KAMA UNA TUKIO LOLOTE LA KIJAMII, SIASA, UCHUMI TUWASILIANE KWA E-mail: shehesemtawa@gmail.com SIMU: 0719 352 268

Saturday 6 February 2016

SHIVYATIATA: SHAKA OMBA RADHI NDANI YA SIKU SABA



SHIRIKISHO la Vyama vya Tiba Asili Tanzania (SHIVYATIATA), limemempa siku saba Mwenyekiti wa Baraza la Waganga Tanzania (BAWATA), Shaka Mohamed kuomba radhi baada ya kuupotosha umma kuhusu kazi yao.
Kauli hiyo imekuja siku chache baada ya BAWATA, kudai eti hivi sasa kumeibuka kundi la wafanya biashara wanaotumia kivuli cha Dawa Asili kwa kutoa huduma za Tiba Asili, ambao wanajiita watabibu wa Dawa Asili.
Kwa mujibu wa Tamko kwa vyombo vya habari liliyosainiwa na Mwenyekiti wa Taifa wa SHIVYATIATA, Abdulrahman Lutenga, imebaini kuwa mtoaji wa taarifa hiyo aliamua kwa makusudi kuupotosha Umma kitendo ambacho hakikubaliki.
Lutenga, alisema wamefikia hatua baada ya kugundua kuwa Shaka alitoa kauli hiyo bila ya kufanya utafiti wa kutosha na pia hakujielekeza kwenye sheria no 23 ya Tiba Asili na Tiba Mbadala ya mwaka 2002 ambayo inatambua kuwepo wauza dawa, watengeneza dawa, na waganga wa Tiba Asili na wakunga wa Tiba Asili na wasaidizi wao.
“Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na chama cha waganga kinachojulikana kwa jina la (Bawata), taarifa hiyo waliyotoa tarehe 29/01/2016 katika kufuatilia taarifa hiyo Shirikisho la Vyama vya Tiba Asili Tanzania tumegundua kuwa mtoaji wa taarifa hiyo Shaka amepotosha umma,”alisema Lutenga.
Alisema kutokana na upotoshaji huo wanamtaka Shaka  atekeleze na kuthibitish kauli yake kwamba ni kwa jinsi gani Mweneyekiti wa SHIVYATIATA, alivyotumiwa na kundi hilo hadi kufikia hatua ya kuwatetea.
“Tunampa siku saba kuanzia Februari 3 mwaka huu ikiwa atashindwa kuthibitisha tunamtaka aombe radhi kwa mwenyekiti wa SHIVYATIATA na shirikisho kwa ujumla kwa kitendo chake cha kuchafua jina la kiongozi na taasisi kwa ujumla,”alisema Lutenga.
Aidha, Lutenga alisema alimtaka Shaka kuomba radhi kwa njia ile ile aliyotumia kwa kuzungumza na wandishi wa habari nchini.
Alisema endapo atashindwa kuomba radhi basi wanasheria wa shirikisho hilo na wale wa binafsi wataelekezwa kumfikisha mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.

No comments:

Post a Comment