KAMA UNA TUKIO LOLOTE LA KIJAMII, SIASA, UCHUMI TUWASILIANE KWA E-mail: shehesemtawa@gmail.com SIMU: 0719 352 268

Thursday 6 August 2015

SHEHENA YA MENO YA TEMBO YAKAMATWA USWISI

Waziri wa Maliasili na Utalii, Nyalandu
SHEHENA ya masanduku ya meno ya tembo yenye uzito wa kilo 262 ambayo yanadaiwa kutoka nchini Tanzania yamekamatwa juzi jijini Zurich, Uswisi.
Kwa mujibu wa taarifa iiyochapishwa na gazeti la The Guardian la Uingereza jana, ilieleza kuwa shehena hiyo inayokadiriwa kuwa na thamani ya euro 265,000 (sawa na sh. bilioni moja za Tanzania ) ilikamatwa Julai 6, mwaka huu huku raia watatu wenye asili ya China wakiwekwa chini ya ulinzi.
Taarifa hiyo ilibainisha kuwa idadi hiyo ya shehena ilikuwa na vipande 172 vya meno ya tembo, yanayokadiriwa kuwa ni ya kati ya tembo 40 hadi 50.
Taarifa hiyo ilimnukuu Ofisa Mkuu wa Idara ya Forodha wa Uwanja wa Ndege wa Zurich nchini humo, Heinz Widmer, aliyesema shehena hiyo ilikuwa ikisafirishwa kutoka Tanzania kupitia Uswisi kisha kupelekwa Beijing, China.
Widmer alisema kuwa katika shehena hiyo kulikuwa na kilo moja ya kucha za simba ambayo ni sawa na kucha 35 pamoja na meno 21 ya mnyama huyo.
Tanzania Daima ilimtafuta Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, kwa njia ya simu yake ya kiganjani ili kuzungumzia tukio hilo ambapo simu yake ilipokewa na Katibu wake, Imani Nkuwi, ambaye alisema kiongozi huyo yupo kwenye kikao.
Hata hivyo gazeti hili ilimtafuta Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk. Adelhelm Meru, aliyesema suala hilo linafanyiwa kazi na Polisi wa Kimataifa (Interpol).
Alisema kuwa hivi sasa uchunguzi unafanyika ili kuweza kuthibitisha iwapo shehena hiyo ilitokea hapa nchini.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Waziri Nyalandu jana  jioni ilithibitisha kutokea kwa tukio hilo huku akiupongeza Uwanja wa Ndege wa Zurich na Serikali ya Uswisi kwa kubaini nyara hizo.
Taarifa hiyo ilisema kuwa wizara imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa hiyo kwa kuwa tukio hilo linadhihirisha kwamba ujangili bado unaendelea licha ya juhudi za serikali za kupambana kwa kushirikiana na  jumuiya za kimataifa za kupambana na ukatili huo wa wanyama. 
“Wizara inapenda kuuhakikishia umma kuwa sisi kama nchi tunafanya na kutumia jitihada zote kupambana na vitendo vya ujangili unaotishia kutoweka kwa rasilimali za wanyamapori wetu,” ilisema

Ilisema kuwa wizara imeanza kufanya uchunguzi wa tukio hilo ikiwemo Mamlaka husika ya Viwanja vya Ndege (TAA) pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama  ili kuchukua hatua stahiki dhidi ya wote watakaobainika kuhusika na kadhia hiyo.

CHANZO TANZANIA DAIMA

No comments:

Post a Comment