NA
ANDREW MSECHU
KATIBU
Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa amesema Tanzania imedumaa kutokana na Chama
Cha Mapinduzi (CCM) ambacho kimetawala kwa miaka zaidi ya 50 kushindwa
kurutubisha rasilimali kwa manufaa ya wananchi na kwamba njia pekee ya
kulikomboa taifa ni kukiondoa madarakani
kupitia sanduku la kura.
Dk.
Slaa alisema CCM ni sawa ni saratani inayolitafuna taifa, kutokana na serikali
yake kukosa maadili na kukumbatia makundi ya wahalifu waziwazi bila hata kuona
aibu, huku wananchi wake wakiendelea kuteseka na kwamba Watanzania wameendelea
kuwa wabeba mizigo badala ya kuwa washindani katika uchumi wa dunia.
Akiwahutubia
mamia ya wanazuoni katika Chuo Kikuu cha Purdue, nchini Marekani, Dk. Slaa alisema
njia pekee ya kulinusuru taifa na saratani hiyo, ni kuleta mabadiliko ya kweli
kupitia sanduku la kura na kwamba tiba ni kumpata rais atakayetokana na vyama
vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
“Bila
shaka, haya ni mambo muhimu ambayo yanahitaji tuyazungumze sisi kama
Watanzania kwa kushirikiana na wadau
wetu na marafiki kama nyie.
Tunahitaji
msaada wenu katika kukabiliana kuiondoa saratani hii CCM ili tuijenge jamii
yetu kiuchumi,”alisema Dk. Slaa.
Alisema
Tanzania ni maskini na kwamba watu wake ni maskini pia lakini jambo la
kushangaza ni kwamba Rais Jakaya Kikwete aliwahi kusema hadharani kwamba hajui
chanzo cha umaskini wa wananchi wake, kauli ambayo Dk. Slaa alisema ililenga kuficha
ukweli wa ubadhirifu mbele ya mataifa ya nje.
“Mlishuhudia
taarifa za kusikitisha sana na za aibu kutoka kwa mkuu wa nchi. Labda rais
alikuwa akiona aibu kuuambia ukweli ulimwengu, kwamba kwa miaka 54 nchi inaugua
saratani inayoitwa Chama Cha Mapinduzi,”alisema Dk. Slaa na kuongeza:
“Hii
ni saratani ya kisiasa tangu kuanzishwa kwa taifa, chama ambacho kimekuwa
kinara wa rushwa na ubadhirifu, ambacho kimekuwa hakina muda wa kuangalia namna ya kuinua uchumi, zaidi
kinaangalia namna ya kuomba misaada badala ya kuangalia namna ya kuboresha
uzalishaji na uimarishaji wa rasilimali za taifa.”
Dk.
Slaa alisema ni wazi saratani hiyo imeshalitafuna taifa kiasi cha kutosha na
hata kusahau ilipoanzia na kwamba imelifanya kuwa miongoni mwa nchi maskini
duniani kwa makusudi, hivyo njia pekee ya kuondokana na tatizo hilo ni
kuhakikisha inaondolewa kwa kura.
Alisema
chama hicho tawala kimekuwa kikwazo cha ukuaji wa uchumi kwa kuua ubunifu wa
ndani na badala yake kimetengeneza mfumo wa
kuingiza bidhaa hatari zisizokuwa na viwango kutoka mashariki ya mbali.
Aliongeza
kuwa serikali imejaa viongozi wanaopandikiza mbegu ya ukabila kwa wananchi ili
kutumia mwanya wa kugawanyika kwao kuwatawala, bila kujali athari za baadaye za
mgawanyiko huo.
“Ni
Tanzania pekee ambapo kutokana na utawala dhalimu wa CCM, maskini aliyeiba
mbuzi kwa ajili ya kuinusuru familia yake na njaa anaweza kufungwa jela, lakini
muuza dawa za kulevya, wahalifu wa kiuchumi na majangili (wauaji wa tembo)
wanalindwa kwa gharama zote na CCM. Wale wanaoiba mabilioni ya fedha za umma
wanatembelea magari na kupata ulinzi wa serikali,” alisema.
Katika
hotuba yake hiyo, Dk. Slaa alisema ni Tanzania pekee ambayo wale wanaopigania
masilahi na kuangalia namna ya kulinda rasilimali za nchi wanaitwa ‘magaidi’ na
kwamba CCM kimekuwa kikitumia polisi na vyombo vya usalama si kulinda rais na
mali zao, bali kukandamiza haki za wananchi.
“…ukiwa
mwanachama wa upande wa upinzani, wewe ndiye shabaha ya kwanza ya askari polisi
na adui namba moja wa dola,”alisema.
Dk.
Slaa alisema katika miaka yote ya utawala wake, serikali ya CCM imekuwa kikwazo
cha Tanzania kuingia katika mapinduzi ya viwanda na kwamba imeua ndoto za mapinduzi
ya kilimo.
Alisisitiza
kwamba CCM ni chanzo cha kuharibika kwa huduma hata za afya, elimu na kufa kwa
uchumi, mambo ambayo alisema yamekuwa kichocheo kikubwa cha kuwageuza wananchi
na taifa lao kuwa wategemezi wa misaada na ombaomba, badala ya kuwa washiriki
katika uchumi wa kimataifa.
