WAFANYABIASHARA wenye
ulemavu wa Soko la Mchikichini, Karume wilayani Ilala, jijini Dar es Salaam
wamesema hawana mpango wa kuandamana tena kama walivyofanya siku tano
zilizopita.
Wafanyabiashara hao Mei 21mwaka
huu walifunga makutano ya barabara ya Uhuru na Kawawa wakipinga kitendo cha
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ilala kuwatuma polisi na mgambo wa jiji kwenda
kuvunja meza za kupangia biashara zao kwa madai kuwa eneo hilo sio rasmi wakati
akijua fika kuwa walipewa kwa maandishi mbele ya mwanasheria wa halmashauri
hiyo.
Kitendo cha askari hao kinadaiwa
kuwa kilisababisha upotevu wa mali za wafanyabiashara hao kwa vile kazi hiyo
ilifanyika kinyemela majira ya saa nne usiku bila ya wafanyabiashara hao
kuelezwa kama kungefanyika zoezi hilo.
Akizungumza na wandishi wa habari leo, Mwenyekiti wa Umoja wa Walemavu Dar es Salaam
(Uwawada), Mohamed Kidumke, alisema, hakuna maandamano na kwa kawaida hata
wanapotaka kuandamana hawana utaratibu wa kutoa taarifa bali wanashtukiza tu.
Alisema, hivyo kwa vile
hivi sasa wako katika mazungumzo na serikali ya kuwapatia eneo la kudumu ili
kuepuka mivutano ya mara kwa mara kati yao na serikali.
“Ijumaa tulikuwa na kikao
na Mkurugenzi, Mkuu wa Wialaya, Ofisa maendeleo na Jamii kwa ajili ya kujipanga
hasa kwa ajili mambo ambayo tuliyokuwa tukiya lalamikia lakini kubwa ilikuw ni
kuweka mikakati ya kutafuta eneo la kudumu ili kuondoa usumbufu ambao
unaonekana kujirudia rudia,”alisema Kidumke.
Alisema katika kikao hicho,
walipendekeza kupewa eneo ambalo ni zuri na linawafaa kwa kuendesha shughuli
zao, akibainisha kwamba wakipewa eneo hilo basi anaamini tatizo hilo litakuwa
limekwisha.
“Hatuwezi kulitaja kwa
sababu hivi sasa tuko katika majadiliano
kuhusu eneo hilo lakini yote hayo tumewaachia viongozi wa wilaya kwani wao ndio
wenye wajibu wakutupatia eneo hilo,”alisema Kidumke.
Kidumke, alisema
majadiliano yanaendelea leo kwa ajili ya kukukamilisha baadhi ya makubaliano
ambayo yatakuwa kwa maadishi ili yaweze kufanyiwa kazi haraka.
Kuhusu uhalibifu wa mali na
kuibiwa bidhaa zao, juzi, Kidumke, alisema kuwa mchakato wa kufanya tathimini
unaendelea na kuahidi kuwa haki itatendeka hivyo kuwataka wenzake kuwa
watulivu.
Aliongeza kwa kusema kuwa hivi
sasa wafanyabiashara hao wameruhusiwa kuendelea na shughuli zao hadi hapo
watakapopatiwa eneo la kudumu na kwamba hakuna atakayewabugudhi tena.
MWISHO
No comments:
Post a Comment