Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dk. Albina Chuwa akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari kuhusu ujio wa sheria mpya ya Takwimu ya mwaka 2015 iliyopitishwa na Bunge Mwezi Machi mwaka huu leo jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi wa Ofisi hiyo, Morrice Oyuke.
Wadau mbalimbali na waandishi wa habari wakimsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dk. Albina Chuwa wakati akitoa ufafanuzi kuhusu ujio wa sheria mpya ya Takwimu ya mwaka 2015.
BAADA ya sheria mpya ya
takwimu kulalamikiwa na wadau mbalimbali, ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), imetoa ufafanuzi kuhusu sheria hiyo na
kusema haina uhusiano na haitahusika katika uchaguzi mkuu.
Akizungumza na waandishi
wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Dk. Albina Chuwa, alisema: “Hatuna
uhusiano na hatushiriki katika uchaguzi mkuu. NBS imetoa takwimu kuwa
wapigakura ni milioni 24”.
Kauli hiyo ya Dk. Chuwa
imetokana na swali aliloulizwa na waandishi wa habari iwapo sheria hiyo
inavibana vyombo vya habari vitakavyoripoti matokeo ya awali ya uchaguzi mkuu.
Mbali na hilo alisema sheria hiyo haizuii au haihusiki na taasisi
au mtu binafsi kufanya utafiti.
Alisema taasisi za utafiti
zina sheria na kanuni za kufanya tafiti ikijumlisha kukusanya na kusambaza
matokeo ya tafiti zao.
“Kwa mujibu wa sheria hii
kila taasisi au chombo chochote cha utafiti hakizuiwi kuendelea na utaratibu
wake wa utoaji wa takwimu kulingana na tafiti wanazofanya. Kwa wanafunzi wa
vyuo vikuu na vinavyolingana sheria hii haihusiki na “Thesis au dissertation”
zao wanasimamiwa na wahadhiri wa vyuo vikuu. Ipo sheria inayowalinda na matokeo
hayo na husambazwa kwa utaratibu
uliowekwa na sheria zilizoanzisha vyuo vikuu.
Hata hivyo, alisema jambo
la msingi linalopaswa kuzingatiwa ni iwapo taasisi au mtu binfasi anataka
takwimu alizokusanya zitumike katika
mipango ya maendeleo ya nchi na kusema kuwa atalazimika kutoa
takwimu hizo kwa kuzingatiia misingi ya takwimu rasmi.
Dk. Chuwa alisema takwimu
rasmi ambazo huzalishwa na wizara, idara
na taasisi za serkali hufuata kanuni 10
na misingi zilizotolewa na Kamisheni ya Umoja wa Mataifa ya Tamwimu.
Pia alisema vyombo vya
habari vitakavyopotosha takwimu rasmi, vitakuwa vimekiuka kifungu cha 37(4) na
(5) cha sheria hiyo, hivyo kitashughulikiwa kwa mujibu wa sheria.
Alisema kwa mujibu wa
kifungu hicho kinalenga kuwa takwimu
rasmi inayotangazwa ieleze chanzo chake
na kutoa mfano kama chombo cha habari kitatangaza kuwa mfumuko wa bei
uliotolewa na NBS ulikuwa asilimia 3.0 baada ya asilimia 4.5, chombo hicho
kitastahili kupewa adhabu.
“Napenda kutumia fursa
hii, kuwaomba kuendelea kutangaza taarifa hizi kwa usahihi, ili kusaidia
wananchi na wadau wote wa ndani na nje ya nchi kutoa mawazo yaliyojengeka kuwa
sheria hii ni kandamizi…. Ikumbukwe kuwa serikali ina wajibu wa kuandaa mipango
ya maendeleo kwa wananchi wake. Vilevile wananchi tuna wajibu wa kutoa taarifa
sahihi kwa serikali.Takwimu bora husaidia serikali yoyote ile duniani kupanga
mipango ya maendeleo ya wananchi wake. Kutofanya hivyo, serikali haitaweza
kupanga mipango yoyote ya maendeleo kwa wananchi wake,” alisema.
Alisema
makosa ya jinai yaliyoainishwa katika sheria hiyo ni endapo watumishi wa NBS watatumia taarifa
za kitakwimu rasmi kwa manufaa binafsi, kutoa taarifa za kitakwimu rasmi bila
kibali, kudai taarifa tofauti na
zilizoruhusiwa kukusanywa na kuomba malipo au ujira.
Alieleza kuwa vitendo
vyote hivyo ni makosa ya jinai na mhusika akipatikana na hatia atapewa adhabu
isiyopungua mezi sita au kulipa faini isiyopungua sh. milioni 2 au vyote kwa
pamoja.
Mkurugenzi mkuu huyo
alisema mtu atakayetoa taarifa zilizopatikana isivyo halali, kwa mujibu wa sheria atapewa adhabu ya
kifungo kisichopungua miezi 12 au faini isiyopungua sh. milioni tano au vyote
kwa pamoja.
Mbali na hilo, alisema mtu
akikataa kutoa ushirikiano katika zoezi la kitakwimu adhabu ni kifungo kisichopungua miezi sita au faini
ya sh. milioni moja.
No comments:
Post a Comment