SIKU chache
baada ya Kituo cha Polisi cha Stakishari jijini Dar es Salaam kuvamiwa na watu
wanaosadikiwa kuwa ni majambazi, Jeshi la Polisi nchini limeunda kikosi maalumu
chenye askari waliopata mafunzo ya ziada kupambana na matukio ya aina hiyo.
Akizungumza
kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Ernest Mangu, wakati wa kuaga miili
ya askari waliouawa kwenye tukio hilo kwenye Kituo cha Polisi cha Kilwa Road
jijini Dar es Salaam jana, Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,
Suleiman Kova alisema kikosi hicho kimeundwa maalumu kutokana na aina ya
matukio ambayo yanaonekana ni zaidi ya ujambazi.
"Tukio
lile ni zaidi ya ujambazi na ni tukio kubwa kufanyika hapa jijini Dar es Salaam,
majambazi kwa kawaida huwa wanavamia sehemu ambayo kuna fedha au mali na huwa
hawazidi watano, lakini kwenye tukio lile walikuwa majambazi 16," alisema.
Askari
walioagwa jana ni D6752, Adam Nyamhangwa (50) ambaye atasafirishwa leo kwenda
kuzikwa kijijini kwao Korotange Tarime na E 1279 Coplo Peter Sabuni (51),
ambaye mwili wake utasafirishwa kwenda mkoani Mwanza.
Kamanda Kova
alisema jeshi hilo limejipanga kupambana kwa mbinu zote kuhakikisha wahalifu
waliohusika na tukio hilo wanakamatwa na
kwamba kikosi kilichoundwa na IGP kimekabidhiwa magari ya kufanya kazi usiku na
mchana.
Hata hivyo,
ibada hiyo ya kuaga marehemu hao haikuhudhuriwa na viongozi wa ngazi ya juu wa
jeshi hilo na Wizara ya Mambo ya Ndani kutokana na kile kilichoelezwa na Kamanda
Kova kuwapo kwenye vikao kulifanyia kazi
tukio hilo.
"Sisi
si wanasiasa bana! Nataka niwahakikishie kuwa tumefikia hatua nzuri ya
upelelezi kwenye tukio hili na si muda mrefu tutawaeleza hatua tuliyofikia
lakini kwa sasa niishie hapo maana nikiendelea nitaharibu uchunguzi
unaoendelea," alisema.
Kova
aliwataka askari kufanya kazi yao bila woga, kwani wanatakiwa kuwajibu wahalifu
hao kwa vitendo na wakae tayari kwa kujibu mapigo.
Awali , Kamanda
wa Mkoa wa Ilala, SACP Lucas Mkondya, alisema anataka tukio hilo liwe la mwisho
kwenye mkoa wake na amewataka wahalifu kutolilaumu Jeshi la Polisi kwa hatua
watakazozichukua.
Kituo cha
Polisi Stakishari kilicho Ukonga jijini Dar es Salaam kilivamiwa na majambazi
Julai 12 mwaka huu na kuwaua askari wanne na raia watatu.
CHANZO TANZANIA DAIMA
No comments:
Post a Comment