KAMA UNA TUKIO LOLOTE LA KIJAMII, SIASA, UCHUMI TUWASILIANE KWA E-mail: shehesemtawa@gmail.com SIMU: 0719 352 268

Wednesday 29 July 2015

BVR 3,717 ZAANDIKISHA WAKAZI 1,172,855

MASHINE 3,717 za kuandikisha wapiga kura kwa mfumo wa kielektoniki zimeandikisha wakazi 1,172,855 wa Jiji la Dar es Salaam huku muda wa kufungua vituo hivyo ukiongezwa kutoka saa 2 asubuhi hadi saa 1 asubuhi.
Maboresho hayo yalifanywa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), baada ya kuwepo kwa malalamiko ya wakazi wa jiji hilo, hali iliyotiliwa shaka huku wengine wakiomba muda wa uandikishaji uongezwe kutoka siku 10 za awali hadi siku 15 au zaidi.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu Damian Lubuva, alisema lengo la ofisi yake ni kuandikisha wakazi milioni 2.92 wa jiji hilo.
Akifafanua idadi ya walioandikishwa na wilaya zao, alisema: “Temeke tumeandikisha wapiga kura 389,558; Kinondoni wapiga kura 490,428 na Ilala wapiga kura 302,871,” alisema Jaji Lubuva alipokuwa akiwaeleza waandishi wa habari hatua iliyofikiwa na NEC katika uandikishaji.
“Shughuli ilianza vizuri japo kulikuwa na changamoto ya vifaa vya kutosha wakati wa kuanza kwa kazi ya uandikishaji ndiyo maana kulikuwa na malalamiko mengi kutoka kwa wananchi,” alisema.
Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo wa tume, idadi ya vifaa zikiwemo mashine za kuandikisha wapiga kura iliongezeka baada ya mashine zilizokuwa mikoani kuwasili jijini Dar es Salaam na kuendelea na uandikishaji katika Manispaa za Ilala, Temeke na Kinondoni.  
Alisema hadi sasa mashine zilizogawanywa katika kila halmashauri hizo na idadi yake ni Ilala yenye idadi ya vituo 395 ilipata mashine 927 sawa na asilimia 117; Kinondoni yenye vituo 702 imepata mashine 1,462 sawa na asilimia 104 huku Temeke yenye vituo 572 ikipata mashine 1,328 sawa na asilimia 116 na kufanya idadi ya mashine za BVR jijini hapa kufikia 3,717.
Kuhusu wale wanaojiandikisha kwenye vituo ambavyo si makazi yao, mwenyekiti huyo wa NEC alisema huo si utaratibu bora kwa kuwa kunaweza kuleta usumbufu wakati wa kupiga kura, hivyo kusisitiza kwamba watu wajiandikishe katika vituo vilivyopo wanakoishi. 
Alisema hakuna mwananchi mwenye sifa za kuandikishwa atakayekosa fursa endapo atafika kituoni huku akisisitiza kwamba hakuna sheria inayomlazimisha mtu kujiandikisha.


No comments:

Post a Comment