Uhuru wa habari
Dk.
Slaa ambaye yuko katika ziara ya kikazi ya siku tisa nchini Marekani, pia
alizungumzia uhuru wa habari nchini akisema
hali siyo nzuri kwani baadhi ya magazeti yamekuwa yakiandamwa na mengine
kufungiwa kwa sababu ya kuanika uovu wa serikali na mengine kufungiwa kwa
sababu ya kuchora vikaragosi tu.
Alisema
baadhi ya waandishi wa habari wamekuwa wakikamatwa, kutishwa na hata kuuawa kikatili
na vyombo vya usalama, pale wanapoandika habari zinazokinzana na maoni au
mitazamo ya watawala.
Utajiri wa
rasilimali
Akizungumzia
utajiri wa rasilimali nchini, Dk. Slaa alisema Tanzania imejaliwa vyanzo vya
asili na vyanzo mbadala vya nishati, kuanzia hifadhi kubwa ya gesi asilia (ujazo
wa meta 47 trilioni za mraba), mito mikubwa, vyanzo muhimu kwa ajili ya umeme
wa maji, jua na upepo kwa ajili ya nishati mbadala.
Alisema
kwa utajiri huo, nchi imegeuzwa kuwa sehemu ya watu kuvuna madini na kuondoka,
kuzima ndoto za mamilioni ya vijana kupata ajira kiasi cha kusababisha suala
hilo kuwa bomu linaloweza kulipuka na kusababisha matatizo makubwa katika nchi.
“Tanzania
ina hifadhi kubwa yenye kila aina ya madini na vito kuliko inavyodhaniwa, Kuna
uranium, makaa ya mawe, chuma, shaba, bauxite, almasi, akiki, nikeli,
tanzanite, yakuti na mengine mengi ambayo hupatikana Tanzania, tena kwa wingi,”
alisema.
Alisema
kwamba hata hivyo, pamoja na utajiri huo mkubwa kitendawili ni kwamba Afrika na
Tanzania bado zinaorodheshwa katika ‘nchi maskini’ duniani, wakati rasilimali
hizo ni chanzo cha utajiri unaoweza kuinua taifa.
Alisema
pamoja na madini, Tanzania pia ina utajiri mkubwa wa mifugo na kwamba inashika
nafasi ya tatu duniani kwa wingi wa mifugo hasa ng’ombe, lakini cha kushangaza
hata bidhaa za ngozi tu zinaagizwa kutoka nchi za nje.
Alisema
baada ya kuingia madarakani, serikali ya upinzani kupitia Ukawa itahakikisha
bidhaa zote za mazao ya mifugo zinazalishwa nchini, badala ya kuuza mazao hayo
kwa bei nafuu na kwenda kurutubishwa nje kisha kurudishwa na kuuzwa kwa bei ya
kutupa.
Alisistiza
kwamba, hata utajiri wa dhahabu, Chadema inataka utumike vyema si kwa nia ya
kuzuia kuuza nje, bali kuhakikisha inashughulikiwa na kusafishwa nchini ili
kutoa ajira kwa Watanzania kisha kuuzwa nje kwa thamani halisi.
Muungano wa Ukawa
Dk.
Slaa alitumia fursa ya Ukawa, akisema kwamba Chadema na vyama rafiki vya ndani;
CUF, NCCR-Mageuzi na NLD vimeamua kuunda ushirikiano maalumu kwa ajili ya
kuhakikisha wanakabiliana isapavyo na CCM.
Alisema
kupitia ushirika wa Ukawa wamejipanga kurejesha heshima ya Tanzania iliyopotea
na kwamba kipaumbele chao baada ya kuingia Ikulu kitakuwa ni kufuta aibu ya nchi
kuwa ombaomba duniani.
Alisema
badala yake wataelekeza nguvu katika kurutubisha utajiri wa nchi ili kulifanya
taifa lisimame kiuchumi na kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kimataifa.
“Daima
nimekuwa nikisisitiza kwamba Chadema tunatoa kipaumbele namba moja kwa elimu, na
elimu pia ni kipaumbele namba mbili na elimu hiyohiyo ni kipaumbele namba tatu kwani
ndiyo msingi wa maendeleo ya uchumi. Misaada ya kiuchumi si kipaumbele cha
Chadema,” alisema.
Alisema
hali hiyo inatokana na ukweli kwamba mafanikio ya kiuchumi ya Marekani na ya
mataifa mengine ya magharibi yanatokana na uwekezaji wao katika elimu ambao
umewezesha kupata rasilimaliwatu ya kukuza kilimo, viwanda na uhakika wa chakula.
Ziara
ya Dk. Slaa nchini humo inatokana na mwaliko wa Gavana wa Jimbo la Indiana,
Mike Pence pamoja na taasisi mbalimbali za nchini humo vikiwamo vyuo vikuu
kutokana na kutambua mchango wake wa kisiasa na kijamii na chama chake katika
maendeleo ya Bara la Afrika.
Mbali na Chuo Kikuu cha Purdue, pia Dk. Slaa
anatarajiwa kutoa mihadhara katika vyuo vikuu vya Indiana na Marion.
CHANZO TANZANIA DAIMA
No comments:
Post a Comment