Mwenyekiti
wa Bodi ya Wakurugenzi ya Baraza la Kiswahili la Taifa(BAKITA),
Prof.Martha Qorro(Kulia) akifafanua jambo katika mkutano na waandishi wa
habari ambapo wamempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.
Dkt. John Pombe Magufuli kwa uzalendo wake wa kuitumia lugha ya
Kiswahili katika mikutano mikubwa ya kitaifa ikiwemo mkutano wa 17 wa
nchi wananchama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki , katikati ni Katibu
Mtendaji wa BAKITA Dkt. Seleman Sewangi na kushoto ni Afisa Habari wa
Idara ya Habari(MAELEZO) Bi.Lorietha Laurence.
(Picha na Eliphace Marwa-maelezo).
………………………………………………………………………………………
Na Lorietha Laurence-Maelezo.
Na Lorietha Laurence-Maelezo.
Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) limempongeza Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.John Pombe Magufuli kwa
uzalendo wake wa kuitumia lugha ya Kiswahili katika mikutano mikubwa na
hafla mbalimbali za kitaifa na kimataifa.
Akiongea na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi BAKITA, Prof. Martha Qorro ameeleza
msimamo huo wa Rais Dkt.Magufuli umewasidia Watanzania kupata taarifa
moja kwa moja kutoka tukio husika.
“Uamuzi na msimamo wa Rais Magufuli wa kutumia lugha ya
Kiswahili katika mikutano mikubwa ikiwemo mkutano mkuu wa 17 wa viongozi
wa wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki umepokelewa
kwa furaha kubwa na wananchi na wadau wengi wa Kiswahili ndani na nje ya
Tanzania” alisema Prof.Martha.
Aliongeza kuwa kupitia msimamo huo wa Mhe. Rais Magufuli, Baraza
linaamini kwamba hatua hiyo itasaidia kukuza lugha ya Kiswahili na
kutoa fursa ya ajira kwa Watanzania kupitia tafsiri na ukalimani na
hivyo kuwapelekea maendeleo wananchi wote wa Afrika Mashariki.
Naye Katibu Mtendaji wa BAKITA Dkt. Seleman Sewangi ametoa wito
kwa viongozi wengine wa ngazi mbalimbali za Kitaifa kufuata nyao za
Mhe.Rais Magufuli kwa kuipa kipaumbele lugha ya Kiswahili ili kufikisha
ujumbe kwa Watanzania walio wengi.
“Natoa wito kwa viongozi wetu wa ngazi mbalimbali za kitaifa
kuitumia lugha ya Kiswahili katika mikutano mikubwa na hafla mbalimbali
za kitaifa na kuachana na dhana ya kutumia lugha ya kigeni yenye lengo
la kuwafurahisha wageni wachache” alisema Dkt. Sewangi.
Aidha, aliongeza kuwa katika kuhakikisha kuwa lugha ya kiswahili
inatumiwa vizuri, Baraza hilo linaendelea kutekeleza mkakati wa
kukamilisha kanuni zitakazopelekwa bungeni ili kumuwezesha Waziri mwenye
dhamana kuwa na mamlaka ya kusimamia sheria ya lugha ya Kiswahili ya
mwaka 1961 iliyorekebishwa mwaka 1985 ili kuipa nguvu ya kumshitaki mtu
yeyote kwa matumizi mabaya ya lugha hiyo.
Kwa upande wake Mkurugenzi,Taasisi ya Taaluma za Kiswahili chuo
kikuu cha Dar es Salaam Dkt. Ernesta Mosha ameziomba ofisi za Serikali
hususani mahakama kutumia lugha ya Kiswahili kwa kuwa ni lugha
inayoeleweka na Watanzania wengi ikizingatiwa kuwa sio wote wanajua
kutumia lugha ya kiingereza.
No comments:
Post a Comment