KAMA UNA TUKIO LOLOTE LA KIJAMII, SIASA, UCHUMI TUWASILIANE KWA E-mail: shehesemtawa@gmail.com SIMU: 0719 352 268

Friday, 1 July 2016

WAKAZI 65, WA BONDE LA MKWAJUNI WAOMBA MSAADA KWA RAIS MAGUFULI

WAKAZI 65 ambao wamebomolewa nyumba zao katika bonde la Mkwajuni wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam, wameiomba serikali ya Rais John Magufuli, iwapatie msaada wa kibinadamu.
Wakazi hao wanahitaji msaada ikiwa ni pamoja na mahitaji ya kijamii kwa vile tangu nyumba zao zilipobomolewa kimakosa ni zaidi ya miezi sita huku wakiishi katika vibanda bila ya msaada wowote kutoka serikalini.
Wakizungumza na wandishi jijini jijini, kwa nyakati tofauti, wakazi hao walisema wamekuwa wakiendelea kuishi katika mazingira hayo magumu, kwa sababu ya kuasubiri uamuzi wa serikali ambayo iliahidi kwa wale waliyokuwa wamejenga kutokana na vibali walivyopewa na maofisa wa serikali wangefidiwa.
Miongoni mwa wakazi hao ni Sabrina Hilal (63), alisema wamefikia hatua hiyo kwa vile wakati nyumba zao zinabomolewa wakazi hao walikuwa na hati halali hivyo kuahidiwa kuwa wangelipwa fidia kwa ajili ya kwenda kuanza maisha mapya sehemu nyingine.
“Tunamuomba Rais Magufuli, atusaidie kwani tunadhani yeye ndiyo mtu wa mwisho ambaye anaweza kutuokoa katika maisha haya magumu kwenye hivi vibanda tunamoishi, atusaidie tuondoke hapa,” alisema Sabrina.
Alisema, tangu opeaheni ya bomoabomoa ya nyumba zilizojengwa katika maeneo ya mabondeni na hatarishi ni zaidi ya miezi sita sasa lakini walipopewa hadi kwamba wangefidiwa hakuna kitingozi yoyote wa serikali aliyewatembelea kuja kujua hatima ya maisha ya wakazi hao.
“Sisi tumebomolewa nyumba zetu lakini tuna hati ambazo tulipewa na Manspaa Kinondoni huku tukilipa hata kodi zaajengo, leo tunashangazwa na ukimnya wa Manispaa yetu”alisema.
Alisema kuwa haki ya kuishi katika vibanda hivyo kumekuwa na madhara makubwa sana ikiwemo watoto kubanwa na kifua kutokana na hali ya hewa ya kipupwe.
Mwanaidi Idd, alisema kwa vile Rais Magufuli ameaikika mara kwa mara nia ya serikali yake ni kusaidia wananchi hivyo anaamini kuwa atalishugulikia suala hilo ili haki ipatikane.
Alisema wanamuomba Rais Magufuli, afanye ziara ya kushtukiza ili kwenda kujionea maisha wanayoishi wananchi wake waliyompigia kura katika uchaguzi mkuu uliyofanyika mwaka jana.

Aidha, Mwanaidi, alishauri serikali kuwachukulia hatua za kishwria kwa maofisa wote wa manispaa ya Kinondoni, ambao walihusika katika utoaji wa vibali vya ujenzi katika maeneo hayo huku wakijua ni hatarishi.

