KATIBU MKUU TAMISEMI, SAGINI ASISITIZA UIMARISHAJI WA ELIMU
Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la
Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Tanzania, Bi.
Zulmira Rodrigues akisalimiana na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu
Tawala za Mikoa na. Serikali ya Mtaa (TAMISEMI), Jumanne Sagini
alipomtembelea ofisini kwake mjini Dodoma wakati wa ziara ya kikazi ya
siku moja ya kukutana na wadau wa elimu walioshiriki mkutano wa
kutathmini sekta ya Eimu nchini kwa mwaka 2014 uliofanyika katika kumbi
za mikutano Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
……………………………………………….
(Habari -Picha zote na Zainul Mzige wa modewjiblog).
KATIBU Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu
Tawala za Mikoa na Serikali ya Mtaa (TAMISEMI), Jumanne Sagini amesema
elimu ya sasa inaelekezwa zaidi katika kumwezesha mtu kujitegemea.
Kauli hiyo ameitoa katika mahojiano maalum na mtandao wa habari wa modewjiblog kuhusu
maendeleo na changamoto kwenye sekta ya elimu nchini katika wiki ya
maadhimisho ya elimu inayofikia tamati leo mjini Dodoma.
Alisema katika mahojiano hayo
kwamba mfumo sasa unawaondoa watu kwenye ajira ya serikali na kutokana
na hilo uimarishaji wa elimu ndio kitu cha msingi kabisa.
Alisema katika maadhimisho ya elimu watu wanajifunza usimamizi kama msingi mkubwa wa maendeleo ya elimu nchini.
Alisema kuna mambo mengi ambayo
yanastahili kuangaliwa kwa sasa kutokana na vigezo vya ufanisi wa elimu
kuonesha changamoto zinazokabili sekta hiyo pamoja na kuimarika kwake.
Alizitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na kupungua kwa uandikishaji wa watoto na mdondoko.
Alisema viongozi, wazazi pamoja na
walezi wamesahau wajibu wao na kumwachia mwalimu pekee katika kumlea
mwanafunzi kimasomo na hii ndio chanzo kikubwa cha mdondoko na ufaulu
mbaya.
Alisema ni vyema watu wakajiuliza hawa wanaondoka wanakwenda wapi na wanafanya nini.
“kuna sheria ambapo viongozi wa
kata wanaruhusiwa kuwachukulia hatua na kuwafikisha mahakamani wazazi
wanaokwamisha elimu, lakini watu hawachukia sheria hiyo” alisema.
Aidha alisema ubora wa elimu una
vigezo vingi ikiwa ni pamoja na kujituma kwa walimu katika ufundishaji
na kuwa na dhamira ya kuwapa watoto vitu vyenye maana.
Alisema kuna mambo mengi
yanatakiwa kufanywa kuinua elimu na usimamizi unapokuwa mkali na
wahusika kuadhibiwa ndio ufanisi unafanyika na mdondoko kuangaliwa.
Alisema ipo haja kubwa ya kuwekeza kwenye elimu kwa viongozi na wadau kutimiza wajibu wao.
Naye Mkurugenzi Msaidizi wa
Ufuatiliaji na Tathmini wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi , Makuru
Petro akitoa tathmini ya sekta ya elimu kwa wadau wa sekta ya elimu
alisema pamoja na ongezeko la ufaulu ndani ya miaka miwili ipo haja ya
kutathimini uimara wa mfumo katika kutoa huduma ya elimu.
Alisema pamoja na ufanisi kuwapo kwa idadi kubwa ya watu wanaokacha shule kunaonesha mfumo kuwa na kasoro na lazima uangaliwe.
Aidha alisema sekta ya elimu
wamepokea asilimia 97 ya bajeti yake na kwamba asilimia 70 imeenda
kwenye halmashauri ambako ni watekelezaji wa miradi ya elimu.
Tathmini hiyo inayowakilisha
wizara zote zinazoshughulikia elimu kama TAMISEMI, Elimu na Maendeleo ya
jamii na wadau wengine wa elimu ni sehemu ya shughuli inafanywa kila
mwaka kwa lengo la kutambua kilichofanyika, changamoto na namna ya
kukabiliana na tatizo hilo.
Hata hivyo walisema kwamba ndani
ya miaka miwili kumekuwepo na maendeleo makubwa katika sekta ya elimu
hasa ufaulu na ubora wa elimu.
No comments:
Post a Comment