JUMUIYA ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT), imeituhumu Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA) kwa kuendesha vitendo vya ufisadi bandarini kwa kushirikiana na
wakala wanaohusika na forodha.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo, Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo,
Johnson Minja, alisema kuwa sheria ya ulipaji kodi haiwapi nafasi wafanyabiashara kujua kiwango halisi
cha ulipiaji mzigo bandarini.
Alisema wafanyabiashara wanapoaingiza kontena moja hulipia shilingi
milioni 40 huku risiti ikionyesha kuwa kontena hilo limelipiwa shilingi milioni
10.
Minja alisema kuwa serikali inapoteza mapato kupitia mikono ya watu
wachache walioaminiwa na serikali kuifanya kazi hiyo.
“Sheria haikupi nafasi ya kujua ni
kiwango gani unatakiwa kulipia, hapo unalazimika kumfuata wakala wa
forodha ambaye anakupangia bei ya kulipia,” alisema.
Minja alisema wafanyabiashara
walianza kupinga kitendo hicho cha ulipaji kodi usioeleweka kwa muda mrefu
lakini serikali haikuwasikiliza.
“Tunataka serikali iweke mfumo ulio wazi wa ulipaji kodi kwa
wafanyabiashara kama ilivyo kwa ulipaji kodi wa magari ili iweze kunufaika,
tofauti na ilivyo sasa ambapo kwa sasa wanaonufaika ni watu wachache, tuna nia
ya dhati ya kulipa kodi kwa serikali
yetu,” alisema Minja.
Aliongeza kuwa migorogo ya wafanyabiashara na serikali inatokana na kutosikilizwa
kilio chao cha muda mrefu, hivyo wanataka kulipa kodi halisi kwa serikali ili
iweze kupata pato.
Minja alisema serikali
itilie mkazo jambo hilo ili kuondokana
na mambo yanayosababisha migogoro ya mara kwa mara baina yao na wafanyabiashara.
Alisema kuwa ataendelea kutoa elimu kwa wafanyabiashara na kuishauri
serikali juu ya mfumo wa ulipaji kodi utakaozidi kuinufaisha Tanzania, ambayo
inaingiza fedha nyingi kuliko nchi za jirani zinavyoingiza kupitia kodi.
“Lazima tufike mahali tuangalie kwa dhati suala hili ili kuweza
kuepuka migogoro isiyo na tija kwa taifa letu,” alisema.
Minja aligusia kufutwa kwa dhamana yake ya awali kuwa kulitokana na
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George
Masaju, hakupitia faili lake vizuri kabla ya kufuta dhamana hiyo.
Alisema amemsamehe Masaju na hana kinyongo pia hatadai fidia kwa
mambo yaliyotokea.
Alisema sababu ya kufutiwa dhamana yake ya awali ni kutokana na
wafanyabiashara wengi kufika mjini Dodoma kusikiliza kesi yake.
Minja alipewa dhamana juzi ya masharti ya kuwa na mdhamini mmoja
ambaye ni mfanyakazi wa serikali anayeishi Dodoma, aliyesaini bondi ya shilingi
milioni nne.
Minja alifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Dodoma Januari 28,
mwaka huu kwa kosa la uchochezi na kuwashawishi wafanyabiashara wasilipe kodi
kwa kutumia mashine za kielektroniki (EFDs).
Kesi hiyo itaanza kusikilizwa kwa maelezo ya awali Aprili 9, mwaka
huu kutokana na ushahidi wa kesi hiyo kukamilika.
Akijibu malalamiko hayo, Ofisa Mkuu wa Huduma na Elimu wa TRA, Julius
Mjenga, alisema kuwa wafanyabiashara wana vyama vyao hivyo kama kuna jambo
linawatatiza wanaweza kuonana na Kamishna wa Forodha ili watafute ufumbuzi.
Alisema kuwa wanafanya kazi na wakala waliosajiliwa kisheria na
kwamba sheria zao zipo wazi.
Aliongeza kuwa sheria ya bidha haiwezi kuwa sawa na ili ya magari,
kwa kuwa wafanyabiashara wanatakiwa kuonyesha nyaraka za mizigo waliyoingiza.
Aliwataka wafanyabiashara kushirikiana na TRA kufuatilia na kamishna
atachukua hatua sitahiki.
Juzi wakati akitoa hotuba
ya kuahirisha Bunge, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alitoa wito kwa wabunge na
viongozi wengine nchini kushirikiana na serikali kuwaelimisha wananchi na wafanyabiashara
kuhusu manufaa ya matumizi ya mashine za kielektroniki za EFDs.
Pinda alisema elimu hiyo
itasaidia kujenga tabia ya kufanya biashara kwa kutunza kumbukumbu za mauzo ili
Tanzania iweze kufikia maendeleo endelevu kwa
wananchi kulipa kodi stahiki.
No comments:
Post a Comment