KAMA UNA TUKIO LOLOTE LA KIJAMII, SIASA, UCHUMI TUWASILIANE KWA E-mail: shehesemtawa@gmail.com SIMU: 0719 352 268

Wednesday 6 May 2015

SERIKALI YAFIKIA MUAFAKA NA MADEREVA WALIYOKUWA WAMEGOMA NCHI NZIMA

Askari wakiimarisha ulinzi kwenye eneo la ndani la kituo kikuu cha mabasi Ubungo, jijini Dar es Salaam jana, ambapo mara kadhaa vurugu zilikuwa zikitokea kabla ya kusitishwa kwa mgomo wa madereva wa mabasi.
JANA jioni, Tanzania Daima liliwasiliana kwa njia ya simu na Msemaji wa Umoja wa Madereva Tanzania, Rashid Saleh kutaka kujua walichokubaliana na alisema: “Tumeyamaliza na serikali imetupa siku 30 kuanzia leo (jana) yataisha.” Hivyo Juni 4 mwaka huu itakuwa mwisho wa siku 30.
Alisema baadhi ya mambo yatakayoshughulikiwa ndani ya kipindi hicho ni pamoja na mishahara na posho, bima ya afya, suala la kutokurudi darasani kusoma nalo limefutwa sanjari na mikataba yao kuandaliwa yenye ubora na si bora mikataba.
Salehe alisema mazungumzo yalikuwa mazuri na kwamba wamefurahi kwani katika kamati iliyoundwa ya watu 15 walipewa nafasi tano za uwakilishi. “Tutachaguana madereva wa bodaboda, malori, mabasi na wengine tutakaoona wanafaa,” alisema.
Alitaja viongozi waliohusika katika majadiliano hayo kuwa ni; Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta, Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Abdallah Kigoda, Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Makongoro Mahanga, Waziri wa Fedha, Saada Mkuya, Msaidizi wa Waziri Mkuu (hakumtaja jina lake), Waziri wa Mambo ya Ndani, Mathias Chikawe, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda na viongozi wa madereva. Kikao hicho kilifanyikia Ofisi ya Waziri Mkuu.
“Nimemaliza kuwatangazia wenzangu hapa sasa hivi (Ubungo) na kazi zinaendelea kama kawaida na tunachokisubiri sasa ni utekelezaji tu,” alisema.

CHANZO TANZANIA DAIMA


No comments:

Post a Comment