KAMA UNA TUKIO LOLOTE LA KIJAMII, SIASA, UCHUMI TUWASILIANE KWA E-mail: shehesemtawa@gmail.com SIMU: 0719 352 268

Friday 24 July 2015

BVR YAZUA KIZAZAA DAR


Baadhi ya wananchi wa eneo la Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam, wakiwa katika foleni ya kusubiri kupewa namba watakazotumia kuandikishwa katika Daftari la Wapigakura kwa kutumia mfumo mpya wa kielektroniki wa BVR, katika kituo cha Shule ya Msingi Ulingoni jana. 
WAKATI uandikishaji wapiga kura kwa kutumia mfumo mpya wa kielektroniki wa Biometric Voters Registration (BVR), ukiingia siku ya tatu jijini Dar es Salaam, hali imeendelea kuwa tete baada ya kuibuka kwa ngumi katika kituo cha Nunge, Kata ya Vijibweni, Kigamboni jijini hapa.
Baadhi ya watu pia walilazimika kutumia vyeti vya hospitali kuonyesha wanaumwa ili wapewe fursa ya kuandikishwa kwanza huku wengine wakiwabeba watoto wasio wao kwa lengo la kuonewa huruma na kuandikishwa mapema.
Wakati kila mmoja akibuni namna nzuri ya kuandikishwa mapema, katika  kituo cha Nunge ngumi zilitawala wakati wananchi waking’ang’ania nafasi ya kuandikishwa haraka.
Tukio hilo lilitokea jana saa tano asubuhi baada ya wakazi wa eneo hilo kulazimika kupanga foleni kwa muda mrefu wakisubiri kuandikishwa.
Wananchi hao ambao majina hayakuweza kufahamika mara moja walijikuta wakirushiana ngumi baada ya kuwepo kwa wenzao waliovuruga utaratibu wa kupanga foleni na kwenda kukaa mbele wakiwapita waliotangulia.
Kitendo hicho kiliwafanya wale waliowahi kwenye foleni kuamua kupambana na wenzao hali iliyosababisha vurugu zilizoacha majeraha na kumwagika kwa damu.
Vurugu hizo zilikwamisha zoezi hilo kwa muda kutokana na utulivu na amani kwenye eneo hilo kuwa tete.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Vijibweni, Jaffar Athumani, alikiri kuwapo kwa changamoto nyingi katika uandikishaji huo.
Alizitaja changamoto hizo kwamba ni mashine hizo kuchukua muda mrefu kuandikisha, ulinzi mdogo na vijana waliofikisha umri wa kuandikishwa katika daftari hilo kukataliwa kufanya hivyo.
“Mtu mmoja anaandikishwa zaidi ya dakika 20 na kwa huku Kigamboni kumekuwa na mwamko mkubwa wa watu kujitokeza kujiandikisha...lakini nimezungumza na Ofisa Mtendaji ili afanye utaratibu wa mashine moja itumike kwa makundi maalumu lakini wamekataa,” alisema.
Mbunge wa Kigamboni, Faustine Ndugulile, (CCM) alisema kazi ya uandikishaji imekumbwa na changamoto ya wingi wa watu na mashine kutokufanya kazi licha ya NEC kujitahidi kuweka vituo vingi.
Ndugulile aliwataka wananchi kuwa wavumilivu ili wapate haki yao ya msingi ya kujiandikisha katika daftari hilo.
wandishi walilitembelea vituo mbalimbali na kushuhudia kukithiri kwa msongamano wa watu na vurugu za kugombania kuandikishwa zikitawala.
Katika kituo cha Mwangaza, Gongo la Mboto, vurugu zilitawala majira ya asubuhi na kulazimika polisi zaidi ya watano kufika wakiwa na silaha kutuliza ghasia na uandikishaji ukaendelea.
