KAMA UNA TUKIO LOLOTE LA KIJAMII, SIASA, UCHUMI TUWASILIANE KWA E-mail: shehesemtawa@gmail.com SIMU: 0719 352 268

Sunday 5 April 2015

MTANZANIA AKAMATWA KWA MADAI YAKUSHIRIKI UGAIDI NCHINI KENYA

Ummul-Khayr Sadir Abdul (19).
VYOMBO vya usalama nchini Kenya, vinawashikilia wasichana watatu akiwamo Mtanzania, kwa kile kunachodaiwa kutaka kujiunga na kundi la kigaidi la al-Shabaab huko Somalia.
Taarifa kutoka kwa Kamishna wa Polisi Jimbo la Mombasa, Nelson Marwa amesema Mtanzania aliyekamatwa, alijieleza kuwa ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Afrika, Sudan.
Mtanzania huyo, Ummul-Khayr Sadir Abdul (19), mwenyeji wa Zanzibar, anatajwa kuwa kiongozi wa kundi hilo lililopanga kujiunga na al-Shabaab.
Wasichana wengine waliokamatwa pamoja na Ummul-Khayr, ni Maryam Said Aboud na Khadija Abubakar Abdulkadir wote raia wa Kenya.
“Hawa wasichana watatu, inaaminika kuwa walikuwa wanakwenda Somalia kupata mafunzo ya kigaidi na baadaye kufanya mashambulizi ya kujitoa mhanga,” alisema Kamishna Marwa.
Akizungumzia suala hilo, Kaimu Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai, DCI Diwani Athumani alisema: “Tunafuatilia hatujapokea taarifa zaidi ya hizo.”
Kamishna Marwa alisema raia hao wawili wa Kenya, mmoja ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mount Kenya kilichopo Thika, na mwingine ni mwanafunzi wa Sekondari ya Burhania, iliyopo Malindi, Kilifi.
“Serikali imepata taarifa kuhusu watu wanaokusanya watu kutoka Afrika Mashariki ili wakajiunge na makundi ya ugaidi nchini Somalia, wakala wetu wa usalama wamepata taarifa hizo na kufanikisha kukamatwa kwa wasichana hao,” alisema Kamishana Marwa. 
BBC

No comments:

Post a Comment