KAMA UNA TUKIO LOLOTE LA KIJAMII, SIASA, UCHUMI TUWASILIANE KWA E-mail: shehesemtawa@gmail.com SIMU: 0719 352 268

Wednesday 5 August 2015

RAIS JAKAYA KIKWETE ASAINI MUSWADA WA SHERIA YA MAFUTA NA GESI

Rais Jakaya Kikwete akitia sahihi sheria mpya ya usimamizi wa mapato ya mafuta na gesi jijini Dar es Salaam jana. Kushoto ni Waziri wa Fedha, Saada Mkuya.
RAIS Jakaya Kikwete amesaini miswada mitano ya sheria ikiwemo ule wa Sheria ya Mafuta na Gesi uliopitishwa hivi karibuni katika Bunge na kuleta mvutano hadi kufika hatua ya wabunge wa kambi ya upinzani kufukuzwa na wengine kususia vikao vya Bunge.
Miswada mingine ni Sheria ya Uwazi na Uwajibikaji, Sheria ya Usimamizi wa Mapato ya Mafuta na Gesi, Sheria ya Tume ya Walimu na  Sheria ya Masoko  ya Bidhaa.
Hafla ya utiaji saini ilifanyika jana Ikulu jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene, Waziri wa Fedha, Saada Mkuya na Waziri wa Elimu, na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa.
Katika Muswada wa Sheria ya Mafuta wa mwaka 2015, Waziri Simbachawene, alisema malengo ya sheria hiyo  ni kuimarisha usimamizi wa sekta ndogo ya mafuta ili kuhakikisha maslahi ya nchi katika tasnia ya mafuta yanalindwa kikamilifu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.
Nyingine alisema ni kuweka mfumo madhubuti wa kisheria utakaorahisisha usimamizi wa shughuli za mafuta katika mkondo wa juu, wa kati na wa chini kupitia sheria moja.
Simbachawene alisema moja ya masuala muhimu yaliyozingatiwa katika muswada huo ni pamoja na kuweka utaratibu ambao Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zitashirikiana katika shughuli za utafutaji, uchimbaji na uendelezaji wa vitalu vya mafuta na gesi katika yaliyo kwenye maeneo yanayogusa pande zote mbili.
Simbachawane alisema sheria ya uwazi na uwajibikaji katika rasilimali za madini, mafuta na gesi asilia Tanzania, imelenga kuweka utaratibu wa upatikanaji kwa wakati wa taarifa sahihi za malipo, mapato, mauzo na gharama za uwekezaji kutokana na shughuli za madini, mafuta na gesi asilia.
Huku mambo muhimu yaliyozingatiwa yakiwa ni pamoja na suala zima la kuweka wajibu kwa kampuni juu ya utoaji na uwekaji wazi taarifa na takwimu za malipo ya kodi, mauzo, gharama za uwekezaji katika shughuli za madini, mafuta na gesi asilia.
Pia kutakuwepo na taarifa kuhusu ushiriki wa Watanzania hususan katika matumizi ya huduma na bidhaa zinazopatikana nchini na gharama zilizotumika katika miradi ya jamii, hatua itakayolenga uwajibikaji kwa kampuni. 
Akizungumzia kuhusu sheria ya Masoko  ya Bidhaa, Waziri wa Fedha, Mkuya alisema unalenga kutekeleza kampeni ya Kilimo Kwanza ambapo kutakuwa na mfumo wa uwazi wa upatikanaji wa taarifa wa bei za mazao na suala zima la mfumo wa stakabadhi ghalani.
Naye Waziri Kawambwa alisema Sheria ya uanzishwaji wa Tume ya Walimu, utamaliza kilio cha muda mrefu cha walimu kuwa na chombo chao.

Katika hatua nyingine, Rais Kikwete jana aliwaapisha makatibu tawala wawili wa Mkoa wa Singida, Festo Kang'ombe na wa Shinyanga, Abdul Dachi.

No comments:

Post a Comment