NYANDUGA: JUKUMU LA KUSIMAMIA HAKI ZA BINADAMU SIYO LA SERIKALI PEKEE

MWENYEKITI wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Bahame Nyanduga amesema kuwa jukumu la usimamizi na utetezi wa masuala ya haki za binadamu sio jukumu la Serikali, Asasi za kiraia wala mtu binafsi, ni jukumu la watu wote.
Nyanduga aliyasema hayo jana alipokuwa akifunga mkutano wa siku tatu wa wadau wa haki za binadamu uliofanyika jijini Dar es Salaam kujadili mapendekezo ya tathimini ya utekelezaji wa masuala ya haki za binadamu.
Katika mkutano huo, Nyanduga alisema kuwa haki za binadamu zinamuhusu kila mmoja wetu, hivyo ni muhimu kwa tume na asasi za kiraia kushirikiana kwani wote wanafanya kazi moja ya kujenga taifa lenye kuheshimu haki za binadamu.
“Tume haichagui nani wa kushirikiana nae kwa kuwa masuala ya haki za binadamu sio miliki ya serikali, asasi za kiraia wala mtu binafsi, bali ni jukumu letu sote” alisema.
Aliongeza kuwa: “ni muhimu tukashirikiana sisi wote kwa kuwa lengo letu ni kujenga taifa lenye kuheshimu haki za binadamu” 
Aidha, Nyanduga alisema baada ya kumalizika kwa mkutano huo ni muhimu kwa tume na asasi za kiraia kukaa pamoja ili kuyapitia vizuri mapendekezo hayo ambayo wamekubaliana na kuandaa taarifa ambayo wataiwasilisha serikalini kwa ajili ya kuishawishi serikali iweze kuyakubali mapendekezo hayo ambayo awali iliyakataa.
Awali, Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Olengurumwa, aliwataka wanahabari kutumia fursa waliyoipata katika mkutano huo kuelimisha jamii kuhusu mchakato mzima wa tathimini ya utekelezaji wa masuala ya haki za binadamu.
“Mkutano huu umekuwa ni fursa kwenu wanahabari  kujua namna mchakato wa tathimini ya utekelezaji wa masuala ya haki za binadamu unavyokuwa kwa kuwa hamkuwepo Geneva, lakini kupitia mkutano huu mumeweza kuelewa, hivyo naomba mtumie fursa hii kuelimisha jamii kuhusu mchakato huo”, alisema Olengurumwa
Olengurumwa aliipongeza tume kama taasisi ya kitaifa inayosimamia masuala ya haki za binadamu kwa ushirikiano wao mkubwa ambao wamekuwa wakiendelea kuutoa kwa asasi za kiraia na  aliiomba taasisi hiyo kuendelea kufanya hivyo kwani ndio njia pekee itakayosaidia kupiga hatua kubwa katika masuala ya usimamizi wa haki za binadamu kama nchi.

Itakumbukwa kuwa Juni 27-29 mwaka huu, wadau wa haki za binadamu walikutana jijini Dar es Salaam kujadili mapendekezo ya tathmini ya utekelezaji wa masuala ya haki za binadamu nchini ili kupanga mikakati ya kuweza kuishawishi serikali kuyakubali mapendekezo iliyokataa katika mkutano wa Baraza la Haki za Binadamu uliofanyika Geneva Mei, mwaka huu.  katika Mkutano huo mapendekezo ya jumla yalikuwa 227, serikali ilikubali mapendekezo 130 na kuyakataa 72  na 25 iliyaweka pembeni.

Saturday, 11 June 2016

MFUMUKO WA BEI WA TAIFA WAONGEZEKA MEI

OFISI ya Taifa ya Takwimu (NBS), imesema Mfumuko wa Bei wa Taifa kwa Mei, 2016 umeongezeka kidogo hadi kufikia asilimia 5.2 kutoka asilimia 5.1 ilivyokuwa katika kipindi cha Aprili, 2016.
Hali hiyo inamaanisha kuwa kasi ya upandaji wa bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia mwezi Mei, 2016 imeongezeka kidogo ikilinganishwa na kasi iliyokuwepo kwa mwaka ulioishia mwezi Aprili, 2016.  Akizungumza na wa andishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mkuu wa NBS, Dk. Albina Chuwa iliyotolewa leo Jijini Dar es Salaam, kuongezeka kwa Mfumuko wa Bei wa mwezi Mei, 2016 kumechangiwa na kuongezeka kwa bei za baadhi ya bidhaa za vyakula na zisizo za vyakula.
 Alisema, baadhi ya bidhaa za vyakula zilizochangia kuongezeka kwa mfumuko huo wa bei ni pamoja na asilimia ikiwa ndani ya mabano kuwa ni mahindi (1.5), unga wa muhogo (6.2), nyama ya kuku (2.6), njegere (5.8), mihogo mibichi kwa (8.0) na ndizi za kupika (2.7).
“Pia bidhaa zisizo za vyakula zilizochangia kuongezeka kwa Mfumuko wa Bei ni pamoja na mafuta ya taa (2.9), mkaa (2.5), dizeli (4.6), petrol (2.5) na vifaa vya michezo (7.8).
Dk. Chuwa alifafanua kwa kusema mfumuko huo wa bei katika kipindi cha Mei, 2016 unaopimwa kwa kipimo cha mwezi umebaki kuwa asilimia 0.5 kama ilivyokuwa Aprili, 2016. Aidha, Fahirisi za Bei zimeongezeka hadi 103.00 katika kipindi cha Mei, 2016 kutoka 102.46 mwezi Aprili, 2016.
 Aidha, ulinganifu wa mfumuko wa mei kwa baadhi ya  nchi  za Jumuia ya Afrika Mashariki, inaonyesha kuwa Mfumuko wa Bei nchini Uganda kwa mwezi Mei, 2016 umeongezeka hadi kufikia  asilimia 5.4 kutoka asilimia 5.1 kwa mwezi Aprili, 2016.
 Dk. Chuwa, akisema kwa upande wa Kenya, Mfumuko wa Bei umepungua hadi kufikia asilimia  5.00 kwa mwezi  Mei, 2016 kutoka asilimia 5.27 iliyorekodiwa mwezi Aprili, 2016.
 Mfumuko wa Bei wa Taifa kwa kipimo cha mwaka unapima kiwango cha kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma zote zinazotumiwa na kaya binafsi.
 

