KAMA UNA TUKIO LOLOTE LA KIJAMII, SIASA, UCHUMI TUWASILIANE KWA E-mail: shehesemtawa@gmail.com SIMU: 0719 352 268

Thursday 26 March 2015

PINDA AWAONYA WANA SIASA KUHUSU GESI ASILIA

Waziri Mkuu, Pinda akiteta jambo na Mkurugenzi Mtendaji wa Repoa, Prof. Samweli Wangwe
WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda, amewaonya viongozi kujiepusha kuingia kwenye mtego wa kutumia rasilimali kama gesi asilia kwa manufaa yao binafsi.

Pinda alitoa onyo hilo jijini Dar es Salaam juzi  alipokuwa akifungua mkutano mkuu wa 20 wa Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Umaskini (Repoa), uliokuwa ukijadili ni namna gani rasilimali zilizopo zinavyoweza kulinufaisha taifa. 

Alisema kama wapo viongozi hasa wanasiasa wanaodhani kupatikana gesi utakuwa mwanzo wa wao kutumia rushwa ili wajinufaishe, watambue kuwa watakapofanya hivyo wanaweza kuingiza nchi katika migongano ya kijamii.

“Rasilimali hizi na hasa hii ya gesi kupatikana kwake inaweza ikawa ni bahati, lakini pia ikawa laana,  inaweza ikawa hivyo kama viongozi hasa sisi wanasiasa tutashindwa kuisimamia  kwa manufaa ya Watanzania,” alisema Pinda.

Aliyekuwa waziri wa viwanda na biashara, Mbunge wa Moshi Vijijini, Dk. Cyirl Chami, aliitaka serikali kujisimamia katika suala zima la gesi huku wageni wawe wanatoa utaalamu na ushauri. 
“Gesi ni zao muhimu kwa Watanzania, ila ni muhimu tukajifunza kujisimamia wenyewe katika rasilimali zetu, hapo ndipo tunaweza kuona faida ya gesi,” alisema. 


Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Repoa, Prof. Samweli Wangwe, alisema taasisi hiyo ipo tayari kuisaidia serikali kuhakikisha mambo yanayohitaji utafiti na utaalamu wa gesi yanafanyika ili kuhakikisha uchumi wa Watanzania unakua.

No comments:

Post a Comment