KATIBU wa Itikadi na Uenezi wa
Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye, ameitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi
(NEC) kuwawekea vijana mazingira bora ya uandikishwaji katika daftari la kudumu
la mpigakura, ili washiriki uchaguzi mkuu ujao.
Akizungumza katika Uwanja wa
Stakishari wakati wa tamasha la vijana lililoandaliwa na Mfuko wa Elimu wa
Bonnah, Dar es Dar Salaam jana, Nape
alisema tume hiyo ichukue hatua ya kuwaangalia vijana na kuwawekea mazingira
bora ili wasipoteze haki yao ya msingi.
“NEC iandae dawati maalumu la
vijana kwa lengo la kuwarahisishia kujiandikisha katika daftari hilo na pia waepuke
kuwauliza maswali magumu ambayo yatawakatisha tamaa na kushindwa
kujiandikisha,”alisema.
Nape aliongeza kuwa ni vyema
wajumbe wa NEC wakaangalia ratiba ya vijana kwa ajili ya kujiandikisha na
kwamba itawafanya wajitokeze kwa wengi kujiandikisha katika daftari hilo.
Alisema wanasiasa wamekuwa
wakiwatumia vijana kwa masilahi yao
binafsi bila kuangalia kwa kina kuwa
ndiyo tegemezi kwa taifa.
Nape aliwataka vijana kutojiingiza
katika makundi ya ushabiki na badala
yake washirikiane na kushawishiana kujiandikisha katika daftari la kudumu la
wapigakura.
Kwa upande wake, Diwani wa Kipawa,
Bonnah Kaluwa alisema vijana ndiyo nguvukazi inayotegemewa na taifa katika
kufanya uamuzi wenye tija ukiwamo wa kujiandikisha katika daftari la kudumu la
mpigakura.
Alisema kujiandikisha katika
daftari la kudumu la mpigakura ni haki ya kila mtu ili asipoteze nafasi ya
kuwachagua viongozi wanaofaa kumwongoza katika uchaguzi mkuu ujao.
Kaluwa, ambaye pia ni Mkurugenzi wa
Mfuko wa Elimu wa Bonnah alisema lengo la tamasha hilo ni kuwakusanya vijana
pamoja na kuelezana juu ya umuhimu wa
kujiandikisha katika daftari la kudumu la mpigakura.
“Mfuko wa Elimu wa Bonnaha umeona
kuna haja ya kuwaleta vijana sehemu hii ili kukumbusha umuhimu wa kujiandikisha
katika daftari la kudumu la mpigakura na hatimaye kuweza kupata nafasi ya
kushiriki katika uchaguzi mkuu ujao,”alisema Kaluwa.
No comments:
Post a Comment