KAMA UNA TUKIO LOLOTE LA KIJAMII, SIASA, UCHUMI TUWASILIANE KWA E-mail: shehesemtawa@gmail.com SIMU: 0719 352 268

Tuesday 28 April 2015

FARIJALA ASWEKWA JELA MIAKA 3



MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imemhukumu kifungo cha miaka mitatu jela, mpwa wa Mwekahazina wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Kigoma, Rajabu Maranda, Farijala Hussein baada ya kutiwa hatiani kwa makosa sita likiwamo la kujipatia sh. milioni 455 kwa udanganyifu.
Hukumu hiyo iliyochukua saa tatu ilitolewa jana na jopo la mahakimu watatu ambao ni Francis Kabwe, Projestus Kahyoza na Panela Mazengo.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mazengo alisema mshtakiwa atatumikia kifungo cha miaka mitatu jela kwa kila kosa.
Hata hivyo, adhabu hizo zitakwenda sambamba, hivyo mshtakiwa atatumikia kifungo cha miaka mitatu jela.
Mbali na hukumu hiyo, hakimu huyo alimtaka mshtakiwa huyo kurudisha fedha hizo.
Katika hukumu hiyo, Hakimu Mazengo alimwachia huru Maranda baada ya kutoonekana na hatia katika makosa mawili yaliyokuwa yakimkabili.
Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Wakili wa serikali, Pius Hilla, aliiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa mshtakiwa  kwa kuwa makosa aliyoyafanya yanachangia kuangusha uchumi wa nchi.
Kwa upande wake, Wakili wa utetezi, Majura Magafu aliiomba mahakama kumpunguzia adhabu mteja wake kwa kuwa  anategemewa na familia yake, pia anasumbuliwa na ugonjwa wa Shinikizo la Damu (BP).
Katika kesi hiyo, Farijala na Maranda walidaiwa kujihusisha na uwasilishaji wa hati za uongo Benki Kuu ya Tanzania (BoT) zikionyesha kampuni yao ya Kiloloma & Brothers imepewa idhini na kudai deni la kampuni ya nje ya M/S BC Cars Export huku wakijua si kweli.
Ilidaiwa kuwa katika udanganyifu huo, watuhumiwa hao walijipatia sh. milioni 455 kutoka katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA).

No comments:

Post a Comment