KAMA UNA TUKIO LOLOTE LA KIJAMII, SIASA, UCHUMI TUWASILIANE KWA E-mail: shehesemtawa@gmail.com SIMU: 0719 352 268

Tuesday 3 March 2015

KIJAZI AWATAKA WAKAZI MABONDENI WAONDOKE


MKURUGENZI wa Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA), Agnes Kijazi, amewataka wakazi wa maeneo ya Ziwa Victoria kuchukuwa tahadhari kutokana na mvua kubwa zinaotarajiwa kunyesha kuanzia sasa kuwa huenda zikasababisha hatari ya mafuriko.

Mkurugenzi huyo alikuwa akitoa muelekeo wa mvua za masika zinazotarajiwa kunyesha kuanzia Machi, Aprili na Mei mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na wandishi wa habari huku akiambatana na wadau wa Kilimo na Afya, Kijazi, alisema izingatiwe kuwa pamoja na kuwapo kwa uwezekano wa matukio ya mvua kubwa katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua juu ya wastani, hali hiyo pia inaweza kujitokeza katika maeneo ambayo yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi wa chini.

Alitaja maeneo hayo kuwa ni mikoa ya Kagera, Mara, Mwanza, Geita hata hivyo kuna baadhi ya maeneo  ya mikoa hiyo pamoja na Simiyu, Shinyanga vipindi vya mvua hizo zilikwishaanza tangu Februari mwaka huu,  zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani.

‘Msimu wa mvua unarajiwa kuanza mapema katika maeneo ya kanda ya ziwa Victoroa na baadhi ya maeneo ya ukanda wa Pwani ya Kaskazini,”alisema Agnes.

Adha, Alisema katika maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua, msimu huo wa masika utaanza Machi hadi Mei ambapo itakuwa ni mahususi katika maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki mwa mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara.

Vilevile katika Pawani ya kaskazini mwa mikoa ya Dar es Salaam Tanga, Pwani, Morogoro-kaskazini pamoja na Visiwa vya Unguja, Pemba na mikoa ya Kanda ya Ziwa victoria.

“Mvua za wastani hadi juu ya wastani tunazitarajia katika baadhi ya maeneo hususan kanda ya ziwa victoria na maeneo ya kusini ya nchi, hata hivyo, hali ya mvua haitakuwa ya kuridhisha katika maeneo mengi ya nchi,”alisema Agines.

Akizungumzia mifumo ya hali ya hewa, Agnes, alisema katika kipindi cha Machi hadi Mei mwaka huu kunatarajiwa kuwa na ongezeko la joto la bahari katika eneo la Tropikali kati ya Bahari Pasifiki.

Alisema hali hiyo ya jotola juu ya wastani linatarajiwa katika ukanda wa Magharibi mwa Bahari ya Hindi (Pwani ya Afrika Mashariki) na Mashariki mwa Bahari ya Hindi (Indonesia).

Agnes alisema hali hiyo itasababisha upepo kutoka mashariki utakaombatana na unyevunyevu hafifu wa hewa yenye unyevunyevu kutoka katika misitu ya Kongo kuelekea maeneo ya magharibi mwa nchi, mikoa ya kanda ya kati kuna nyanda za juu kusini-magaribi na hivyo kusababisha upungufu wa mvua katika maeneo hayo.

 Mkurugenzi wa Usalama wa Chakula, Karim Mtambo, alisema kutokana na utabiri huo anawashauri wakulima wa maeneo ya Kanda ya ziwa Victoria kuandaa mashamba na pembejeo mapema na kuzingatia ushauri wa wataalam wa kilimo kwa matumizi sahihi ya ardhi na mbegu.

“Katika baadhi ya maeneo ya nchi hususan kanda ya ziwa Victoria nyanda za juu kusini magharibi na maeneo ya mkoa wa Mtwara hali ya unyevunyevu wa udongo, tunautarajia kuwa ya utatosheleza katika shughuli za kilimo,”alisema Mtambo.

Mtaalam wa Afya, kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Jubilata Bernad, alisema katika kipindi hicho cha mvua, menejimenti ya maafa na wadau wengine wanashauriwa kuchukua hatua stahiki katika utunzaji wa mazingira, upatikanaji wa majisafi na salama na usambazaji wa dawa, maji na chakula ikiwa ni hatua za  kujiandaa na kukabiliana majanga yanayoweza kutokea.

No comments:

Post a Comment