KAMA UNA TUKIO LOLOTE LA KIJAMII, SIASA, UCHUMI TUWASILIANE KWA E-mail: shehesemtawa@gmail.com SIMU: 0719 352 268

Friday, 17 July 2015

CCK KUIBURUZA TUME YA UCHAGUZI MAHAKAMANI



KATIBU Mkuu wa Chama Cha Kijamii (CCK), Renatus Muhabhi amesema chama hicho kinatarajia kwenda Mahakamani juma lijalo kuiwekea zuio Tume ya Taifa ya Uchaguzi ili kuzuia kutoa fomu kwa mgombea urais wa Chama Chama Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli.
Alisema kuwa zuio hilo linatokana na NEC kushindwa kumchukulia hatua za kisheria Dk Magufuli na chama chake kutokana na kuanza kampeni kabla ya wakati.
Akizungumza na wandishi wa habari jijini jana, Muhabhi, alisema licha ya kuiandikia NEC, barua bado hawaani kama kuna lolote jipya linaloweza kufikiwa na tume hiyo.
Alisema, wamechukua uwamuzi huo kutokana na CCM pamoja na mgombea wake kukiuka sheria na kanuni za uchaguzi huku tume ya uchaguzi ikikaa kimya.
“CCK inapiga kelele kwa vile tunataka lazima kuwe na uwiano wa vyama katika shughuli zote zinazohusiana na demokrasia ya vyama vingi nchini.
“Tunashangazwa na kauli za tume kwamba haihusiki katika kinachoendelea ndani ya CCM bali itawajibika hadi pale itakapotoa fomu kwa kauli hizo inaonesha tume inakilinda chama hicho,”alisema Muhabhi.
Muhabhi, alisema kuwa sheria na kanuni za uchaguzi zinaelekeza kwamba hakuna chama chochote kitakachoanza kamepeni kabla tume haijatoa fomu, kinyume chake chama kitakachofanya hivyo kinaweza kuzuiwa kugombea.
Alisema kwa ukinya wa tume katika hili inaonesha kuwa inaanza kukiuka maadili ya uchaguzi kabla hayajasainiwa na wadau wote wa uchaguzi.
Hivi karibuni Mwenyekiti wa NEC, Jaji Lubuva alikaririwa na vyombo vya habari ikisema mambo yanayoendelea ndani ya CCM kuhusiana na Mikutano, tume haiwezi kuyaingilia.
Alisema tume itaanza kuingilia masuala ya uchaguzi kuona kama kuna kanuni na sheria za uchaguzi zinakiukwa baada ya uteuzi wa wagombea wa vyama vyote kufanyika.

No comments:

Post a Comment