KAMA UNA TUKIO LOLOTE LA KIJAMII, SIASA, UCHUMI TUWASILIANE KWA E-mail: shehesemtawa@gmail.com SIMU: 0719 352 268

Wednesday 22 April 2015

BODABODA WAKIMBIZANA NA POLISI WA 'TIGO' FIRE

VURUGU zimezuka leo eneo la Fire wilayani Ilala, Dar es Salaam, baada madereva wa bodaboda kuwataka askari polisi kumpeleka hospitali mwenzao aliyeumia mguu kutokana na kipigo cha askari hao.
 Askari hao wanadai kuwa walikuwa wakitekeleza tamko la serikali la kuwataka madereva wa bodaboda na bajaj kutoingia katikati ya jiji.
 Machi mwaka 2009, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilifanya marekebisho katika Sheria ya Leseni za Usafirishaji ya Mwaka 1973 ambapo pikipiki za kawaida na za magurudumu matatu maarufu kama Bajaj kwamba zimeruhusiwa kuwa moja ya vyombo vya usafiri vilivyoruhusiwa kutoa huduma ya kubeba abiria kwa malipo au kukodi.
Baada ya marekebisho ya Sheria hiyo, Mamlaka ya Usafiri wa Majini na nchi Kavu (Sumatra) ilitengeneza kanuni mpya kwa ajili ya utekelezaji zilizojulikana kama "The Transport Licensing (Motor cycles and Tricycles) Regulations, 2010.
 Akizungumza na wandishi wa habari jijini leo, James Christopher, ambaye alikuwa ni miongoni mwa mashuhuda wa vurugu hizo, alisema chanzo cha vurugu hizo ni uonevu wa polisi hao wa wanaofanya doria kwa kutumia pikipiki ‘Tigo’.
 “Tatizo limekuja baada ya dereva wa bodaboda kupigwa na askari, kuachwa akiwa ameanguka ndani ya mtaro wenye maji machafu kule Jangwani, wenzake walipoona hivyo, walimwinua kutoka kule na kumleta  hapa Fire na kuwabwagia askari hao wampeleke hospitali, ambapo walidai kuwa amevunjika mguu lakini mimi sikuona jinsi alivyovunjika,” alisema Christopher.
 Alisema, baada ya kumfikisha kwa askari hao yalizuka mabishano kati yao na madereva wa bodaboda ambao walikuwa wakilazimisha mwenzao apelekwe hospitali kwa vile askari hao walimuumiza na kumtelekeza.
 Christopher, alisema inavyonekana askari hao hawakupendezwa na hatua hiyo, hali iliyowafanya waanze kuwafukuza madereva hao wa bodaboda.
 Aliongeza kwa kusema kuwa kitendo hicho kiliongeza hasira kwa madereva wa bodaboda ambao walikuwa wakiongezeka, huku wakijibu kwa kuwarushia mawe askari.
 Christopher, alisema baada askari kuona hali inazidi kuwa mbaya iliwabidi wanze kufyatua risasi za moto hewani huku madereva na askari hao wakikimbia hovyo.
 “Hali ilikuwa inatisha, unaambiwa hata trafiki aliyekuwa akiongoza magari pale Fire alikimbia kwa ajili ya kupata msaada kwa wenzake,” alisema Christopher.
Alisema wakati vurugu hizo zikiendelea madereva hao wa bodaboda wakalipiga mawe gari la serikali namba STL 156 ambalo wandishi walilishudia ilikiwa Kituo cha Polisi Msimbazi.
 Shuhuda huyo, alisema baada ya purukushani hizo polisi waliondoka na dereva wa bodaboda aliyeumia ambapo haikufahamika mara moja kuwa wamempeleka wapi.
 Hata hivyo, baada ya askari hao kuondoka, muda mfupi zilifika gari nne za polisi zikiwa zimewabeba baadhi ya viongozi wa polisi hao ambao walionekana kuorodhesha majina ya askari ambao walianzisha mabishano na madereva hao wa bodaboda.
 Alipotafutwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (ACP), Lucas Mkondya, ili kutoa ufafanuzi juu ya tukio hilo alijibu kwa ufupi kuwa atatoa taarifa siku ya kutoa taarifa.

“Tutawaambia lakini kwa sasa hivi sijapata kitu cha kuaambia, tutakapokamilisha tutawaambia,” alisema Kamanda Mkondya.


No comments:

Post a Comment