JUMUIYA na Taasisi za Kiislam Tanzania
zimesema zitafanya maandamano ya amani ifikapo Mei 15 mwaka huu iwapo serikali
itashindwa kutekeleza madai yao.
Akizungumza na waandishi wa habari jana
jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Jumuiya na Taasisi za Kiislam Tanzania,
Musa Kundecha alisema, serikali inapaswa kuwaombe radhi waislam kutokana na vitendo vya unyanyasaji vinavyofanywa
na jeshi la polisi nchini.
Kundecha alisema kuwa jeshi hilo
limekuwa likiwahujumu waislam kupitia madrasa ambazo ndiyo kiini cha elimu ya
dini ya kiislam na maadili mema kwa jamii.
“Serikali iache mara moja kuvamia na
kuziandama madrasa na kuwaweka mahabusu watoto wadogo kwa kisingizio cha vyuo
hivyo kutosajiliwa ili hali hakuna sheria wala sera ya elimu inayotaka madrassa
zisajiliwe,” alisema
Sheikh Kundecha alisema kuwa Serikali
inapaswa kutoa dhamana kwa masheikh walioko mahabusu kama inavyofanya kwa
maaskofu na wachungaji walioshitakiwa mahakamani.
“Jeshi la Polisi liwaachie au kuwapa
dhamana mashekh, maustadhi na maimamu waliokamatwa sehemu mbalimbali nchini na
ambao wako katika mikono ya Polisi kwa muda mrefu bila kufikishwa mahakamani,”
alisemaKundecha alisema baadhi ya viongozi wa
serikali ngazi za wilaya, mikoa na taifa wamekuwa wakiungana na jeshi la Polisi
katika harakati hizo ambazo zina athari kwa waislamu nchini.
“Tuhuma wanazotoa Polisi kuhalalisha
harakati za uvamizi na kamatakamata ni pamoja na madrassa na masheikh
kufundisha dini ya Kiislam kinyume cha sheria, kukusanya watoto na kuwafundisha
elimu ya dini kinyume cha sheria na katika mazingira yasiofaa,”alisema.
Alisema kuwa polisi wamekuwa wakidai
kuwa madrasa hizo zimekuwa zikifundisha na kufanya mazoezi yanayoendana na
ugaidi kinyume na sheria, kuwepo kwa taarifa za watu wenye milipuko miskitini
na kutuhumiwa kujihusisha na vitendo vya kigaidi.
Akitolea mfano huko Kilombero mkoani
Morogoro alisema watu wengi waliingia msikitini saa tisa za usiku na muda mfupi
baadae polisi wakaja na kuvamia msikiti kwa namna ambayo inatia shaka.
Alihoji kuwa Polisi walifahamu watu hao
wametoka wapi au walihusika kwa nia ya kuchafua hadhi ya msikiti na uislamu.
“Watu waliokamatwa sio wenyeji wala
wakazi wa eneo linalotumia msikiti huo, hilo halikutajwa na Polisi wala
kiongozi yeyote wa serikali,”alisema.
Alisema Polisi wamekuwa wakikiuka haki
nyingi za binadamu, haki za kikatiba, na kisheria huku wakichangia na
kusababisha waislam kuonekana kuwa sio waaminifu na watu wanaochukia amani
hatua inayosababisha wachukiwe na jamii.
Naye Katibu wa Jumuiya hiyo Rajab
Katimba alisema, anashangazwa na Polisi kuwakamata masheikh na maustadhi kwa kisingizio cha vituo kuwa na hali duni
huku wakishindwa kuwakamata walimu wanaofundisha shule zenye ukosefu wa vyoo.

No comments:
Post a Comment