KAMANDA WA KANDA MAALUM, SIMON SIRRO |
MAGENGE ya uhalifu maarufu kama ‘Panya Road’ yameendelea
kuvamia mitaa, safari hii ikiwa Manzese- Kibamba na Msakuzi- Mbezi wilayani
Kinondoni jinini Dar es Salaam, ambapo ndani ya wiki moja iliyopita yameua watu
wawili na kujeruhi kwa kutumia silaha za moto.
Hata hivyo, Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni amesema
kama magenge hayo yamefikia hatua ya kutumia silaha za moto basi yatakuwa ni
majambazi hivyo ameyataka yakatafute kazi nyingine halali kwani hata kubali
kuona yanaendelea kunyanyasa wananchi.
Magenge hayo hujulikana
kwa majina tofauti katika mtaa husika, mfano mbwa mwitu, machizi 70,
watoto wa mbwa, Hapa Kazi Tu, na wadudu wa dampo.
Ndugu wa marehemu hao kwa nyakati tofauti walisema magenge
hayo hivi sasa yanafanya unyama huo kwa kujiambini kana kwamba hakuna vyombo
vya usalama.
Akizungumzia tukio la mauaji ya Msakuzi Mbezi jana, ambalo
limetokea juzi Aprili 23 mwaka huu, mmoja wa mashuhuda, Amiri Masagati, alisema
Msonje Mnyampala (22), aliuawa baada ya
kupigwa risasi mgongoni wakati akikimbia genge hilo la wahalifu.
“Hiki kikundi kilituvamia muda wa saa 2:00 usiku kikiwa na
gari ambayo hakiujua ila ilikuwa Pickup, wakati tukiwa kijiweni tukinywa kawa
ndipo walipotuambia tulalale chini na kutuamlisha tutoe simu zetu na fedha
lakini wakati wanafika marehemu alikuwa amekwenda kujisaidia haja ndigo.
Mara baada ya kurudi na kuona tumelala chini ndipo
alipouliza kuna nini akajibiwa na wahalifu hao kwa kumtaka alale chini hata
hivyo akadhani ni utani lakini akabaini hali siyo shwari ndipo alipojaribu
kukimbia,”alisema Masagati.
Alisema baada ya kukimbia mmoja wa wahalifu hao alifyatua
risasi hewa kama ishara ya kumtaka kujisalimisha hata hivyo alizidi kukimbia
ndipo alipopigwa risasi ya mgongoni na kufariki papo hapo.
Aidha, Masagati alisema baada ya tukio hiyo, siku
iliyofuata Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa huo, ambaye hakumtaja jina pamoja na
Mbunge wa Kibamba (Chadema), John Mnyika walifika kutoa pole kwa wafiwa.
Mwili wa marehemu umesafirishwa juzi kuelekea nyumbani kwao
mkoani Dodoma kwa ajili ya mazishi.
Naye shuhuda wa tukio la Manzese Kibamba, ambaye hakupenda
kuandikwa jina lake gazetini, alisema tukio hilo la mauaji limetokea Aprili 17
mwaka huu baada ya kundi hilo lililokuwa na silaha za jadi na za motokuvamia
nyumba zaidi ya tano na kupora mali mbalimbali ikiwamo fedha.
Alisema, aliyeuawa katika tukio hilo alikwa ni jirani yake aliyetambulika
kwa jina la Julian Karangi ambaye alikuwa mwalimu na mmiliki wa shule ya
chekechea iliyoko Kibamba.
Shuhuda huyo alisema licha ya tukio hilo la kifo bado
wahalifu hao walimkata mkono mama mmoja ambaye alidai hakuweza kulipata jina
lake mara moja.
“Tulitoa taarifa polisi hata hivyo, walipofika
walikwishaondoka kwa kukimbilia katika pori ambalo halijaendelezwa na mmiliki wake
kwa muda mrefu ambapo walitokea kwenye kijiji cha Mpiji ambako waliendelea
walivamia nyumba moja moja,”alisema shuhuda huyo.
Aidha, shuhuda huyo alisema marehemu alizikwa juzi Aprili
23 mwaka huu katika kijiji hicho cha Manzese Kibamba wilayani Kinondoni jiji
Dar es Salaam.
Alipotafutwa Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni,
Christopher Fuime, ili kutoa ufafanuzi kuhusu uvamizi huo, alisema hakuwa na
taarifa zozote kuhusiana na matukio
hayo.
“Kama kuna panya road wanaotumia sialaha basi hao siyo
panya road bali huo ni ujambazi kwa sababu panya road hawana historia ya kuuwa
tangu walipoanza,”alisema Fuime.
Alisema kutokana na mazingingira hayo ya kutumia silaha za
moto anafikiri hilo ni kundi lingine kwa hiyo atalifanyia kazi kuanzia sasa na
kwamba ameahidi hata kubali kuona uhalifu unaendelea kutokea.
Wakati
huo huo Wakazi wa Kimanga wametahadharishwa kwamba wanaweza kufungwa ama
kulipishwa faini iwapo watashindwa kutoa michango kwajili ya uslinzi shirikishi
iwapo mkutano wa mtaa ukipitisha kulipwa kwa michango hiyo.
Mkuu
wa kituo cha Polisi Tabata, Mrakibu Msaidizi wa Polisi, Bakari Goti aliwasihi
wananchi kuharakisha michango ambayo itagharamia askari walioandaliwa
vinginevyo watakaokaidi kuchanga watafikishwa mahakamani.
Diwani
wa Kimanga ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mtaa wa Kimanga, Manase Mjema amewaonya
wananchi wa Kata hiyo juu ya kuweka ngoma za usiku zijulikanazo kama Kigodoro
katika sherehe na badala yake wametakiwa kufanya sherehe zao kwenye kumbi.
Akizungumza
na wananchi juzi, wakati wa uzinduzi wa kikundi cha Polisi Jamii, Diwani huyo
alisema kuwa ngoma hiyo mbali na kuwa kero imekuwa ikisanbaisha watu kuibiwa na
kuporwa mali zao kutokana na vijana wahuni kujiiingiza na kuvizia maeneo yaliyo
karibu na ngoma hizo.
No comments:
Post a Comment