Mmoja wa wakala wa kituo hicho, Ramadhan Mshinda, alisema vurugu hizo zilianza baada ya watu waliojitokeza juzi kujiandikisha kubaki na kutakiwa kufika jana ili waanze kuandikishwa kupingwa na wale waliojitokeza kwa mara ya kwanza hiyo jana.
“Unajua jana (juzi), kuna watu walibaki wakati tukiandikisha na kuwaambia wakija leo (jana) tutaanza nao lakini sasa wale waliofika leo (jana) wakagoma wakisema waanze wao na kweli wengine waliwahi ndipo vurugu zilipoanza na kusimamisha uandikishaji kwa muda,” alisema na kuongeza:
“Tuliamua kuwaita polisi na kufika kutuliza ghasia na uandikishaji ukaanze tena kwa kukubaliana kwamba wale waliobaki jana (juzi) tuwamalizie kwanza lakini bado kuna tatizo la BVR kuwa chache na kukatika kwa mtandao hali inayofanya foleni kuongezeka kuwa kubwa.”
Hali hiyo pia ilijitokeza katika vituo vya Mabibo na Tabata Kisiwani ambapo asubuhi baada ya wananchi kupanga foleni kulijitokeza kwa baadhi kutaka kujipenyeza kwenda mbele hali iliyosababisha vurugu ambazo hata hivyo hazikudumu zikamalizika.
Kutokana na kadhia hiyo, wakazi wa jiji hilo wameitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kufanya uamuzi mgumu wa kuomba msaada wa mashine zinazotumiwa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA). 
Katika baadhi ya vituo nyakati za asubuhi vurugu zilitawala na mistari mirefu ilipangwa na wananchi ambao tangu juzi wamekuwa wakijitokeza kwa wingi kuhakikisha wanaandikishwa huku maeneo korofi iliwalazimu Jeshi la Polisi kuingilia kati kurejesha utulivu.
Tatizo kubwa la mashine hizo za BVR kama ambavyo lilitokea mikoani wakati wa uandikishaji kwa kukatika kwa mitandao, kuharibika kwa mashine na baadhi ya waandikishaji kushindwa kuzimudu kwa siku za awali ndicho ambacho kimejitokeza jijini humo.
Uandikishaji huo unatarajia kudumu kwa siku 10 ambapo utamalizika Julai 31, mwaka huu na kwa mujibu wa takwimu za Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), inaonyesha makadirio ya idadi ya wapiga kura hadi kufikia Oktoba watakuwa milioni 24 nchi nzima huku Mkoa wa Dar es Salaam ukiwa na wapiga kura milioni 2.93.
Awali, Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu Damian Lubuva, alisema uandikishaji utakapoanza jijini humo BVR zote 8,000 zilizokuwa zikiandikisha mikoani zitarejeshwa Dar es Salaam ili kuufanya mchakato huo kumalizika ndani ya siku saba.
Tanzania Daima lilizunguka katika maeneo mbalimbali ya vituo jijini humo na kushuhudia nyuso za huzuni, kelele za hapa na pale na msongamano huku wananchi wakiitupia lawama NEC kwa kushindwa kupeleka BVR za kutosha katika maeneo yenye wakazi wengi ili kurahisisha uandikishaji huo.
Licha ya taarifa zilizotolewa awali kwamba kipaumbele kitatolewa kwa wazee, wanawake wajawazito na wenye mahitaji maalumu lakini nao walijikuta katika adha hiyo ya kupanga foleni kutokana na mashine za BVR kushindwa kufanya kazi kwa ufanisi.

