KAMA UNA TUKIO LOLOTE LA KIJAMII, SIASA, UCHUMI TUWASILIANE KWA E-mail: shehesemtawa@gmail.com SIMU: 0719 352 268

Friday 27 February 2015

WADAI VYOMBO VILIVYOHIFADHIA KINYESI




VIJANA wanaodaiwa kuwa walitumwa na Mwalimu wa Shule ya Sekondari Kibasila, Gaudensia Albert, aliyeishi na kinyesi kilichochanganyika na matapishi kwa muda wa miaka miwili, juzi walikwenda kudai vyombo vilivyokuwa vimehifadhi uchafu huo.
Mrundikano wa uchafu huo uliteketezwa juzi chini ya uangalizi mkali wa Jeshi la Polisi na maofisa  Afya wa Manispaa ya Temeke, wakishirikiana na Ofisi ya Serikali ya Mtaa wa Kisiwani, Kata ya Sandari, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na Tanzania Daima jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa mtaa huo, Yahya Bwanga, alisema haelewi vijana hao ambao hakujua idadi yao walikuwa na lengo gani.
Alisema  vijana hao walijitokeza juzi  na kujitambulisha kuwa ni ndugu wa mwalimu huyo na kwamba walitumwa kuchukua vyombo hivyo.
“Juzi usiku walikuja vijana kwenye ofisi yetu ya serikali ya mtaa wakati mimi sikuwepo, lakini walimkuta mjumbe akawahoji wakaonekana wamekuja kuchukua vile vyombo vilivyokuwa na  uchafu kwamba walitumwa na yule dada.
“Kwa kweli sisi tunashangaa kwa vijana hao kudai vyombo hivyo, kwani tulitarajia kuwa wangeulizia kuhusu vyombo vile ambavyo vimebaki chumbani kwake, leo wanauliza kuhusu vile vichafu, ni ajabu kwa kweli,” alisema Bwanga.
Bwanga alisema vijana hao waliwafahamisha kuwa vyombo havikuwepo kwa vile kazi ya kuteketeza uchafu huo ilifanywa na manispaa, hivyo kama walikuwa wakivihitaji wanapaswa waende huko.
“Hapa ndipo penye utata, juzi tumeambiwa kuwa yuko Muhimbili anapimwa akili, leo tunaambiwa kuwa anadai vyombo vyake. Tumewaambia waende manispaa, kwani wale ndio wanaojua kama vyombo vile kitaalamu vina maradhi au la, pia wameondoka navyo,” alisema Bwanga.
Naye Reuben Shayo, baba mwenye nyumba wa Gaudensia, alisema usalama wa vyombo vyake upo kwa vile Diwani wa Sandari, Abel Tarimo, alinunua kufuli jipya kwa ajili ya kufunga mlango wa chumba hicho chini ya ulinzi wa viongozi wa kata wakiongozwa na Sajenti wa Polisi, Ramadhani Kagolo, huku funguo akikabidhiwa Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa.
Hata hivyo jitihada za kumpata mwalinu huyo zimegonga mwamba kutokana na simu yake kuita muda mrefu bila kupokewa tangu lilipotokea tukio hilo.
Wakati wa uteketezaji wa uchafu huo, Ofisa wa Afya wa Manispaa ya Temeke, Floyd Tembo, alisema mwalimu huyo alikuwa amelazwa Muhimbili.
Tukio hilo ambalo limewaacha wakazi wa eneo hilo na maswali mengi, lilitokea Februari 22 na kuteketezwa Jumatano Februari 25, mwaka huu.

No comments:

Post a Comment