KAMA UNA TUKIO LOLOTE LA KIJAMII, SIASA, UCHUMI TUWASILIANE KWA E-mail: shehesemtawa@gmail.com SIMU: 0719 352 268

Sunday 12 July 2015

MGOMBEA URAIS UKAWA KESHO KUTWA

HATIMAYE Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) umeitangaza Julai 14, mwaka huu ndiyo siku ambayo watamtangaza mgombea wa kiti cha urais katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu.
Siku hiyo ya Jumanne wiki ijayo itahitimisha kimya cha muda mrefu na sintofahamu ndani ya umoja huo unaoundwa na vyama vinne ambavyo ni NLD, CUF, NCCR-Mageuzi na Chadema kumsimamisha mgombea mmoja katika nafasi ya udiwani, ubunge na urais.
Kauli hiyo ya Ukawa waliitoa jana baada ya kumalizika kwa kikao kilichowashirikika viongozi wa juu wa vyama hivyo, wabunge kutoka vyama vyote pamoja na taasisi zake za ufundi.
Mkutano huo ulioanza alasiri ulifanyika katika ukumbi wa jengo la Millennium Kijitonyama jijini Dar es Salaam na kumalizika saa mbili usiku.
Baada ya mkutano huo kumalizika baadhi ya viongozi wa umoja huo walizungumza na waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari waliokuwa eneo hilo tangu kuanza kwa kikao hicho kilichotanguliwa na kikao cha viongozi wa juu wa Ukawa.
Mwenyekiti mwenza wa Ukawa ambaye pia ni Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, akizungumza kwa niaba ya wenzake alisema mazungumzo yanakwenda vizuri ikiwa ni pamoja na kuyagawa majimbo ya uchaguzi.
“Naomba niwaleze kwamba mkutano wetu umekwenda vizuri na Julai 14, mwaka huu ndiyo siku ambayo tutamtangaza mgombea wetu wa kiti cha urais atakayepeperusha bendera ya Ukawa,” alisema Profesa Lipumba na kuongeza:
“Kuna mambo muhimu ambayo tunakwenda kuyaweka sawa katika vyama vyetu ambayo ni ya kiufundi ili tutakapoanza kusiwepo na mkanganyiko.”
Profesa Lipumba ambaye ni miongoni mwa waliochukua fomu ndani ya chama chake akisubiriwa kushindanishwa na wagombea wengine alisema: “Katika majimbo, asilimia 97 ya majimbo yote 189 tayari yamegawanywa, bado kama asilimia tatu.”
Alisema watamsimamisha mgombea atakayekwenda kupambana na vitendo vya rushwa, kusimamia maadili na rasilimali za taifa ambazo Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeshindwa kuzisimamia kwa kipindi kirefu.
“Wananchi walitoa maoni yao katika Rasimu ya Katiba na CCM wakayatoa, hivyo Ukawa tutahakikisha maoni yao yanazingatiwa na kurejeshwa,” alisema na kuongeza:
“Tunataka kumsimamisha mgombea ili kufanya mabadiliko kwa Watanzania na kuhakikisha tunaiangusha CCM katika uchaguzi ujao kwani CCM wameshaanza kushindwa hata ukiona hali ilivyo huko Dodoma.”

Mvutano ndani ya kikao

Habari kutoka ndani ya kikao hicho zinaelezwa kuchelewa kutangazwa kwa mgombea wa nafasi ya urais inatokana na mvutano uliopo baina ya vyama viwili vyenye nguvu.
Awali jana katika mitandao mbalimbali ya kijamii zilienea taarifa zilizokuwa zinazungumzia kuvunjika kwa umoja huo kutokana na vyama kutokukubaliana katika kumsimamisha mgombea wa nafasi ya urais.
“Unajua hii kitu ingekuwa imeshakamilika zamani kama ambavyo tulikuwa tumekubaliana lakini tatizo limejitokeza hivi karibuni baada ya chama kimoja kutaka kumsimamisha mgombea wa nafasi ya urais lakini chama kingine nacho hakitaki,” kilisema chanzo kimoja kikiomba hifadhi ya jina.
Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (CCM), awali akizungumza na waandishi wa habari baada ya kubanwa alisema mazungumzo yanaendelea vizuri licha ya kuwapo kwa kila chama kutaka hiki au kile.
“Kule ndani mazungumzo yako vizuri na Ukawa tutajitahidi sana kuhakikisha tunamsimamisha mgombea na kuwaondoa CCM ambao wameshindwa kwa kiasi kikubwa na dalili inajionyesha huko Dodoma wanavyoshindwa kupata muafaka vizuri,” alisema Kafulila.
Akitolea ufafanuzi suala hilo, Profesa Lipumba alisema hakuna mvutano wowote ndani ya Ukawa na kilichojitokeza ni masuala madogo madogo ambayo wanakwenda kuyafanyia kazi katika vyama vyao.
Naye Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Mosena Nyambabe, aliyemwakilisha Mwenyekiti wa chama hicho, James Mbatia, ambaye hakuwapo kutokana na kile kilichoelezwa anaumwa alisema tatizo lililopo hawakuwa wameandaa utaratibu wa kumpata mgombea urais.
“Unajua bwana katika vikao vyetu tulikuwa hatujaweka utaratibu mzuri wa kumpata mgombea wa urais lakini hili halina tatizo na tunakwenda kumaliza na tutamtangaza mgombea wetu,” alisema Nyambabe.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alipoulizwa na Tanzania Daima Jumapili kuhusu mvutano huo wa vyama viwili alikiri kuwapo kwake lakini alisema unaelekea kumalizwa na kila kitu kitakaa sawa.


CHANZO TANZANIA DAIMA

No comments:

Post a Comment