Watoto, vyeti vyatumika

Baadhi ya wandishi walilidokezwa kuwa baadhi ya maeneo watu walilazimika kuomba kuwabeba watoto wasio wao ili waonewe huruma na kuruhusiwa kuandikishwa mapema.
Ujanja huo ulionekana kuwanufaisha baadhi ya watu katika hatua za awali lakini kadiri muda ulivyokwenda ndivyo watu waliokuwa kwenye foleni walivyokataa kuruhusu wenye watoto kuandikishwa haraka.
Hata hivyo binadamu hawaishiwi mbinu kwani katika maeneo mengine kuliripotiwa kuwa baadhi ya watu walifika vituoni wakiwa na vyeti vya hospitali kuonyesha ni wagonjwa wanaohitaji kuandikishwa haraka ili wakapumzike.
Watu hao walifika kwenye vituo hivyo na kuwaonyesha vyeti hivyo askari na baadhi ya watu waliokuwapo kwenye foleni ambao waliwaonea huruma na kuwapa kipaumbele cha kuandikishwa kwanza.

RC Dar alonga

Hata hivyo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiki, alikiri kuwapo kwa changamoto katika uandikishaji huo tangu ulipoanza na kuahidi kutafuta ufumbuzi haraka iwezekanavyo.
“Kwanza naomba radhi kwa wale wote waliopata usumbufu, napenda niwahakikishie kwamba tayari nimeshafanya mawasiliano na NEC na tayari imeshaongeza mashine, lakini tumeshauriana mashine hizo zitakwenda katika vituo vyenye watu wengi,” alisema Sadiki. 
Mkuu huyo wa mkoa aliwaomba wakurugenzi wa maeneo husika kuwachukulia hatua za haraka waandikishaji watakaobainika kufika katika vituo wakiwa wamechelewa.
“Sitaki kusikia watendaji waliopewa dhamana na wanaotumia fedha za serikali kwamba wanashindwa kufika kwa wakati katika vituo vyao, hivyo basi nawaomba wakurugenzi watakapombaini mtu, wamfukuze kazi mara moja,” alisema Sadiki.

NEC iiombe NIDA

Kutokana na upungufu wa mashine za BVR, baadhi ya wananchi waliitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuomba vifaa vinavyotumiwa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) katika uandikishaji wa vitambulisho vya uraia zitumike kuandikisha wapiga kura.
Mmoja wa waandikishwaji waliojitokeza katika kituo cha Kibamba, Ayoub Swalehe, alisema mashine hizo zina uwezo wa chini kabisa kwa vile haziwezi kuandikisha zaidi ya watu 50 bila ya kupumzishwa licha ya taarifa kwamba zina uwezo wa kuandikisha watu zaidi ya 100 kwa siku.
Swalehe alisema mashine  za NIDA zina uwezo mkubwa wa kuandikisha watu 150 kwa siku ukilinganisha na zile za NEC kwa sasa, kwa kuwa Dar es Salaam kuna watu wengi na siku zilizopangwa ni chache ni vema wakawaomba ili kufanya kazi hiyo ifanikiwe.
“Sioni dhambi kwa Idara mbili za serikali zinazofanya kazi inayofanana zikiungana kwa ajili ya kuwapunguzia wananchi usumbufu wa kukaa na kulala kwenye vituo vya kujiandikishia,” alisema Swalehe.
Mkazi wa Kibamba, Sofia Athuman aliyefika katika kituo cha Shule ya Sekondari Kibamba alisema siku ya kwanza waliandikisha watu zaidi ya 300, cha kushangaza waliopata kitambulisho hicho walikuwa watu 47 huku wengine wakitakiwa kurudi jana.
“Inasikitisha kwani wengine hapa ni watumishi kwa hiyo hii nenda rudi mwisho itatugombanisha na viongozi wetu huko ofisini,” alisema Sofia.

Uandikishaji urudiwe

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kimeitaka NEC kuangalia uwezekano wa kurudia mchakato huo wa uandikishaji wa BVR ili kutoa fursa kwa wale waliokosa fursa ya kujiandikisha ili watekeleze haki yao ya kikatiba.
Mtafiti na Mwandishi wa Taarifa za Haki za Binadamu, Paul Mkongoti, akitoa tafiti za nusu mwaka za kituo hicho kwa masuala mbalimbali yaliyojitokeza katika uandikishaji huo alisema umegubikwa na kasoro nyingi tangu zoezi lilipoanza, hivyo linaweza kusababisha Watanzania kunyimwa haki zao za kikatiba za kuandikishwa.
Mkongoti alizitaja baadhi ya kasoro kuwa ni kutokutolewa kabisa kwa elimu ya uraia juu ya kujiandikisha, kuwapo kwa vifaa vichache vya BVR, kuharibika mara kwa mara vifaa hivyo pamoja na kutozingatiwa kwa haki za walemavu.
“Hayo ni baadhi ya mapungufu ambayo yanasababisha malalamiko kutoka kwa wananchi kukosa fursa ya kujiandikisha, hivyo hali hiyo inawanyima haki Watanzania kushiriki katika mchakato huo,” alisema.


No comments:

Post a Comment