WAZIRI wa Ardhi, Maendeleo na Makazi, William Lukuvi,
ameonya baadhi ya vigogo wenye mawazo ya kuingilia mpango wa kurasimisha makazi
holela kwa lengo la kuwadhulumu viwanja wakazi wamaeneo husika watambue kuwa
watakuwa ni sawa na jipu.
Lukuvi, aliyasema hayo wakati wa uzinduzi wa mpango rasmi
wa kitaifa wa kurasimisha makazi holela, unaotarajiwa kuanza Machi 9 mwaka huu
na uzinduzi huo uliyofanyika katika Mtaa
wa Kirungure, Kimara wilayani Kinondoni jana jijini Dar es Salaam.
Alisema wananchi wanatakiwa kutambua kuwa urasimishaji
utaumiza baadhi ya watu hivyo wanachi hao lazima wawe tayari kujitolea na
kushiriki mpango huo.
Uzinduzi huo, pia ulifanyika katika vijiji vya Chasimba,
Chatembo na Chachui maeneo ambayo yanadaiwa kuwa wanaishi wavamizi wa Ardhi.
Lukuvi, alisema hayo kwa vile maeneo hayo yanawahusu
wakazi masikini ambao walikuwa wakiishi katika makazi hayo holela, kwahiyo
yanapimwa ili wakazi hao waweze kutambulika kihalali na kupatiwa huduma za
kijamii na wala haiwahusu vigogo wakiwemo matajiri kutoka maeneo mingine.
"Nawaonya wanasiasa na baadhi ya matajiri kuacha kufikiri kwamba huu ndiyo wakati wao wakuja hapa kujipatia nyarubanja kama ulikuwa unaishi Kariakoo au sehemu nyingine endekea kuishi huko huko, lakini hapa marufu,"alionya Lukuvi.
Alisema, yeyote atakayejaribu kukwepesha mpango huo kwa
kuwadhulumu wakazi ambao walipaswa kunufaika na urasimishwaji huo, basi ajue
serikali haitamvumilia na hatua kali dhidi yake zitachukuliwa.
“Mpango unatarajia kuanza Machi 9 mwaka huu, utasaidia
katika kuwafanya wakazi wote waliyokuwa wamejenga bila ya kufuata taratibu za
mipango miji kutambulika kutoka makazi holela hadi makazi halali,” alisema
Lukuvi.
Lukuvi, alisema mpango huo wa upimaji umekwishaanza
katika maeneo hayo na unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi mitatu Kisha Hati
za umiliki wa viwanja hivyo vilivyopimwa zitagawiwa kwa wananchi ndani ya mwezi
mmoja.
Hata hivyo, Lukuvi alisema katika kulipia Hati hizo kwa
mwenye uwezo anaweza kulipia Hati hiyo ndani ya mwezi mmoja na kwale ambao
hawana uwezo watalipia hati hiyo kidogo kidogo ndani ya mwaka mmoja.
“Nisisikie kuna mwanasiasa ambaye hakuwa anaishi hapa
kesho na kesho kutwa anakujakutaka eneo hapa kwani tunajua wazi kuwa maeneo
haya yana wenyewe na mkimuona mtu asiyehusika toeni taarifa,”alisema Lukuvi.
Lukuvi alionya kwa yeyote atakayejiingiza kinyume cha
taratibu atambuye kuwa yeye ndiyo anapitisha Hati hizo hivyo akibaini jina la mtu asiyehusika
ataliondoa.
Pia aliwataka wananchi wa kimara kuwa na ushirikiano
kwani mpango huo umeanzia kwao huku akiwataka wawe mfano wa kuigwa.
Urasimishaji huo utasaidia kata zao kuwa na barabara
inayoeleweka,shule,zahanati,maji pamoja na soko katika maeneo hayo.
Chasimba, Chachui na Chatembo
Aliwataka wakazi wa vitongoji hivyo kuhakikisha kuwa
mpango huo wa urasimishaji huo unafanikiwa kwa vile eneo hilo siyo lao bali
wanaishi hapo wakiwa wavamizi wa eneo la Twiga Cement.
Alisema mpango wa upangaji,upimaji,ugawaji na
umilikishwaji wa eneo utazikatia sensa iliyofanyika mwaka 2012 ambapo kulikuwa
na wakazi 4000.
Lukuvi alisema hata watambua wale walioenda kujenga na
kununua viwanja maeneo hayo baada ya sensa kupita.
Pia alimtaka mmiliki wa kiwanda cha Twiga simenti aweke uzio katika maeneo yote
ili wanachi wasiendelee kuvamia eneo hilo na kuepuka madhara yatakayo jitokeza
kwani wanalipua baruti.
Alisema wakazi wa maeneo hayo watambue kuwa gharama zote
zitakazo hitajika katika kupima maeneo hayo watalipa wenyewe kwasababu ni
wavamizi.
“Gharama za kumlipa mwenye kiwanda serikali itawasaidia
ili tupate hekta 224 zitakazo watosha ninyi wote”alisema Lukuvi.
Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea akizungumza kwa nyakati
tofauti akiwa Kirungure na kwa niaba ya mbunge wa Kawe Halima Mdee katika
vitongoji hivyo vitatu alishauri wakazi hao kukubali mpango huo uaze mara moja kwa sababu unalengo la kubadili
maisha yao.
“Mkiruhusu mpango huu usimame tu kwa ajili ya mvutano juu
ya kamati ambayo mnadai ichaguliwe nyingine kuna hatari mpango huo ukachukua
miaka mingi hadi kuanza kwake tena,”alisema Kubenea.
Alisema, utakapokamilika utaweza kuwasogezea huduma zote
za kijamii ikiwemo hospitali, masomo na Shule na kwamba watoe ushirikiano kwa
Kamati ya vitongoji hivyo, na inayosimamia mpango huo.

No comments:
Post a Comment