KAMA UNA TUKIO LOLOTE LA KIJAMII, SIASA, UCHUMI TUWASILIANE KWA E-mail: shehesemtawa@gmail.com SIMU: 0719 352 268

Thursday, 30 April 2015

MADEREVA WATOA SIKU NNE KINYUME CHAKE WATAGOMA


UMOJA wa Vyama vya Madereva nchini umetoa siku nne kwa serikali kukutana nao ili kujadili matatizo na kero zao za siku nyingi zinazowakabili kabla hawajaamua kuchukua uamuzi mgumu wa kuitisha mgomo nchi nzima na kurudisha leseni zao za kazi sehemu husika.
Aprili 9, mwaka huu madereva hao waliitisha mgomo wa nchi nzima uliodumu kwa saa saba, wakiishinikiza serikali kutatua kero zao za miaka mingi, ambazo serikali imeshindwa kuzipatia ufumbuzi.
Baadhi ya madai ya madereva hao ni pamoja na kutokubaliana na agizo lililotolewa na serikali la kuwataka kurudi shuleni kusoma, mikataba ya ajira na kupatiwa huduma za kijamii, ikiwa ni pamoja na huduma za bima ya afya pindi wanapopata ajali.
Akitoa tamko la madereva hao jijini Dar es Salaam jana wakati wa kikao cha mrejesho baada ya kukutana na Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Dk. Makongoro Mahanga, Aprili 18, mwaka huu, Mwenyekiti wa Umoja huo, Clement Masanja, alisema watalazimika kuitisha mgomo mwingine endapo serikali itashindwa kutatua kero zao.
Aliitahadharisha serikali kuwa hatima ya kuitisha mgomo huo wa awamu ya pili itajulikana Mei 4, mwaka huu baada ya siku nne walizotoa kuanzia kesho kukamilika.
“Hatutaki kugombana na serikali wala wamiliki wa mabasi, sisi si wanasiasa, tunarudisha leseni siku hiyo huku tukiendelea kukaa nyumbani hadi serikali itakapotusikiliza,” alisema.
Aliionya serikali kuwa endapo mawaziri wa wizara husika watakubali kukaa nao, waepuke kutoa kauli za kisiasa ambazo hazitekelezeki, kwani wamekuwa wakiahidiwa kwa muda mrefu.
 “Tunajua serikali yetu ni sikivu, siku tukikutana nayo tunataka mikataba yetu iwe mezani, hatutaki kuambiwa suala letu linatafutiwa ufumbuzi,” alitahadharisha.
Masanja alisema kazi ya udereva haina faida kama walivyoona wamiliki wa mabasi baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) kutangaza kushusha nauli.
“Serikali imesaliti amri ya wamiliki wa mabasi, wametishia kugoma, wameitwa kusikilizwa kilio chao na kufanya kikao usiku kucha lakini sisi hatusikilizwi, sasa subirini muone muziki wetu,” alisema.
Masanja alisema ipo migomo ambayo serikali inaisikiliza na kuamua kukaa meza moja kujadili hoja zinazolalamikiwa na kuzipatia ufumbuzi wa kina.
Akitolea mfano mgomo wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT), Masanja alisema waliwahi kuitwa bungeni na kukaa vikao ambavyo vilileta tija kwa wafanyabiashara hao.
Tanzania Daima ilimtafuta Mahanga ili kuzungumzia tamko la umoja wa madereva hao ambapo alisema hawezi kulizungumzia suala hilo, kwani halijafika ofisini kwake kwa njia ya maandishi.
Alisema Aprili 18, mwaka huu alipokutana na viongozi wa umoja huo aliwasomea tamko la serikali na baadaye alitoa nafasi ya kuyajadili yaliyomo na wengi walijadili na kufikia muafaka.
“Baadhi ya masuala tuliyokubaliana ni pamoja na suala la tochi ambalo niliwaambia hili ni lazima, kwani ni kwa ajili ya usalama na suala jingine kuhusu kusoma, nalo tulilitolea ufafanuzi,” alisema.
Naye Katibu Mkuu wa Umoja huo, Rashid Salehe, alisema wanapinga tamko la serikali, kwani majibu yake hayajibu kero zao za msingi.
Alisema tamko hilo walikabidhiwa na Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Dk. Mahanga Aprili 18 walipokwenda kwa ajili ya kukutana na mawaziri hao walioomba kukutana nao ili kutafuta suluhu ya kero zao.
“Tulikuwa tumeomba kukutana na Waziri wa Mambo ya Ndani, Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi, Waziri wa Ujenzi na Miundombinu pamoja na Waziri wa Kazi lakini wote hao hatujafanikiwa kukutana nao na badala yake tumemkuta Naibu Waziri wa Kazi na Ajira Makongoro ambaye  alitukabidhi tamko hilo lisiloonyesha  limetokea wapi, kwani halina utambulisho wa  muhuri wala saini,” alisema Salehe.
Alisema hawana imani na kikao cha jana kati ya waajiri na serikali kwa madai kuwa waajiri hawakuwa na madai yoyote kwa serikali.
Pia alisema tamko hilo linapingana na la Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka, alilotoa kwenye mkutano wa hadhara wakati wa mgomo wa awali kwamba hawatalazimika kwenda kusoma chuoni kila baada ya miaka mitatu.
“Tatizo letu  madereva ni kwamba Waziri Kabaka aliposema hakuna kusoma na Kamanda Kova aliposema hakuna tochi,  wala vituo vya ukaguzi wa magari (Check Points),  tulikimbilia magari bila kuwa na karatasi yoyote yenye chapisho la kauli hizo, ndiyo maana serikali imetugeuka,” alisema.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Madereva wa malori makubwa Tanzania (Chamamata), Shaaban Mdemu, alisema Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohammed Mpinga, amekuwa hakimu wa kuhukumu watuhumiwa.
“Dereva mwenzetu kutoka Kampuni ya Ota High Class yupo mkoani Kigoma kutokana na agizo la Kamanda Mpinga la kuwekwa kituoni siku kumi na nne bila dhamana yoyote, tunataka kujua Kamanda Mpinga ni hakimu?,” alihoji.
Mdemu alisema sababu ya dereva huyo kuwekwa ndani ni baada ya kuwahi kufika mkoani Kigoma nusu saa kabla ya muda anaotakiwa kufika.
Alisema askari wa barabarani wamekuwa kero kutokana na ukaguzi unaofanywa na askari hao kwa siku, hasa kwa daladala, ambapo hukaguliwa muda wote.
“Sitaki kujua Kamanda Mpinga anawatuma wakusanye shilingi ngapi kwa siku askari wake ambao hata mara tatu hufanya ukaguzi kwa daladala moja kwa siku,” aliongeza.

CHANZO TANZANIA DAIMA






No comments:

Post a Comment