KAMA UNA TUKIO LOLOTE LA KIJAMII, SIASA, UCHUMI TUWASILIANE KWA E-mail: shehesemtawa@gmail.com SIMU: 0719 352 268

Thursday, 21 May 2015

RAIS KIKWETE AFUNGUA MKUTANO WA OGP KANDA YA AFRIKA

unnamed
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt Jakaya Kikwete akizungumza alipokuwa akifungua mkutano wa Open Government Partnership kwa wanachama wa Kanda ya Afrika jana jijini Dar es Salaam.
……………………………………………………………………………………
Na Anitha Jonas – MAELEZO.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete amewasihi watanzania kuacha kulalamika juu ya miswada mbalimbali iliyopitishwa na bunge hivi karibuni ukiwemo Muswada wa Makosa ya Kimtandao na badala yake wapeleke maoni yao kwa Waziri wa Mawasiliano,Sayansi na Teknolojia Mhe.Makame Mbarawa.
Ameyasema hayo alipokuwa akifungua mkutano wa Open Government Partinership (OGP) kwa nchi wanachama Kanda ya Afrika unaolenga kujadili na kubadilishana uzoefu juu ya uwazi katika uendeshwaji wa shughuli za Serikali.
“Serikali ya Tanzania inauwazi mkubwa,napenda wananchi wajue namna inavyofanya kazi ndiyo maana nimeruhusu mambo mengi yenye manufaa kuwekwa wazi ikiwemo taarifa ya Mkaguzi Mkuu wa Mahesabu ya Serikali (CAG) kutoa taarifa yake kwa uwazi na kuruhusu ijadiliwe Bungeni pamoja na kuonyesha shughuli za bunge tangu linapoanza mpaka mwisho”,alisema Mhe.Dkt Kikwete.
Aidha Dkt Kikwete aliendelea kusema Tanzania ni nchi ya pili Afrika kusaini mkataba huo wa OGP uliyoanzishwa mwaka 2011,hii ni kutokana na kuona manufaa makubwa kwa taifa pale Serikali inapofanya shughuli zake kiuwazi na kuwapa fursa wananchi kujua namna mambo yanafanyika katika ngazi mbalimbali za Serikalini.
Halikadhalika Waziri wanchi Ofisi ya Rais Utawala Bora Mhe.Kapt George Mkuchika alifafanua kuwa katika kutekeleza mpango huo wa OGP kitaifa iliundwa kamati ya kuratibu inayosimamiwa na Ofisi ya Rais,Ikulu pamoja na wajumbe kutoka Serikalini na asasi za kiraia .
“Mpango kazi huu ulikuwa ni kuboresha utoaji wa huduma katika sekta ya Afya,Maji na Elimu.Mafanikio katika utekelezaji wa mpango kazi huu ni kuboresha tovuti mbalimbali za Serikali na kuwafanya wananchi kupata habari kwa wakati bila kulipia gharama zozote,pamoja na kupitia upya mikataba ya huduma kwa wateja kwenye Sekta ya Afya,Elimu na Maji ili kuimarisha uadilifu na uwajibikaji”,alisema Kapt George Mkuchika.
Hata hivyo Mhe.Rais alisema suala la kutungwa kwa sheria ya uhuru wa kupata taarifa pamoja kuundwa kwa sheria ya uhuru wa vyombo vya habari ni makubaliano kwa nchi wanachama wa (OGP) na hayo aliyaahidi kuyatekeleza kabla ya kuondoka madarakani kwani sheria hizi zitachangia kuboresha hali ya uwazi wa shughuli za Serikali kwa wananchi.
Mbali na hayo Rais Kikwete aliwashukuru washiriki wa mkutano huo OGP kwa kuichagua Tanzania kuwa mwenyeji wa Mkutano huo na pia aliwasihi kutembelea vivutio mbalmbali vya nchi ikiwemo Kisiwa cha Zanzibar pamoja na Mlima Kilimanjaro.
Mkutano huo unahusisha nchi nane washirika katika Kanda ya Afrika ambazo ni Liberia,Afrika Kusini,Malawi,Ghana,Siera Leone,Kenya,Tunisia na Tanzania ambao ni wenyeji,na Kauli Mbiu ni “Kuimarisha Utawala Bora Unaozingatia Uwazi na Uwajibikaji”.

No comments:

Post a Comment