| Waziri Kivuli wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi kulia akizungumza na wandishi wa habari hawako pichani jijini Dar es Salaam jana |
WAZIRI Kivuli wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Suzan Lymo, amepinga kitendo
cha serikali cha kuwataka walimu waliofunga shule kutokana na uhaba wa chakula
waende wakajieleze kwa mkuu wa mkoa kutokana na hatua hiyo.
Suzan alitoa kauli hiyo baada ya serikali kudai kuwa tayari ilikuwa
imekwishapeleka fedha kwenye shule hizo, hivyo walimu hao hawakupaswa kufanya
hivyo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, waziri
huyo kivuli alisema jambo hilo halishangazi kwa vile inaeleweka kuwa serikali
legelege huzaa maamuzi mabovu yasiyo na mantiki.
“Cha ajabu leo hii watoto wanarudishwa nyumbani au kucheleweshwa
kutofungua shule baada ya likizo ya Pasaka, kwa kuwa wazabuni hawajalipwa fedha
zao na hivyo hawawezi kununua vyakula tena,” alisema Suzan.
Alisema, hatua ya walimu kuwarudisha nyumbani wanafunzi,
ilikuwa sahihi
kwa kuwa kama wangewaacha shuleni huku kukiwa hakuna chakula ieleweke wazi kuwa
wanafunzi hao wangefanya vurugu ambazo zingeweza kuleta matatizo mengine.
“Nawapongeza walimu wakuu kwa utaratibu huo swali ni je walimu wanajua
kiasi cha fedha wanachopaswa kupewa?
“Hii ni aibu kubwa kwa serikali, kama mdau wa elimu imenisikitisha sana
na ninatambua kuwa baadhi ya wazabuni ni wazalendo na wengine hata wanakopa kwa
ajili ya kulisha wanafunzi hawa lakini wamefika ukomo,”alisema Suzan.
Suzan, alisema kuwa mwezi wa tano ni wa mitihani ya kidato cha sita
hivyo wanafunzi wanapaswa kusoma kwa bidii bila bugudha ili waweze kufanya
vizuri.
“Nashangaa badala ya kufanya
hivyo wanavurugwa huku wenzao wa shule binafsi wakiendelea na masomo. Sasa
kutokana na wanafunzi hao kupoteza vipindi matokeo yake ni wanafunzi kufeli
mitihani,” alisema Suzan.
Hata hivyo, alishangazwa kusikia kuwa hadi sasa ni asilimia 62 ya fedha
za kulisha shule zimetolewa wakati hii ni robo ya mwisho wa mwaka, ambapo
ilitakiwa kufikia kipindi hiki iwe ilipswa asilimia 75 zimekwishalipwa.
No comments:
Post a Comment