Saturday, 28 May 2016

PROFESA MBARAWA AWATAKA MAKANDARASI NCHINI KUUNGANA.

WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa, amesema Serikali itaweka mazingira wezeshi ili kuwawezesha Makandarasi wazawa kupata miradi mingi ya ujenzi wa miundombinuya nchini.
Akifunga mkutano wa siku mbili wa Makandarasi Prof. Mbarawa amesema, Serikali itatenga miradi mikubwa maalum kwa ajili ya Makandarasi wazawa ili kuwajengea uwezo.
“Kazi yenu ni moja tu ni kuwajengea watanzania miundombinu iliyobora ili wa/kie uchumi wa kati i/kapo 2025”, amesema Prof. Mbarawa.
Amesisitiza umuhimu wa Makandarasi wazawa kuungana ili waweze kupata miradi mingi ya Serikali na kuijenga kwa muda sahihi kwa thamani inayowiana na fedha wanazolipwa.
Amezitaka Taaasisi za fedha nchini zipunguze riba za mikopo kwa Makandarasi wazawa ili kuwawezesha kukua na hivyo kupata miradi mingi ya ujenzi ndani na nje ya nchi.
“Changamkieni fursa katika ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Tanga-Tanzania hadi Hoima- Uganda (km 1410), ujenzi wa reli ya kati na ujenzi wa viwanda vikubwa vya kati na vidogo”,amesisitiza Prof. Mbarawa.
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Joseph Nyamhamga, amewataka Makandarasi kujipanga vizuri kutumia fursa zilizopo katika bajeti ijayo kwa kujenga miradi kwa ubora na gharama sahihi.
Amewaonya Makandarasi kuacha kufanya kazi chini ya kiwango na kujiepusha na vitendo vya rushwa kwani husababisha miradi kutokuwa na ubora uliokusudiwa.
Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya Makandarasi Mhandisi Consolata Ngimbwa amemhakikishia Waziri Prof. Mbarawa kuwa Makandarasi wazawa wataungana katika kutekeleza miradi mikubwa na kuiomba Serikali watengeneze mazingira ya Makandarasi wazawa kushirikiana na Makandarasi wa nje katika ujenzi wa miradi mikubwa.
Asilimia 46 ya Bajeti ya Maendeleo ya mwaka 2016/2017 imetengwa kwa ajili ya ujenzi wa miradi mbalimbali ya miundombinu hapa nchini.

CHAKUA: TEMESA PUNGUZENI TOZO YA KUVUSHA DALADALA KATIKA DARAJA LA KIGAMBONI


MWENYEKITI WA CHAKUA, HASSAN MCHANJAMA (KUSHOTO), AKIWA NA OFISA WAKE, GERVAS RUTAGUZINDA

CHAMA cha Kutetea Abiria (Chakua), kinatarajia kukutana na Wakala wa Ufundi na Umeme (Temesa), ili kujadili tozo ya sh. 7000 ya kuvusha magari ya kusafirisha abiria (daladala), katika daraja la Kigamboni ambayo ina lalamikiwa na wamiliki wa vyombo hivyo kuwa ni kubwa.
Mwenyekiti wa Chakua, Hassan Mchanjama, aliyasema hayo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wa miliki wa daladala hizo, kudai kwamba wameshindwa kulipa tozo hiyo, hivi sasa baadhi yao wamesitisha huduma kwa vile wamekuwa wakipata hasara kila waanapovusha magari yao.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo, Mchanjama, alisema lengo la kukutana na Temesa wiki ijayo ni kutaka kuona wamiliki hao wanasikilizwa lakini kubwa ni kutetea ambiria wao.
Alisema, wamefikia hatua hiyo baada ya kusikia kuwa baadhi ya wamiliki wa daladala hizo kusitisha huduma katika ruti hiyo, kwa kuogopa tozo hiyo kwa kila safari, hali ambayo imesababisha kukosekana kwa usafiri kwa wakazi wa Kigamboni.
“Chakuwa imepokea malalamiko kutoka kwa abiria pamoja na wamiliki wa daladala kuwa daladala zao zinatozwa ushuru wa sh.7000 kwa kila safari moja kwa siku karibu sh. 150,000  huku wakipata hasara kutokana na hali hiyo wamiliki wameacha kupeleka magari na kufanya abiria wahangaike kwa kukosa usafiri.
“Tunatambua juhudi za serikali ni kuwapunguzia adha ya usafiri wananchi wake, lakini kutokana na malalamiko hayo ya abiria yanaondoa matumaini yao ya kuondokana na adha hiyo ya usafiri kwani hivi sasa baadhi wameanza kusafiri na vyombo vya majini ambavyo usalama wake ni mdogo hivyo kuhatarisha maisha ya abiria hao,”alisema Mchanjama.
Mchanjama, alisema Chakua wanatarajia kuishauri Temesa kuangalia tozo hiyo upya kwa lengo la kuifanyia marekebisho ili wamiliki hao waweze kutoa huduma kwa abiria wao ambao hivi sasa wanataabika.

