MHARIRI Mtendaji Mstaafu wa Kampuni ya Free Media,
inayochapisha magazeti ya Tanzania Daima na Sayari, Ansbert Ngurumo, leo aliwaaga
rasmi wafanyakazi wa kampuni hiyo, huku akiwaasa kuendelea kutetea haki za
wanyonge bila kujali itikadi za kidini au za kisiasa.
Ngurumo, ambaye ni mmoja wa wahariri waanzilishi wa
gazeti hili, amekaa katika kampuni hii kwa miaka 10 na miezi miwili; aliwaasa
waandishi wasiyumbe na kuacha dhima ya kuwasemea wananchi wasio na sauti, na
kutetea wanaodhulumiwa haki zao, kazi ambayo imelitambulisha Tanzania Daima
katika jamii.
Ngurumo, ambaye ni mmiliki wa Kampuni ya Vox Media na
mwandishi wa safu ya Maswali Magumu katika Tanzania Daima Jumapili, aliwataka
waandishi kuandika habari kwa weledi na ujasiri, bila kuonea au kuogopa mtu
yeyote, kwani kazi wanayofanya ina mkono wa Mungu.
Alisema gazeti la Tanzania Daima linaaminika kwa
kusimamia ukweli na kutetea wanyonge ambao hawana pengine pa kukimbilia.
“Naamini gazeti hili litaendelea kuwepo na kutetea
wanyonge wasiokuwa na fedha wala madaraka bila ya kujali itikadi; lakini pia
litetee wenye uwezo na madaraka wanaoonewa na mifumo,” alisema.
Akizungumza katika ofisi za gazeti hili, Ngurumo alisema awali
alipanga kuwaaga wafanyakazi hao Januari 7, mwaka huu, lakini alichelewa
kutokana na mazingira magumu aliyokuwamo kifamilia na kiafya, hasa baada ya
kufiwa na binti yake mwishoni mwa mwaka jana.
Ngurumo, alikuwa anasumbuliwa na maumivu ya mgongo kiasi
kwamba asingeweza kusafiri kwa muda mrefu kutoka Kamachumu hadi Dar es Salaam,
hadi alipopata nafuu.
“Siondoki ghafla, lazima na hili lieleweke. Nimeondoka
baada ya mipango ya muda mrefu, na kwa kuwa huu ni mwaka wa uchaguzi, ilibidi
nichague moja kati ya mawili; nikaamua niache ofisi ili nikajiandae kwa uchaguzi,”
alisema Ngurumo.
Akizungumzia maisha yake nje ya chumba cha habari,
Ngurumo alisema kwa sasa anafanya kazi ya ushauri wa kitaalamu katika habari na
mawasiliano, biashara na intelijensia ya kisiasa.
Kuhusu sisasa
Ngurumo alisema alianza kuandaa chama kwa uchaguzi tangu Juni
mwaka 2011 katika jimbo la Muleba Kaskazini, akishirikiana na viongozi na
wanachama katika kuinuia chama kilichokuwa kimedorora.
“Nilikuta chama kimedorora, hakifanyi vikao vya ndani;
hakifanyi mikutano ya hadhara katika maeneo mengi, hakina msingi hata mmoja,
hakina uongozi uliochaguliwa... sasa hivi kina misingi zaidi ya 200, kina
uongozi uliochaguliwa kikatiba jimbo zima, mikutano mikubwa ya hadhara
inafanyika tangu mwaka 2012.
“Na katika matokeo ya uchaguzi, tumegawana jimbo na CCM. Miongoni
mwa vijiji 64, tumechukua 27, na miongoni mwa vitongoji 285, tumechukua 147.
Kwa hiyo, nakwenda kushirikiana na wenzangu kuimarisha msingi tuliokwisha kuujenga
ili tufanye vizuri zaidi katika Uchaguzi Mkuu,” alisema.
Aidha, alisema kwa vile ameamua kuingia kwenye siasa,
ameamua kwenda kujikita jimboni ili aweze kushirikiana na wananchi kuimarisha
shughuli zake za kisiasa.
Ingawa hajatangaza rasmi, Ngurumo anatarajiwa kuwania
ubunge katika Jimbo la Muleba Kaskazini kupitia Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema), na anasubiri mchakato rasmi ili atimize azima yake hiyo.
Alisema katika Jimbo la Muleba Kaskazini mchuano ni kati
ya CCM na Chadema, kwani vyama vingine havina mizizi.
Alimshukuru Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, kwa
ushauri na malezi mazuri aliyompa kibiashara na kisiasa, kwa zaidi ya miaka 10
mfululizo, na kwamba atatumia stadi hizo kufanya siasa za kizalendo, zenye
msimamo na kwa uaminifu mkubwa.
Pamoja na siasa, Ngurumo anajiandaa kuchapisha kitabu cha
Maswali Magumu, ili kusaidia wananchi kutathmini utendaji wa Serikali ya Awamu
ya Nne, chini ya Rais Jakaya Kikwete, kama sehemu ya elimu ya uraia kwa Watanzania. CHANZO TANZANIA DAIMA
No comments:
Post a Comment