UMOJA
wa Vyama vya Madereva Tanzania, umetangaza kufanya mgomo usio na ukomo wa nchi
nzima kuanzia leo, kw amadai kwamba serikali imepuuza ombi lao la kukutana
walilotoa siku nne zilizopita ili kujadili madai yao ya msingi.
Akitoa
tamko la mgomo huo jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Umoja wa madereva
hao, Rashid Salehe, alisema kuwa kauli za dharau kutoka kwa baadhi ya viongozi
ndizo zilizowasukuma kugoma.
Alisema,
hivi karibuni Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta alikaririwa na baadhi ya vyombo
vya habari akisema kuwa madereva wapo wengi hivyo wasifanye migomo ya mara kwa
mara isiyo na madai ya msingi.
Saleh,
alisema Waziri huyo alitoa kauli ya dharau isiyowaridhisha na kuwakatisha tamaa
katika taaluma yao kwa kusema madereva wapo wengi na kwamba hupatikana kwa
urahisi kuliko wasichana wa kazi za ndani.
"Tumechaka
na kauli za kisiasa za viongozi wetu. Sasa tumaeamua hatutayatoa magari hadi
serikali itakapoamua kukaa meza moja na kusikiliza madai yetu," alisema.
Alisema
kauli za kisiasa ambazo hazitekelezeki, zimewachosha kwani wamekuwa wakiahidiwa
kwa muda mrefu bila ya madai yao kupatiwa ufumbuzi na badala yake wamekuwa
wakipigwa dana dana.
Aliongeza
kuwa leo watakuwepo katika kituo cha mabasi yaendayo mikoani na nje ya nchi ili
kuendelea na mijadala yao ya kutathimini maamuzi yao baada ya kuona wamepuuzwa
na serikali.
Naye
mwenyekiti wa umoja huo Clement Masanja, alisema kuwa kinachofuata baada ya
mgomo huo ni kurudisha leseni sehemu husika ili wakalime.
"Hatuwezi
kufanya kazi bila kuwa na mikataba inayotambulika kisheria, tunarudisha leseni
zetu ili wanaotaka kufanyakazi bila mikata waende wakachukue nafasi hizo,"
alisema.
Kwa
upande wake Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Madereva wa malori Tanzania, Shaban
Mdemu aliwatahadharisha baadhi ya dereva wenye leseni kwamba kwamba kwa siku ya
leo wasijaribu kutoa magari hadi mgogoro
huo utakapopatiwa ufumbuzi.
"Tumenyanyasika
vya kutosha tunawaomba Kamanda wa kikosi cha usalama Barabarani na Kamanda wa
Kanda Maalumu Kamanda Suleiman Kova kutupatia ulinzi kwa usalama wetu lakini
sio kutubuguzi," alisema Mdemu.
Mgomo
huo unafanyika baada ya siku nne zilizotolewa na uongozi wa umoja huo ulikutana
Aprili 29 mwaka huu kutoa mrejesho baada ya kukutana na Naibu Waziri wa Kazi na
Ajira, Dk. Makongoro Mahanga, Aprili 18, mwaka huu, kwa madereva wenzao na
kuyajadili majibu waliyoyapata kwa Naibu Waziri huyo.
Mrejesho
huo ni kwamba katika kikao walichokutana na Naibu Waziri Dk. Mahanga kulikuwa
hakuna jipya zaidi ubabaishaji.
Mgomo wa awali
Aprili
9 mwaka huu madereva hao waligoma wakiitaka serikali kuweka mfumo mzuri wa
ajira na kupinga kujerejea katika mafunzo kila baada ya mika mitatu.
Mafunzo
hayo yalitokana na Serikali kuifanyia marekebisho Sheria ya Usalama Barabarani
kwa kuingiza kipengele kinachowataka madereva kwenda Chuo cha Usafirishaji
(NIT), kwa mafunzo ya muda mfupi mara kila wakati leseni zao zinapoisha ili
kupata sifa ya kupata leseni nyingine.
Utaratibu
huo uliotangazwa Machi 30 mwaka huu, ulipingwa vikali huku madereva wakidai
kuwa hawakushirikishwa katika kuuandaa.
Madai
hayo ni pamoja na kuondolewa kwa ulazima wa kusoma kila baada ya miaka mitatu
na kujilipia gharama za mafunzo ambazo walidai ni Sh560,000 kwa magari ya
kawaida na sh. 200,000 kwa magari ya abiria.
Madereva
hao pia wanadai kuwa hawawezi kuhudhuria mafunzo hayo wakati hawana mikataba ya
ajira inayoweza kuwahakikishia kazi zao zinalindwa hadi wanapomaliza mafunzo.
Madai
mengine ni kuondolewa kwa faini ya sh.300,000 kwa kila kosa la barabarani,
Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchikavu (Sumatra) kuhakiki uhalisi
wa dereva anayeandikishwa na mmiliki wa chombo husika.
No comments:
Post a Comment