RAIS Jakaya Kikwete leo alishindwa kujizuia na kujikuta
akibubujikwa na machozi wakati wa hafla ya kuuga mwili ya Marehemu, Mbunge Mbinga Magharibi, Kapteni John Komba.
Mbali ya Rais Kikwete baadhi viongozi mbalimbali waandamizi
wa vyama vya siasa na Serikali walimwaga machozi kumlilia Kapteni Komba
aliyefariki dunia juzi wakati akipatiwa matibabu katika hospitali ya TMJ,
jijini Dar es Salaam.
Hali hiyo ilijitokeza leo katika viwanja vya Karimjee ambao
ulitawaliwa na majonzi, vilio na huzuni wakati maelfu ya wakazi wa jijini la
Dar es Salaam na mikoa jirani walipojitokeza kuuaga mwili wa Kapteni Komba.
Walioibua vilio na hisia za kifo cha Kapteni Komba ni wasanii wa muziki wa dansi wakiongozwa
na mwanamuzii mkongwe King Kiki walipoimba wimbo na ‘Nani Yule’
Wimbo
huo ulitungwa na Kapteni Komba wakati wa kifo cha Baba wa Taifa mwaka 1999,
Mwalimu Nyerere, lakini jana wimbo huo huo ulibadilishwa baadhi ya maneno na
kuingiza jina la Marehemu Komba.
Baadhi
ya wasanii walioimba wimbo huo, Jose Mara, King Kik na wengine kwa kushirikiana
na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye waliimba kwa hisia kali na
kusababisha baadhi ya wananchi
waliohudhuria hafla hiyo akiwemo Rais Kikwete, kububujikwa na machozi.
Mbali
ya Rais Kikwete, viongozi wengine walioshindwa kujizuia ni pamoja na aliyekuwa
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Yusuf Makamba ambaye baadaye alisema chama hicho kimepoteza jino la dhahabu na
kubaki na pengo ambalo haliwezi kuzibika tena.
Baadhi
ya viongozi waliohudhuria shughuli hiyo ni pamoja na
Makamu wa Rais Dk. Mohamed Ghalib Bilal, marais wastaafu Ali Hassan Mwinyi na
Benjamini Mkapa, Katibu Mkuu Kiongozi Ombeni Sefue na wake zao pamoja na
Wengine ni mawaziri mbalimbali
wa sasa na zamani akiwamo Hussein Mwinyi (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa),
Sophia Simba (Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto), Aggrey Mwanri (Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri
Mkuu-Tamisemi).
Alikuwepo pia Asha Rose Migiro
(Sheria na Katiba), Lazaro Nyalandu (Maliasili na Utalii), Jenister Mhagama
(Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi), Januari Makamba (Naibu Waziri Sayansi
na Teknolojia), Mwigulu Nchemba (Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi) na wengine.
Baadhi ya wabunge waliokuwapo
katika hafla hiyo ni Edward Lowassa (Monduli) Iddi Azzan (Kinondoni),
Christopher Ole Sendeke (Simanjiro) Steven Ngonyani (Korogwe Vijijini), Mussa Zungu (Ilala) na wengine wa
viti maaluma.
Msajili wa Vyama vya Siasa,
Jaji Francis Mutungi, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Damian
Lubuva, Meya wa Jiji la Dar es Salaam Didas Masaburi, Meya wa Ilala Jerry Silaa
na viongozi wengine wa kiserikali.
Pia walikuwamo viongozi wa
taasisi binafsi akiwemo Mwenyekiti Mtendaji wa Makapuni ya IPP, Dk. Reginald Mengi, Mkurugenzi wa Msama
Promotion Alex Msama na wengine.
Shughuli
ya kutoa heshima za mwisho kwa Marehemu Kapteni Komba, ilianza majira ya saa tatu asubuhi.
Viongozi
mbalimbali wa serikali na vyama vya siasa na wananchi waliwasili kwa nyakati tofauti na kuchukua
nafasi zilizotengwa kwa ajili yao.
Mbunge
wa Arumeru Mashariki, Joshua Nasari, ambaye alimwakilisha Kiongozi wa Kambi ya
Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe alifika katika viwanja hivyo majira ya saa 4:33
asubuhi.
Spika
wa Bunge, Makinda aliwasili majira ya saa 4:39 asubuhi na kufuatiwa na Makamu
wa Rais Dk. Mohammed Gharib Bilali aliyewasili majira ya saa 4:50 asubuhi.
Ilipotimu
majira ya saa 5:15 asubuhi, Rais Kikwete aliwasili katika viwanja hivyo
akiambatana na mkewe, Mama Salma Kikwete.
Mwili
wa Kapteni Komba, uliwasili baada ya Rais Kikwete kufika uwanjani hapo,
ukiandamana na familia ya marehemu pamoja na ndugu wa karibu na majirani.
Watumishi
wa idara, taasisi na mashirika ya umma na binafsi, nao walifika kuuaga mwili wa
Kapteni Komba na kusababisha shughuli mbalimbali katika ofisi hizo kusimama.
Baada
ya mwili kuwasili, kulikuwa sala fupi iliyoendeshwa na Padri wa Kanisa la
Kikatoliki, Parokia ya Bikira Maria Mpalizwa ya jijini Dar s Salaam, Florian
Tindwa.
Wananchi wamzungumzia
Mwenyekiti
wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere Joseph Butiku alisema Kapteni Komba atakumbukwa
kwa kuwa msanii na kiongozi mahiri kupitia nyimbo zake.
“Wakati
wa uhai wake, hakuteteleka katika shughuli zake za kisanii hata alipokuwa
bungeni kwani alikuwa na uwezo wa kusimamia ukweli.
Vituko
Katika
hali isiyo ya kawaida wapiga picha kutoka kutoka vyombo mbalimbali vya habari,
walijengewa uzio uliyowafanya washindwe kufanya kazi zao kwa uhuru.
Hali
hiyo iliwafanya washindwe kupata picha nzuri na baadala yake kupata za upande mmoja.
Rais
Kikwete alipoona hali hiyo, aliagiza waandishi hao waachiwe waendelea na kazi
yao vila kuwekewa kizuizi.
Kepteni
Komba alifariki dunia Februari 28 katika Hospitali ya TMJ alipokimbizwa kupata matibabu ya ugonjwa wa kisukari.
Mwili
huo ulisafirishwa jana kwenda Songea kwa ndege maalum ya Serikali na mazishi
yanatarajiwa kufanyika leo katika kijiji cha Lituli alikozaliwa.
No comments:
Post a Comment