RAIS John Magufuli amewasamehe wafungwa 3,551, ikiwa ni sehemu
ya maadhimisho ya miaka 52 ya Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar, ambao
umeasisiwa Aprili 26 mwaka 1964.
Lengo la serikali katika msamaha huo ni kuona wafungwa walioachiliwa
huru wanarejea tena katika jamii, kushirikiana na wenzao katika ujenzi wa Taifa
na kwamba watajiepusha kutenda makosa ili wasirejee tena gerezani.
Katika taarifa yake hiyo kwa vyombo vya habari na kusainiwa
na Meja Jenerali Projesta Rwegasira, alisema msamaha huo wa Rais hautawahusu
wafungwa waliohukumiwa kunyongwa, kifungo cha maisha, makosa ya dawa za
kulevya, rushwa na wale waliyojihusisha na mashambulizi, ukatili dhidi ya watu
wenye ualbino na waliyowapa mimba wanafunzi.
Alisema Rais Magufuli ametumia madaraka yake aliyopewa
chini ya Ibara ya 45 (1) (d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Rwegesira, alisema wafungwa hao wapatao 3551 watafaidika na
msamaha huo, baada ya kupunguziwa moja ya sita ya vifungo vyao ambapo 580
wataachiliwa huru na wengine 2,971 watanufaika na kubaki gerezani wakitumikia
sehemu ya kifungo chao kilichobaki.
Aliwataja wafungwa waliyonufaika na msamaha huo kuwa ni
pamoja na wagonjwa wa Ukimwi, Kifua Kikuu (TB) na saratani.
“Wafungwa hawa ni wale ambao wamethibitishwa na Jopo la
waganga chini ya uenyekiti wa Mganga Mkuu wa Mkoa na wa Wilaya,”alisema.
Wengine ni wazee wenye umri wa miaka 70 au zaidi, wanawake
waliyoingia gerezani huku wakiwa wajawazito pamoja na wale waliyoingia na
watoto wanaonyonya na wasiyonyonya.
Pia, aliwataja wengine kuwa ni kundi la watu wenye ulemavu
wa mwili na akili.
Aidha, alisema msamaha huo wa rais hautawahusu wafungwa
wanaotumikia kifungo kwa makosa ya unyang’anyi na unyang’anyi wa kutumia silaha.
Kundi lingine ni wanaotumikia kifungo kwa makosa ya
shambulio la aibu kama vile kunajisi, kubaka, na kulawiti, au akujaribu kutenda
makosa hayo.
Rwegasira alisema wafungwa wanaotumikia kifungo chini ya
Sheria ya Bodi ya Parole (Act. No. 25/1994) na Sheria ya Huduma kwa Jamii
(Act.No.6/2002) na wale waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo kwa makosa
ya kutumia vibaya madaraka yao nao hawahusiki na msamaha huo.
No comments:
Post a Comment