![]() |
| Naibu Katibu Mkuu-Zanzibar, Salum Mwalimu |
Aidha, Chadema imetangaza pia gharama za fomu kwa kila ngazi ya uteuzi
ikiwemo udiwani, uwakilishi, ubunge na Urais
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam leo, Naibu
Katibu Mkuu wa CHADEMA Zanzibar Salum
Mwalim ametaja mchakato wa uteuzi huo kuwa utahusisha hatua tatu katika ngazi
ya kata na jimbo/wilaya husika na hatua moja katika ngazi ya kitaifa.
“Kupitia mkutano wetu nanyi, tunapenda kuwataarifu Watanzania wote wenye
sifa za kuwania uteuzi kupitia CHADEMA kuwa kwa kuzingatia matakwa ya katiba ya
chama na ya demokrasia pana ikilenga kuhakikisha tunapata wagombea waadilifu,
wenye uwezo wa kuwatumikia watu na wanaokubalika na wapiga kura.”Alisema Mwalim.
Katika kikao cha Kamati Kuu ya Chama kilichoketi Mei 3 na 4 jijini Dar
es salaam kilipitisha utaratibu huo utakaotumika kupata maoni na hatimaye
kufanya uteuzi wa wagombea watakaosimama kugombea nafasi hizo tajwa kupitia
CHADEMA katika ushirikano wa vyama vinavyounda UKAWA.
Mwalim ameutaja utaratibu huo katika makundi mawili ya
ubunge/uwakilishi na udiwani, kuwa ni:
Ubunge/Uwakilishi
1. Mkutano Mkuu Maalum wa Jimbo
Mkutano huu utafanyika kwenye Kila
Jimbo la Uchaguzi na utafanyika siku moja kwenye eneo moja Makao Makuu ya Jimbo
au eneo ambalo litaamuliwa na vikao vya Chama .
Washiriki watatakiwa kuwapigia
kura moja wagombea ambao wamejitokeza ndani ya chama na kura hiyo itakuwa ya
siri .
Wasimamizi wa Mikutano hii maalum
ya kura ya maoni watatakiwa kuwa watu ambao hawana ‘maslahi’ kwenye uchaguzi huo yaani wasiwe wagombea au wasiwe na
mgombea ambaye wanamuunga mkono kati ya wanaogombea wa nafasi hiyo.
Kila Mgombea atapewa fursa ya
kujieleza mbele ya wapiga kura kwa dakika tano (5) na ataulizwa maswali
yasiyozidi matatu kutoka kwa washiriki .
Kura zitapigwa
mwishoni baada ya wagombea wote kumaliza kujieleza mbele ya Mkutano Maalum wa
kura ya Maoni , na kila Mgombea atakuwa na haki ya kuweka wakala wa kuhesabu
kura zake .
Matokeo ya Kura
hizi yatawasilishwa kwenye Kikao Cha Kamati ya Utendaji ya Jimbo/Wilaya kabla
ya kufanya kikao chake cha uteuzi .
Gharama za kuendesha mikutano
maalum ya kura ya maoni zitatokana na malipo ya fomu za ugombea wa nafasi ya
ubunge na kata .
Wajumbe wa Mkutano Maalum wa Kura
ya Maoni Jimbo/Wilaya :
(i)
Wajumbe wote wa Kamati ya Utendaji ya Jimbo
(ii)
Wenyeviti wote wa kata za wilaya /jimbo
(iii)
Makatibu wote wa kata za wilaya/jimbo
(iv)
Makatibu waenezi wote wa kata za jimbo/wilaya
(v)
Wenyeviti na makatibu wa Mabaraza yote ya Chama
Jimbo/Wilaya
(vi)
Wenyeviti wa Mabaraza yote katika Kata za wilaya/jimbo
(vii)
Makatibu wa mabaraza yote ya kata katika
jimbo/wilaya
(viii) Wenyeviti
wa Serikali za Vijiji, Mitaa na Vitongoji watokanao na Chama kwenye Jimbo.
2. Wagombea kujipigia kura wenyewe
Wagombea wote wapewe fursa ndani
ya Mkutano Maalum ya kujipigia kura wenyewe na kila mmoja apige kura tatu, kura
moja iwe yake binafsi na kura nyingine mbili atakiwe kuwapigia wagombea wengine
waliopo .
Matokeo ya kura hizi pia
yatawasilishwa Kamati ya Utendaji na pia Ofisi ya Katibu Mkuu.
3. Kamati ya Utendaji ya Jimbo/Wilaya
Kamati ya Utendaji ya Wilaya
/Jimbo itafanya uteuzi wa awali kwa mujibu wa Katiba ya Chama Ibara ya 7.4.10 (q)
Kamati ya Utendaji itatakiwa
kupiga kura za awali na kuwasilisha taarifa yake pamoja na Mapendekezo yake kwa
Kamati Kuu kwa mujibu wa Katiba ya Chama kwa ajili ya uteuzi mwisho.
