KAMA UNA TUKIO LOLOTE LA KIJAMII, SIASA, UCHUMI TUWASILIANE KWA E-mail: shehesemtawa@gmail.com SIMU: 0719 352 268

Thursday, 9 April 2015

TPA YAWASHAURI WADAU WA BANDARI KUPITISHIA MIZIGO YAO DAR

WADAU wa Mamlaka ya Usimamizi Bandari nchini (TPA), wameshauri taasisi zinazotoa huduma kwa mizigo kupitia bandari ya Dar es Salaam kutoa huduma hizo katika kituo kimoja, ili kuiongezea ufanisi bandari hiyo.
Ushauri huo ulitolewa hivi karibuni jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Awadh Massawe, alisema  katika vikao vya wadau wa mamlaka hiyo.
“Katika mkutano wetu, wadau wa bandari wamependekeza kuwa taasisi hizo zisogeze huduma zao karibu na bandari kuongeza ufanisi wa kazi,” alisema Massawe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya vikao vya wadau wa mamlaka hiyo.
Mapendekezo hayo yamekuja kutokana na mikutano ya kawaida ya kamati ya vikao vya wadau wa TPA ambayo hufanyika kila mwezi katika juhudi za kuimarisha huduma za bandari.
Alizitaja baadhi ya taasisi hizo kuwa ni Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Ofisi ya Mkemia Mkuu na wakala wa Mizani na Vipimo.
Alisema wadau wa bandari wamebaini kuwa kitendo cha taasisi hizo kuwa mbali na eneo la bandari imekuwa ni kikwazo kwao na kuchangia kusababisha mizigo kukaa bandari muda mrefu.
Alisema wadau wa bandari wangependa kuona shughuli zote zinakuwa katika kituo kimoja, ili kuleta ufanisi wa kazi na kuiwezesha bandari hiyo kuwa moja ya bandari shindani katika ukanda huu na barani Afrika kwa jumla.
Pia alisema kwa sasa TPA inajenga jengo la ghorofa ambapo taasisi au kampuni zinazohusika na masuala ya huduma za bandari zinaweza kuomba, ili huduma nyingi ziwe katika kituo kimoja kurahisisha utendaji kazi bandarini.
Kwa upande wake, Rais wa Chama cha Wakala wa Mizigo Tanzania (Taffa), Stephene Ngatunga, alisema kumekuwa na ucheleweshaji mkubwa wa kuondoa mizigo bandari kutokana na taasisi hizo kuwa mbalimbali.
“Kwa utaratibu ulivyo, Mamlaka ya Mapato (TRA) haiwezi kutoza kodi bila ya taasisi hizi kumaliza kazi zake...hii inaleta changamoto,” alisema.

Mwisho

No comments:

Post a Comment