KAMA UNA TUKIO LOLOTE LA KIJAMII, SIASA, UCHUMI TUWASILIANE KWA E-mail: shehesemtawa@gmail.com SIMU: 0719 352 268

Tuesday, 7 April 2015

NEMC YAWATAKA WAZALISHAJI WA RAMBO KUJIORODHESHA


Mhandisi Bonaventure Baya

BARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), limewataka wazalishaji, waingizaji, wasambazi, na wauzaji mifuko ya plastiki (Rambo), kujiorodhesha, watakaoshindwa kutekeleza agizo hilo watachukuliwa hatua za kisheria.



Tangazo hilo limekuja baada ya Baraza hilo kubaini kuwa matumizi ya mifuko hiyo licha ya kupigwa marufuku, yamekuwa yakiongezeka kila kukicha.

Agosti mwaka 2013 serikali kupitia aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (mazingira), Dk. Terezya Huvisa, ilipiga marufuku wazalishaji, waingizaji, wasambazi, wauzaji na utumiaji wa mifuko hiyo ya plastiki.

Wakati huo, Dk. Huvisa alikaririwa na vyombo vya habari akisema kuwa jitihada zinahitajika ili kuhakikisha kuwa marufuku hiyo inazingatiwa, msako wa watu wanaofanyabiashara hiyo unafanyika katika maeneo yote ndani ya nchi na watakaokiuka sheria wachukuliwe hatua.

Madhara yanayosababishwa na mifuko ya plastiki ni pamoja na uharibifu wa udongo unaotokana na kuunguzwa kwa plastiki hizi na hivyo kusababisha madhara ya kiafya kwa binadamu na wanyama ,kutooza kiurahisi wa njia za kiasili (non-biodegradable) kuzagaa katika mito, maziwa, bahari na nchi kavu hivyo kuhatarisha maisha ya viumbe hai wanaoishi katika mazingira.

Hata hivyo, tangu kipindi hicho mifuko hiyo imekuwa ikiendelea kutumika katika maeneo mbalimbali ya nchi tena bila kificho.

Katika tangazo lake alilolitoa kwenye vyombo vya vya habari, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Bonaventure Baya,alisema kazi hiyo ya kujiandikisha itafanyika katika Ofisi za Baraza hilo, ziliziko makao makuu Dar es Salaam au zile zilizoko Mbeya, Mwanza, Arusha na Mtwara  miezi kwa miezi miwili kuanzia Aprili Mosi hadi Mei 30 mwaka huu.

Kwa mujibu wa NEMC, hatua hiyo ni kutimiza matakwa ya sheria ya usimamizi wa mazingira namba 20 ya mwaka 2004 na kanuni ya mifuko ya plastiki ya mwaka 2006.

“Usajili huu ni muhimu sana katika kusaidia maamuzi ya namna ya kushughulikia tatizo la mifuko hii ya plastiki nchini,”alisema.
Baya, alisema kuwa watakaoshindwa kujiorodhesha ifikapo Mei 30 watambue kuwa shughuli zao zitasimamishwa na kuchukuliwa hatua za kisheria

“Tunaujulisha umma kuwa wazlishaji kuwa wazalishaji, waingizaji, wauzaji wa jumla na watumiaji wakubwa wa mifuko ya plastiki wote nchini, mfano Supermarket mnatakiwa kujiorodhesha katika ofisi zetu za NEMC tilizowajulisha,”alisema.

Baraza linaendelea kusistiza kuwa kwa mujibu wa kanuni ya mifuko ya plastiki ya mwaka 2006, mifuko inayoruhusiwa kisheria ni ile yenye unene wa kuanzia mikroni 30 na yote inayotumika au kuzalishwa nchini kuwa ni lazima iwe na alama (Nembo), ya mzalishaji au muagizaji.  

No comments:

Post a Comment