KAMA UNA TUKIO LOLOTE LA KIJAMII, SIASA, UCHUMI TUWASILIANE KWA E-mail: shehesemtawa@gmail.com SIMU: 0719 352 268

Friday, 15 May 2015

CRDB YATAKA BoT ISISHINIKIZWE




Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dk. Charles Kimei, akifafanua jambo wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam juzi, kuhusu mdororo wa shilingi. Kulia ni Mkurugenzi wa Masoko, Utafiti na Huduma kwa Wateja wa benki hiyo, Tully Mwambapa. (Picha na Francis Dande).
WADAU wa maendeleo nchini hususan wanasiasa, wametakiwa kuacha tabia ya kuishinikiza Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kudhibiti mdororo wa shilingi ya Tanzania, kwani si njia sahihi na badala yake waache thamani ya fedha hiyo kukua kulingana na mahitaji ya kiuchumi.
Wito huo umetolewa juzi na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dk. Charles Kimei, alipozungumzia kushuka kwa thamani ya shilingi ya Tanzania na kusema mashinikizo kutoka kwa wadau hao yanaziathiri taasisi za kifedha, hususan benki.
Dk. Kimei alisema shinikizo hilo linailazimu BoT kuziminya benki, kwani njia nzuri inayotumiwa na taasisi hiyo katika kuzuia anguko hilo na mabadiliko ya fedha za kigeni ni kubana sera za kifedha na kuondoa zaidi shilingi katika mzunguko wake.
“Moja ya athari za kuondoa shilingi katika mzunguko wake ni kupanda kwa riba miongoni mwa watumiaji wa huduma za kibenki, hivyo kupunguza nia ya kukopa waliyonayo wateja wetu na kuathiri mzungunko wetu wa fedha,” alisema Dk. Kimei.
Aliwataka wadau hao, hasa wanasiasa, waguswe kwa namna moja ama nyingine na ukuaji huo wa riba kwa Mtanzania wa kawaida ambao unaathiri harakati za maendeleo, na kwamba waelekeze nguvu zao katika hilo ili kupunguza ukali wa maisha na kuleta maendeleo ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment