KAMA UNA TUKIO LOLOTE LA KIJAMII, SIASA, UCHUMI TUWASILIANE KWA E-mail: shehesemtawa@gmail.com SIMU: 0719 352 268

Monday 2 March 2015

JAMII YATAKIWA KUJIFUNZA

Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, amesema jamii wakiwemo viongozi wanapaswa kujifunza kwamba maisha ya duniani si ya kudumu, hivyo wanatakiwa kutenda wema wakati wote.
Salamu za Mbowe ambaye hata hivyo hakuweza kuhudhuria kutokana na kwamba yuko safarini kikazi, zilitolewa kwa niaba yake na Mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nassari, ambaye alisema wameguswa na msiba wa mbunge mwenzao.
“Nimesimama hapa kutoa salamu za Kiongozi wa Kambi ya Upinzani  Bungeni, Freeman Mbowe, ambaye yupo safarini …lakini pia sisi na wabunge wenzetu wa upinzani tuko hapa kumsindikiza mbunge mwenzetu katika safari yake ya mwisho, hivyo itikadi zetu tunaziweka pembeni.
“Katika kipindi kama hiki ambacho akizoeleki, tunapaswa kujifunza kwamba maisha ya hapa duniani si ya kudumu, hivyo tunapaswa kutenda mema ili tutakapoitwa tuwe salama …na katika kufanya hivyo tuongozwe na Kitabu cha Biblia cha Zaburi kinachosema ‘Nitayainua macho yangu, nitazame milima…” alisema Nassari.
Miongoni mwa viongozi na wabunge wa upinzani waliokuwapo katika Viwanja vya Karimjee kumuaga Kapteni Komba ni pamoja na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, Mwenyekiti wa TLP, Augustino Mrema, Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi, Mbunge wa Mbozi Mashariki (Chadema), David Silinde na Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Naomi Kaihula.

Salamu za CCM

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, alisema marehemu Komba atakumbukwa na wengi kwa sababu alikuwa mfano wa kuigwa kwa Wana CCM, wanasiasa na wasanii kutokana na mchango wake wa maneno na hamasa katika nyimbo zake.
Kinana alisema alikuwa na kipaji cha pekee kutunga na kuimba nyimbo za CCM katika chaguzi na za kitaifa, za furaha na huzuni, hata kuwatia moyo Watanzania katika tukio hilo husika.
Kinana alitoa mfano kwamba mwaka 1978 wakati wa vita ya kumng’oa Idd Amin katika ardhi ya Tanzania, marehemu Komba aliwatia hamasa wanajeshi wenzake kwa kuhamasisha kwa nyimbo mbalimbali katika mapambano. 
 “Si kwa tukio la vita ya Idd Amin tu, Komba aliimba wakati wa msiba wa Mwalimu Julius Nyerere, marehemu Komba atakumbukwa sana na wengi kwa sababu alikuwa ndugu, rafiki, mwalimu, mwanajeshi, mwanasiasa, mtumishi hodari na mzalendo kwa taifa lake.
“CCM tutamuenzi marehemu Komba kwa mengi aliyoyafanya katika chama na taifa …ametangulia nasi tutafuata kwa sababu kifo hakikwepeki, chama kinatoa salamu za rambi rambi kwa Bunge, Serikali na sh. milioni tano kwa familia kufuatia msiba huu mzito,” alisema Kinana.


No comments:

Post a Comment