitu na tumejiridhisha kuwa wao hawakupaswa kufunguliwa kesi, sasa sisi
tutafungua kesi ya madai dhidi ya wahusika,” alisema Mallya.
Mafundi hao zaidi ya 4,000
wanatakiwa kuhama eneo hilo kutokana na mtu anayedaiwa kumilikia eneo hilo
kufungua kesi mahakamani ambapo alishinda kesi hiyo.

No comments:
Post a Comment