Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta |
WAZIRI wa Uchukuzi, Samuel Sitta, ameonyesha wasiwasi wake kuwa iwapo
Katiba inayopendekezwa haitapitishwa na kuchangia Uchaguzi Mkuu kufanyika kwa
kufuata Katiba ya zamani, kuna uwezekano wa kutokea vurugu katika uchaguzi huo
unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
Akifungua mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa wizara hiyo uliofanyika
jana jijini Dar es Salaam, Sitta alisema wapo baadhi ya Watanzania wanaoikataa
Katiba hiyo bila kueleza mbadala wake uliko.
“Unapokikataa kitu ni lazima
ueleze mbadala wa kitu unacho kikataa ni nini, na unaposema Katiba hii ni
batili, tueleze iko wapi ambayo si batili. Katiba hii isipopitishwa na tukaenda
kwenye uchaguzi kwa Katiba ya zamani, bila shaka tunaandaa vurugu nchini ambazo
hazina sababu,” alisema.
Sitta alisema kuwa kundi linalopinga Katiba inayopendekezwa ndilo
lililokuwa la kwanza kupinga Katiba inayotumika sasa.
“Watu wanaoikataa Katiba inayopendekezwa ndio walewale waliokuwa wanaikataa
kwa nguvu zote Katiba inayotumika hivi sasa…hao hao ndio watakaogeuka baadaye
kupinga matokeo ya uchaguzi kwa madai Katiba iliyotumika haikuwa na sifa,” alisema
Sitta.
Aliwataka wajumbe wa baraza hilo kuisoma vema Katiba inayopendekezwa
ili waweze kuipigia kura kutokana na kuwa na masuala ya msingi na yenye masilahi
kwa taifa.
Mkutano huo ulikuwa mahususi kwa ajili ya kuwachagua katibu na msaidizi
wa baraza hilo pamoja na kujadili maandalizi ya bajeti ya wizara hiyo
inayotarajiwa kujadiliwa kwenye Bunge la Bajeti linalotarajiwa kufanyika mwezi ujao.
Awali akimkaribisha Sitta, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Shaaban
Mwinjaka, alisema wizara hiyo imekuwa na changamoto kubwa ya bajeti finyu
ambayo inayumbisha baadhi ya kazi za wizara hiyo na kushindwa kutekelezwa.
Akitoa mfano wa kwenye sekta ya anga, Mwinjaka alisema walipeleka
maombi ya fedha kwa ajili ya kununua rada za kuongoza ndege mbili, ambayo Tume
ya Mipango iliyapitisha, lakini hadi leo hawajaingiziwa fedha.
“Tanzania pamoja na ukubwa wake huu ina rada moja tu, na hii si nzuri
kwa masuala ya usalama kwenye sekta hii, hasa ukilinganisha na jirani zetu kama
Kenya, wana rada sita, Burundi na Rwanda zaidi ya rada nne lakini sisi rada
moja, hii si sawa,” alifafanua.
No comments:
Post a Comment