![]() |
| Mkugenzi Mtendaji wa Tanesco, Felchesmi Mramba |
SHIRIKA la Umeme Tanzania
(Tanesco), limewataka wateja wake kununua huduma ya umeme wa LUKU kwa kutumia
Wakala wa Maxmalipo nchi nzima, Benki ya CRDB na NMB kila zilipo.
Kauli hiyo hiyo imetolewa na Meneja Uhusiano wa Tanesco, Adriano Severine,
baada ya Kampuni moja ya simu za mikononi kusambaza ujumbe unaosema: Ndugu
mteja huduma ya LUKU haipatikani kwa sasa kutokana na shida iliyopo upande wa
washirika wetu, tafadhali tembelea wakala wa Tanesco kununua umeme wako.
Akizungumza na Tanzania Daima jijini Dar es Salaam jana, Severine, alisema kampuni
iliyofasambaza ujumbe huo ina matatizo ya kimkataba na Tanesco.
Meneja Uhusiano huyo, alisema ili Wateja wenye Akaunti ya Benki ya
CRDB, wapate huduma hiyo watapaswa kupiga *150*03# na wale wa NMB, wapige
*150*66#, kisha wafuate maelekezo.
“Tunaomba wateja wetu watumie njia hizo ili kujipatia huduma
hiyo,”alisema Severine.
Severine, alisema pia wateja wa NMB wanaweza kununua LUKU kupitia NMB
Mobale, sehemu nyingine ambazo mteja anaweza kununua LUKU ni katika Ofisi zote
za Tanesco zilizoko nchi nzima ambazo zitafanyakazi mpaka siku za Jumapili.
“Tanesco inawaomba wateja wake kuzipuuza taarifa za kukosekana kwa
huduma ya LUKU kwa baadhi ya Mawakala, tunakanusha taarifa zinazosambazwa
kwenye mitandao kuhusu kukosekana kwa huduma hiyo kuwa si sahihi bali huduma
hiyo inapatikana kwa kutumia Maxmalipo nchi nzima, CRDB na NMB kwa wateja wenye
Akaunti na benki hizo,”alisema Severine.
Aliongeza kwa kusema kuwa kwa upande wa mitandao ya Simu wateja
wanaweza kununua umeme kupitia M-Pesa na Airtel Money.
Aidha, aliwataka Mawakala ambao hawawezi kuuza umeme wasiliane na
Tanesco kwa mujibu wa mikataba yao
na si vinginevyo.

No comments:
Post a Comment