MARWA: SPIKA WATAJE WANAOINGIA BUNGENI WAKIWA WAMETUMIA KILEVISPIKA wa Bunge Job Ndugai ametakiwa kuweka hadharani majina ya wabunge, aliyodai kuwa wamekuwa wakiingia bungeni huku wakiwa wametumia kilevi.
Kauli hiyo inakuja siku chache baada ya Rais John Magufuli kutengua uteuzi wa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga, anayedaiwa kuwa alionekana amelewa muda wa kazi pale alipokuwa akijibu maswali ya wabunge katika kipindi cha maswali na majibu bungeni.
Akizungumza na wandishi wa habari jijini Dar es Salaam, jana Mwenyekiti wa Jukwaa la Watetezi wa Rasilimali wasiokuwa na Mipaka (WARAMI), John Marwa, alisema wanampongeza Rais kwa hatua aliyochukuwa dhidi ya waziri huyo kwa vile itakuwa fundisho kwenye jamii iliyozoea kuishi maisha ya mazoea.
Alisema wamefikia hatua hiyo, kutokana na kiongozi huyo wa Bunge kukiri akiwa bungeni kwamba kuna wabunge wanakuwa wa,elewa hata kuvuta bangi wakati wa mikutano ya Bunge ikiendelea hali iliyowafanya wananchi kupoteza imani na chombo hicho muhimu.
“Kwa sababu Bunge ni chombo ambacho kinasemea wananchi dhidi ya Serikali na kama kiongozi wa Bunge amekiri jambo hili tunamtaka aweke wazi majina ya hao Wabunge hadharani ili chombo hicho cha uwakilishi kirudishe heshima yake kwa Umma.
“Pia tunaomba sheria kali zitungwe ili kukidhi na kutoa adhabu kali kwa Wabunge watakaobainika kujihusisha vitendo hivyo vya aibu wa wapo ndani Bunge,”alisema Marwa.
Aidh, Marwa alisema endapo kiongozi huyo atashindwa kutaja majina ya wabunge hao, basi watamtaka awaombe radhi wabunge na Watanzania ili waendelee kuwa na imani na wabunge wao.
“Hatuwezi kusema tutamchukulia hatua gani endapo atashindwa kufanya hivyo,  cha msingi hapa ni suala la tunasubiri muda,”alisema Marwa.
Katika hatua nyingine Mkurugenzi wa Jukwaa la Watetezi wa Rasilimali wasiokuwa na Mipaka WARAMI, Evance Kamenge, alimelitaka Jeshi la Polisi Kitengo cha Usalama Barabarani (Trafic), kupitia upya sheria ya barabara za Mabasi ya endayo haraka, ikiwa ni pamoja na kutambua kuwa yale ni magari na siyo treni.
“Waifahamishe Kampuni ya UDRT kwamba, lazima waajiri madereva wenye sifa za kuendesha magari ya abiria, pili  madereva watambue kuwa wanaendesha magari siyo treni.
“Kwa kuwa huu ni usafiri mpya WARAMI tunapendakeza Mwekezaji wa mradi huu ahakikishe anatoa ajira kwa madereva wenye sifa stahiki na wanaojua vema sheria za barabarani  kwani tumebaini wapo baadhi ya madereva ambao wamejenga kiburi kwa kuitumia vibaya sheria ya mbasi hay,”alisema Kamenge.
Aidha, Kamenge, WARAMI, inamtaka mwekezaji kuangalia uimarishaji wa vitoa ishara au honi kwa mabasi yake upya kwani hadi sasa havijakuwa msaada wa kuepusha ajali katika makutano ya barabara.
Alisema tangu kuanza mradi huo takribani wiki mbili sasa tayari kuna kumeripotiwa vifo vya watu watano waliyofariki kwa ajali zilizotokana na uzembe wa madereva wa mabasi hayo au watumiaji wa barabara hizo.
Kamenge, alisema wakati mwingene watumiaji wa barabara hizo, wamekumbwa na ajali hizo kutokana na kutoelewa matumizi ya barabara hizo kwani baadhi yao wamekuwa wakiingia kwenye njia hizo hali inayosababisha wagongwe.
Pia, alisema WARAMI inapendekeza Kamati ya Usafirishaji pamoja na Mkuu wa Mkoa kukaa chini upya kutafakari matumizi ya barabara hiyo hususan kwa wavukao kwa miguu.