Utaratibu wa kuendesha vikao vya
Kamati ya Utendaji Jimbo/Wilaya utazingatia Katiba na Kanuni za Chama.
Udiwani
Katika nafasi ya udiwani Mwalim
alisema kuwa utaratibu utakaotumika ni ule ule kama ilivyo katika nafasi ya
ubunge isipokuwa hapa itakuwa katika ngazi ya kata kama
ifuatavyo;
1.
Mkutano
Mkuu Maalum wa Kata/Wadi
Wajumbe wa Mkutano Maalum wa Kura
ya Maoni kata/wadi:
(i)
Wajumbe wote wa Kamati ya Utendaji ya Kata
(ii)
Wenyeviti wote wa matawi katika kata
(iii)
Makatibu wote wa matawi katika kata
(iv)
Wenyeviti wote wa mabaraza ya wazee, wanawake na
vijana katika kata
(v)
Diwani wa Chama wa Kata/Wadi, Diwani wa Viti
Maalum, Mbunge/Mwakilishi anayeishi katika kata husika.
(vi)
Wenyeviti wa Serikali za Vijiji na Wenyeviti wa
Kamati za Mitaa au Shehiya wanaotokana na Chama katika kata.
(vii)
Wenyeviti wa Serikali za Vitongoji, Mitaa na
wajumbe wa serikali hizo katika kata wanaotokana na CHADEMA.
2.
Wagombea
kujipigia kura wenyewe
3.
Kamati ya
Utendaji ya Jimbo/Wilaya
Mwalimu ameongeza kuwa tofauti na
kwenye nafasi ya ubunge na uwakilishi ambayo uteuzi wake wa mwisho unafanywa na
Kamati Kuu ya Chama, kwenye ngazi ya udiwani uteuzi utafanywa na Kamati ya
Utendaji ya Jimbo/Wilaya kwa mujibu wa Katiba ya CHADEMA.
“Lakini pia hapa kwenye udiwani,
mkutano mkuu maalum wa kata ambao utawapigia kura za maoni wanaowania uteuzi wa
udiwani, mbali ya kujumuisha wenyeviti wa vijiji, vitongoji na mitaa,
utahusisha pia wajumbe wote wa serikali katika vitongoji, vijiji na mitaa
wanaotokana na CHADEMA katika kata husika. Unaweza kuona tunavyopanua wigo wa
demokrasia,” amesisitiza Mwalim.
Gharama
za fomu, utaratibu wa kuzichukua na kuzirejesha
Kuhusu gharama za kuchukua fomu za
uteuzi huo, Mwalimu alisema kuwa baada ya Kamati Kuu kuamua tarehe za kuchukua
na kurejesha fomu za uteuzi wa ndani ya Chama na mfumo mzima wa kuwapata
wagombea ilikasimisha mamlaka kwa sekretarieti ya chama kufanya maamuzi na
kuidhinisha kutolewa kwa fomu pamoja na gharama zake.
Fomu zitaweza kuchukuliwa eneo
lolote lile yaani kwenye ngazi zifuatazo; Taifa, Mkoa ,Wilaya na Jimbo kwa
upande wa fomu za ubunge na kwa upande wa udiwani fomu zitaweza kuchukuliwa
kwenye ngazi ya wilaya, jimbo na kata.
Fomu hizo pia zitapatikana
mitandaoni kupitia website ya chama; www.chadema.or.tz.
Kurejesha fomu ni lazima
zirejeshwe kwenye Jimbo au Kata ambayo mgombea anagombea na ndipo
atapaswa kulipia gharama za fomu
husika.
Kwa upande wa Ubunge wa Viti
Maalum, fomu zao zitalipiwa moja kwa moja kwenye Akaunti ya BAWACHA Taifa
ambayo ipo kwenye fomu husika, hivyo wagombea wa nafasi hiyo watalazimika
kuambatanisha fomu zao na risiti ya kibenki (Pay Slip) ambayo inaonyesha kuwa
wamelipia fomu hizo.
Gharama za fomu hizo ni kama ifuatavyo;
·
Urais shilingi 1,000,000/=
·
Ubunge/Uwakilishi wa Jimbo shilingi 250,000/=
·
Ubunge Viti Maalum shilingi 250,000/=
·
Udiwani wa Kata shilingi 50,000/=
·
Udiwani wa Viti Maalum 50,000/=
Imetolewa leo Alhamis, Mei 14, 2015
na;
………………………………………………..
Salum Mwalim
Naibu Katibu Mkuu - Zanzibar

No comments:
Post a Comment